1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ahimiza ushirikiano Moscow

10 Mei 2015

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Jumapili (10.05.2015) ametowa heshima zake kwa wanajeshi wa Urusi waliouwawa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kutowa wito wa ushirikiano na Urusi kutokana na mzozo wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/1FNgc
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Vladimir Putin wa Urusi wakiweka shada la mauwa katika kaburi la mwanajeshi asiejulikana karibu na Ikulu-Kremlin mjini Moscow.(10.05.2015)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Vladimir Putin wa Urusi wakiweka shada la mauwa katika kaburi la mwanajeshi asiejulikana karibu na Ikulu-Kremlin mjini Moscow.(10.05.2015)Picha: Reuters/Host Photo Agency/RIA Novosti

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Jumapili (10.05.2015) ametowa heshima zake kwa wanajeshi wa Urusi waliouwawa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kutowa wito wa ushirikiano na Urusi wakati kukiwa na mvutano wa mzozo wa Ukraine.

Merkel amewasili Moscow kuweka shada la mauwa katika kaburi la mwanajeshi asiejulikana karibu na kuta za Ikulu ya Kremlin ikiwa kama ishara ya kuleta maridhiano baada ya kukwepa kuhudhuria maadhimisho makuu ya Siku ya Ushindi hapo Jumamosi.

Akikutana na mwenyeji wake Rais Vladimir Putin kwa mazungumzo katika Ikulu Kansela Merkel amesisitiza umuhimu wa ushirikiano.

Merkel amesema mwanzoni mwa mazungumzo hayo baada ya tukio la kuweka shada la mawaua kwenye kaburi la askari huyo aliyeuwawa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kwamba "ni muhimu kwetu kufanya kazi,kushirikiana ikiwa ni pamoja na wakati wa hali ngumu .....kama hali ya hivi sasa na kujaribu kupata ufumbuzi wa kidiplomasia."

Viongozi hao wawili wameujadili mzozo wa Ukraine katika mazungumzo yao ambapo Merkel amesema bado hakuna usitishaji wa mapigano wa dhati na kwamba waasi wamekuwa wakikiuka mara kwa mara makubaliano ya kusitisha mapigano.

Amesema mchakato huo ni mgumu na walitaraji usitishaji huo wa mapigano ungeliheshimiwa lakini kwa bahati mbaya hilo halikutokea.

Kwa upande wake Putin amesema wanatafautiana na Merkel kuhusiana na mzozo huo wa Ukraine lakini kwa maoni yake anauona mchakato wa amani wa Minsk unapiga hatua.

Kususiwa kwa gwaride la kijeshi

Urusi hapo Jumamoi iliandaa gwaride kubwa kabisa la kijeshi kuadhimisha miaka sabini ya ishindi dhidi ya utawala wa Wanazi wa Ujerumani lakini takriban nchi zote za magharibi zilisusia sherehe hizo kutokana na hatua ya Urusi kulinyakuwa jimbo la Ukraine la Crimea na kuwaunga mkono waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine.

Gwaride la kijeshi Siku ya Ushindi Moscow. (09.05.2015)
Gwaride la kijeshi Siku ya Ushindi Moscow. (09.05.2015)Picha: Reuters/Host Photo Agency/RIA Novosti

Hapo mwezi wa Februari Putin alikuwa mwenyeji wa Merkel na Rais Francois Hollande wa Ufaransa kwa mazungumzo muhimu kuhusu Ukraine ambapo ilikuwa ni ziara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa Ujerumani nchini Urusi tokea kuibuka kwa mzozo huo wa Ukraine.

Katika miezi ya hivi karibuni Merkel alitimiza dhima muhimu katika mazungumzo ya mzozo wa Ukraine akiwasaliana kati ya pande mbili serikali ya Urusi na mataifa ya magharibi.

Ukraine na mataifa ya magharibi yaishutumu Urusi kwa kupanga njama za mzozo huo wa kinyama wa waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine ambao umeuwa zaidi ya watu 6,100 katika kipindi cha mwaka mmoja na kitu.

Karata za Putin hazikubaliwi na Merkel

Mchambuzi wa kisiasa Lilia Shevtsova amesema mkutano huu wa Jumapili kati ya Putin na Merkel kwa kiasi kikubwa ni wa ishara.Mchambuzi huyo mashuhuri anayeegemea upande wa mataifa ya magharibi ameandika kwenye mtandao wake wa Facebook kwamba haimaanishi kwamba wanafuraha kukutana.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Vladimir Putin wa Urusi wakiwa Ikulu Moscow. (10.05.2015)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Vladimir Putin wa Urusi wakiwa Ikulu Moscow. (10.05.2015)Picha: Getty Images/AFP/M. Shipenkov

Amesema Putin anajaribu kushikilia karata zake katika meza ya mazungumzo kwa kutumia vivuli vya kale na heshima za watu wengine lakini Merkel haukubali mchezo wake huo na kwamba amefika hapo kutowa heshima zake kwa watu walioshinda vita vikuu.

Kuna wasi wasi mkubwa kwamba Putin anazitumia sherehe za Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kuhalalisha hatua ya Urusi kuingilia kati masuala ya Ukraine na kuipigia debe agenda yake ya uzalendo.

Putin apuuza bebeduo

Putin alipuuza bebeduo la mataifa ya magharibi na badala yake alionyesha umuhimu wa kukuza uhusiano na Asia, Amerika Kusini na Afrika.

Rais Vladimir Putin wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya Siku ya Ushindi Moscow. (09.05.2015)
Rais Vladimir Putin wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya Siku ya Ushindi Moscow. (09.05.2015)Picha: Reuters/G. Dukor

Katika matamshi kupitia televisheni Jumamosi jioni amekaririwa akisema "kila tuliyemtaka kumuona yuko hapa".

Kabla ya kukutana na Merkel, Putin alikutana na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye amempongeza kwa kusimama kidete dhidi ya serikali ya Marekani na kutaja kwamba nchi zao mbili zimeadhibiwa kwa kuwekewa vikwazo.

Mugabe amesema hiyo ndio sababu kwa nini inabidi waendelee kuwa pamoja.

Kurekebisha uhusiano

Lakini Putin pia ameashiria kuwa tayari kurekebisha uhusiano na Ulaya wakati alipokutana na Rais Milos Zeman wa Jamhuri ya Czech mmojawapo wa viongozi wachache wa Ulaya aliekwenda Moscow kwa ajili ya sherehe za ushindi.

Ndege za kivita zikivinjari angani sherehe za Siku ya Ushindi Moscow. (09.05.2015)
Ndege za kivita zikivinjari angani sherehe za Siku ya Ushindi Moscow. (09.05.2015)Picha: Reuters/T. Makeyeva

Katika mazungumzo yake na kiongozi huyo wa sera za mrengo wa kushoto Putin amesema hapo Jumamosi sio wao waliosababisha kudhoofika kwa uhusiano na Ulaya lakini anataraji kutokana na wanasiasa kama kongozi huyo wa Czech wataweza sio tu kuufuwa uhusiano huo kikamilifu bali pia kusonga mbele.

Umma wa watu 500,000 waliandamana mjini Moscow Jumamosi wakiwa na picha za jamaa zao waliopigana katika vita vikuu katika maandamano makubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 15 cha utawala wa Putin.

Putin mwenye umri wa miaka 62 alishiriki kwenye maandamano hayo bila ya kutarajiwa akiwa na picha ya baba yake mkononi aliepigana katika vita hivyo vikuu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri :Hamidou Oummilkheir