Merkel akutana na Li | Habari za Ulimwengu | DW | 07.01.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Merkel akutana na Li

Naibu Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang, yupo Ujerumani kwa ziara ya kikazi inayotarajiwa kuzaa matunda makubwa ya ushirikiano kati ya mataifa haya mawili na leo alitarajiwa kukutana na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel

Chansela wa Ujerumani, Angela Merkel, akiwa na mgeni wake Naibu Waziri Mkuu wa China, Li Kepiang, mjini Berlin, Ijumaa 7 Januari 2011

Chansela wa Ujerumani, Angela Merkel, akiwa na mgeni wake Naibu Waziri Mkuu wa China, Li Kepiang, mjini Berlin, Ijumaa 7 Januari 2011

Li Kepiang, Naibu Waziri Mkuu wa China, na mtu anayetarajiwa kuwa Waziri Mkuu ajaye wa taifa hilo kubwa barani Asia, anakutana hivi leo na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, katika mazungumzo ambayo yanatarajiwa kutuwama kwenye ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imesema kwamba kabla ya viongozi hao wawili kukutana, Li alitia saini kwa niaba ya nchi yake na makampuni ya Daimler na Volkswagen, muda mfupi tu baada ya Naibu Waziri Mkuu huyo wa China, kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle.

Wizara hiyo imesema kwamba mazungumzo kati ya Westerwelle na Li yalijikita zaidi kwenye juhudi za China kuleta mageuzi ya kisiasa. Vile vile, Li alipangiwa kukutana na Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Rainer Brüderle, ambaye katika mahojiano yake na gazeti la Handelsblatt, kabla ya mazungumzo hayo, alisisitiza juu ya umuhimu wa kufanywa mabadiliko makubwa kwenye soko la China ili kuwezesha viwanda vya Ujerumani kuingia kwenye soko hilo.

"Makampuni ya kigeni yanalalamikia ukosefu wa uwazi na umakini katika mfumo wa soko la China. Katika ziara yangu China, nilisikia malalamiko kwamba mara kwa mara sheria muhimu huanzishwa bila ya kushauriana na wadau muhimu wa uchumi." Alisema Brürdele

Baada ya kumaliza ziara yake nchini Ujerumani, Li anatarajiwa kuelekea nchini Uingereza, katika kile kinachotajwa kama jitihada za China kujiimarisha kiuchumi katika nchi za Magharibi. Tayari kiongozi huyo ameshaitembelea Hispania, ambako gazeti la nchi hiyo la El Pais, lilimnukuu kiongozi huyo akisema kwamba nchi yake iko tayari kulinunua deni la Hispania lenye thamani ya mabilioni ya Euro.

Baada ya Ugiriki na Ireland kujikuta zikilazimika kuchukua mkopo wa mabilioni ya Euro kunusuru uchumi wake, Uhispania na Ureno zinatazamiwa kufuatia miongoni mwa nchi 17 zinazounda umoja wa sarafu wa Euro. China inashikilia nafasi ya kwanza kwa usafirishaji wa bidhaa zake nje ya nchi, ikifuatiwa na Ujerumani, ambapo Ujerumani inakisiwa kusafirisha bidhaa zenye thamani ya Euro bilioni 37.3 kwenda China kwa mwaka 2009, huku China ikiingiza Ujerumani bidhaa zenye thamani ya euro bilioni 56.7.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE

Mhariri: Othman Miraji

DW inapendekeza

 • Tarehe 07.01.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/zuss
 • Tarehe 07.01.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/zuss

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com