Merkel akosoa mpango wa Israeli
6 Desemba 2012Akizungumza leo katika mkutano na waandishi wa habari na Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu mjini Berlin, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kwa kawaida Ujerumani imekuwa ni miongoni mwa mshirika mkubwa wa Israeli, lakini mpango wa kujenga makaazi 3,000 ya walowezi katika eneo muhimu la Ukingo wa Magharibi, umesababisha upinzani wa kimataifa na kuifanya Ujerumani kuukosoa wazi mpango huo. Kansela Merkel amebainisha kwamba mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa kuwepo mataifa mawili lazima yaendelee na kwamba hatua zinazochukuliwa na upande mmoja hazina budi kuepukwa. Amerudia kuelezea dhamira yake kuhusu usalama wa Israeli.
Netanyahu asikitishwa na hatua ya Ujerumani
Kwa upande wake Netanyahu ameelezea kusikitishwa na hatua ya Ujerumani kutopiga kura katika Hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa, ingawa amesema kwamba ana uhakika Ujerumani inaunga mkono ustawi wa Israeli. Amefafanua kuwa bado ana amini anaungwa mkono na Ulaya, hata baada ya baadhi ya nchi za Umoja huo kuwahoji mabalozi wa Israeli walioko katika nchi hizo ikiwa ni katika kupinga mpango huo wa ujenzi wa makaazi mapya ya walowezi kwenye Ukingo wa Magharibi. Amesema hadhani kama wameipoteza Ulaya, ingawa kuna mtazamo tofauti barani humo kuhusu suala la ujenzi wa makaazi mapya. Netanyahu amesema Ulaya imeuelewa vibaya mgogoro wa Mashariki ya Kati na kudhani kuwa ni kuhusu suala la makaazi peke yake, akisisitiza kuwa hilo siyo chimbuko la matatizo na kwamba matatizo yalianza baada ya mwaka 1967.
Israeli yafikia uamuzi huo baada ya kura ya UN wiki iliyopita
Hatua ya Israeli kutangaza kujenga makaazi mapya ya walowezi imefikiwa baada ya wiki iliyopita hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa kupiga kura ya kuipandisha hadhi Palestina kuwa mtazamaji asiyekuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Aidha, Wapalestina wanasema kuwa mpango huo wa Israeli katika ardhi ambayo wanaipigania kuwa taifa lao, unaweza ukaugawa Ukingo wa Magharibi na kujitenga kutoka Jerusalem, ambao utakuwa mji wao mkuu wa baadae. Mbali na mkutano wa Merkel na Netanyahu, ilifanyika pia mikutano iliyohusisha mawaziri saba wa Israeli na mawaziri kumi wa Ujerumani ambapo pamoja na mambo mengine wamezungumzia miradi ya pamoja katika sekta ya sayansi na elimu.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,DPA
Mhariri:Yusuf Saumu