Merkel akabiliwa na kisiki cha Ugiriki Bungeni | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.02.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Merkel akabiliwa na kisiki cha Ugiriki Bungeni

Bunge la Ujerumani (Bundestag), leo litapiga kura kuidhinisha kiasi cha Euro bilioni 130 kama dhamana mpya kwa Ugiriki, huku Kansela Angela Merkel akikabiliana na upinzani kutoka ndani ya serikali yake.

Kansela Angela Merkel

Kansela Angela Merkel

Kiasi ya dazeni moja ya wabunge katika muungano huu wametoa msimamo wao wa kupiga kura ya hapana na endapo idadi hii itafikia wabunge 20, Kansela Markel, atalaazimika kuangalia upande wa upinzi ili kuweza kupata idadi ya kura inayotakiwa kuidhinisha dhamana hii.

Ikiwa hivyo, wadadisi wanasema litakuwa pigo la aibu kwa Kansela Merkel, na itazidisha shaka iliyoanza kutawala juu ya uwezekano wa kuvunjika mapema kwa muungano huu. Lakini washirika wa Merkel wanasema wana uhakika wa kupata kura za kutosha kutokana na kuungwa mkono na vyama vya upinzani vya Social Democrats na Kijani.

Kansela Merkel anahitaji kura 311 ili kupata wingi unaotakiwa katika Bunge la watu 620, ambako muungano wake una viti 330. Hata hivyo, katika kura iliyopigwa September 27, manaibu 15 katika muungano huu walipiga kura ya hapana na hivyo kuuacha muungano huu na wingi wa viti 315 tu.

Dalili zinaonyesha kuwa Wajerumani wameanza kukosa uvumilivu na mzozo wa madeni ya Ugiriki. Mmoja wa watendaji wakuu katika serikali ya Angela Merkel, Waziri wa mambo ya ndani, Hans-Peter Friedrich alitamka wazi kuwa ugiriki inapaswa kuondolewa katika kanda wa Euro, na kuongeza kuwa nafasi ya nchi hii kufufuka itakuwa kubwa zaidi ikiwa nje ya ukanda huu.

Kura ya maoni iliyoendeshwa na gazeti la Bild am Sonntag siku ya Jumapili, ilibainisha kuwa, asilimia 62 ya wajerumani wanapinga kutolewa kwa kiasi hicho cha Euro bilioni 130 kuinusuru Ugiriki, wakati asilimia 33 wanaunga mkono. Katika kura kama hiyo mwezi Septemba, asilimia 53 walikataa wakati asilimia 43 waliunga mkono.

Bwana Klaus-Peter Willsch

Bwana Klaus-Peter Willsch

Mmoja wa wabunge wa chama cha Kansela Merkel, cha Chritian Democats (CDU), anayepinga kutolewa kwa fedha hizi, Klaus-Peter Willsch, alibainisha kuwa hali ndani ya Ujerumani inaonyesha kuwa watu wamechoka kuisadia Ugiriki.

Willsch, ambaye alitengwa na chama chake kutokana na msimamo wake mkali juu ya suala hili, alisema hafahamu ni manaibu wangapi watapiga kura ya kuidhinisha dhamana hii lakini akasema anatumaini watakaopinga watakuwa zaidi ya wale 15 waliopinga mwezi septemba.

Wajerumani ambao ndiyo wanaochangia kwa kiasi kikubwa jitihada za kunusuru uchumi wa Ugiriki, wanazidi kukosa uvumilivu na kile Waziri wa fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble alichokiita 'kisima kisicho na kina' ndani ya Ugiriki.

Na wakati huohuo, habari zinazidi kuenea katika taifa hili lenye uchumi mkubwa zaidi barani ulaya kuwa, mafanikio yake yanazidi kuwa katika hatari kwa kadri mgogoro wa madeni unapozidi kuuma na hivyo kuathiri uwezo wa watu ndani ya kanda kufanya manunuzi ya bidhaa za Ujerumani.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble

Ukosoaji wa Ugiriki kutoka kwa Wajerumani umetonesha majeraha ya enzi za vita vikuu ya pili vya Dunia. Wandamanaji mjini Athens walichoma bendera ya Ujerumani mwanzoni mwa mwezi huu wakati magazeti ya nchi hiyo yalikuwa yakiwaonyesha Kansela Angela Merkel na Waziri wa Fedha Wolfgang Schaeuble wakiwa wamevaa sare za Kinazi.

Pamoja na umaarufu wake kuonekana bado uko juu katika kura za maoni, Kansela Merkel amekumbana na changamoto kadhaa hivi karibuni, takribani miezi 18 tu kabla ya uchaguzi mwingine, jambo ambalo linaanza kutia mashaka juu ya uwezekano wa mwanamama huyo kubakia madarakani.

Tarehe 17 Febuari, Christian Wulff, alijiuzulu kama Rais wa Ujerumani kufuatia kashfa ya upendeleo wa kisiasa na hivyo kutoa pigo kubwa kwa Kansela Merkel, ambaye alimteua mwenyewe kwa nafasi hii isiyo na madaraka ya uamuzi kisiasa.

Siku chache baadae, Kansela Merkel alilaazimika kukubali chaguo la Joachim Gauck, aliependekezwa na washirika wake katika muungano, Chama kidogo cha Kiliberali (FDP), kushika nafasi ya Rais. Merkel alimkataa Gauck awali na kumpendekeza Wulff kushika nafasi hiyo.

Japo Merkel hakubaliani na maoni ya kuiondoa Ugiriki katika kanda ya Euro, washirika wake katika serikali, chama cha Christian Social Union (CSU), wanakabiliwa na uchaguzi mgumu wa Jimbo mwaka 2013 na wamekuwa wakipaza sauti kutaka Ugiriki iondoke.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga

Mhariri: Mohamed Abdul Rahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com