1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel akutana na Abbas kujadili taifa la Wapalestina

Admin.WagnerD6 Mei 2011

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas, amekutana na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, katika jitihada za Rais Abbas kutafuta uungwaji mkono wa kuanzishwa kwa dola huru ya Wapalestina.

https://p.dw.com/p/11Ad7
Kansela Angela Merkel (kushoto) na mgeni wake, Rais Mahmoud Abbas
Kansela Angela Merkel (kushoto) na mgeni wake, Rais Mahmoud AbbasPicha: dapd

Ziara ya Rais Abbas mjini Berlin haikupangwa juzi wala jana. Hata hivyo, maridhiano ya kisiasa kati ya chama chake na Hamas yaliyotiwa saini mjini Cairo wiki hii, yameishangaza na kuiweka serikali ya Ujerumani katika wakati mgumu, ikijiuliza ni namna gani inapaswa kuliendelea suala hili.

Pamoja na kusisitiza mara kadhaa kuwa amani baina ya Israel na Palestina ni miongoni mwa vipaumbele vyake, lakini sasa Kansela Merkel hataki kusema sana juu ya uungaji mkono wa nchi yake kwa azma ya Palestina kuanzisha taifa lao kupitia ridhaa ya Umoja wa Mataifa.

"Ndio tunataka suluhisho la kuwa na mataifa mawili huru, na suluhisho lazima lifanyiwe kazi. Lakini hatufikirii kuwa hatua ya hivi karibuni inasaidia kufikia suluhisho hili." Alisema Kansela Merkel kwenye mkutano na waandishi wa habari mara tu baada ya mazungumzo yake na Rais Abbas hapo jana jioni mjini Berlin.

Hatua hiyo ya karibuni anayoikusudia Kansela Merkel hapa ni makubaliano baina ya Fattah na Hamas, ambayo anasema kwamba lazima yaakisi mambo matatu: kwanza hakikisho la usalama na uwepo wa taifa la Israel, pili tangazo la kuacha matumizi ya vurugu na tatu kuyatambua makubaliano ya awali na Israel.

Ufaransa na Ujerumani siasa tafauti Mashariki ya Kati

Rais Mahmoud Abbas (kushoto) na kiongozi wa Hamas, Khalid Meshaal mjini Cairo
Rais Mahmoud Abbas (kushoto) na kiongozi wa Hamas, Khalid Meshaal mjini CairoPicha: Picture-Alliance/dpa

Baadaye leo, Rais Abbas atakutana na Rais Nikolas Sarkouzy wa Ufaransa huko mjini Paris, ambapo tafauti za mitazamo baina ya Ujerumani na Ufaransa kuelekea siasa za Mashariki ya Kati ziko wazi.

Waziri Mkuu wa Israel alikuwa huko wiki hii kutafuta uungwaji mkono kwa upinzani wa maridhiano ya kisaa baina ya Fattah na Hamas. Rais Sarkouzy alisema katika mahojiano ya wiki hii kwamba pindi suala la dola huru ya Palestina litakapoletwa kwenye Umoja wa Mataifa, nchi yake itawajibika ipasavyo kusaidia.

Katika ziara yake ya mwezi uliopita nchini Israel, Kansela Merkel alimuahidi Waziri Mkuu Netanyahu kwamba Ujerumani haitaunga mkono uanzishwaji wa taifa huru la Palestina, kauli ambayo ilikosolewa vikali na vyama vya upinzani hapa nchini.

Hata hivyo, sasa Kansela Merkel anasema kwamba tafauti hii baina yake na Rais Sarkouzy si kitu kikubwa sana.

"Kile alichokisisitiza jana Rais wa Ufaransa ndicho ambacho mimi pia nakimaanisha: Sote tunataka hatua za haraka zichukuliwe ili kufikia suluhisho. Na matarajio haya ni yetu sote, iwe Ufaransa, iwe Ujerumani, na sote tungelitaka kuona kuwa maneno ya Rais Abbas yanatimizwa, na hilo ndilo jambo ambalo kwa sasa tunapaswa kulizingatia." Alisema Kansela Merkel kwenye mkutano huo.

Rais Abbas ataka ulimwengu uamue

Wapalestina wa Gaza wakishangilia muafaka wa kisiasa kati ya Hamas na Fattah
Wapalestina wa Gaza wakishangilia muafaka wa kisiasa kati ya Hamas na FattahPicha: ap

Kwa upande wake, Rais Abbas ametumia mkutano wake na Kansela Merkel kupiga njiwa wawili kwa jiwe moja. Kwanza kuyafafanua makubaliano yake na Hamas na pili kutafuta uungwaji mkono wa Ujerumani hapo mwezi Septemba, wakati Mamlaka ya Ndani ya Palestina itakapowasilisha pendekezo la kuundwa kwa taifa lake huru.

Rais Abbas amesisitiza kwamba, maridhiano ya kisiasa kati ya Fattah na Hamas ni muhimu sana kwa amani ya ndani ya Palestina na pia baina ya Palestina na Israel.

Huku akirejelea kauli yake kwamba yeye ndiye Rais wa Palestina na mwenye dhamana ya kutafuta amani, Rais Abbas amesema kwamba, hata ndani ya Israel yamo makundi ya upinzani ambayo hayataki amani na Wapalestina, lakini hilo halizuii uungwaji mkono wa kimataifa kwa Israel.

Akizungumzia kile hasa ambacho serikali yake inakusudia kukifanya hapo Septemba mwaka huu kwenye Umoja wa Mataifa, Rais Abbas amesema kwamba ulimwengu ndio sasa wa kuamua kuwa ni kwa muda gani zaidi Wapalestina waendelee kuishi chini ya ukaliwaji wa kijeshi wa Israel.

"Hatwendi Umoja wa Mataifa kuomba kuwa na dola huru ya Kipalestina, bali tunataka kuuliza ulimwengu maoni yake. Je, ulimwengu huu unafikiria kuwa jamii ya watu inaweza kuishi bila ya kuwa na dola yake? Kwa miaka 67 Palestina imeishi chini ya ukaliwaji. Sisi ni watu pekee duniani tunaoishi chini ya ukaliwaji wa kijeshi." Alisema Rais Abbas kwenye mkutano huo.

Hadi sasa tayari zaidi ya mataifa 110 duniani yameshautambua uwakilishi wa kidiplomasia wa Palestina, yakiwemo mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, kama vile Poland, Romania na Hungary. Sasa Mamlaka ya Ndani ya Palestina inatafuta uungwaji mkono zaidi kwenye Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Bernd Gräßler/DW Berlin
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo