1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel afadhaishwa na kashfa ya Hoeness

22 Aprili 2013

Kansela Angela Merkel amefadhaishwa na kashfa ya kukwepa kodi inayomkabili rais wa timu ya mpira wa miguu ya Bayern Munich, Uli Hoeness, huku Hoennes akisema hatajiuzulu kupisha uchunguzi unaoendelea dhidi yake.

https://p.dw.com/p/18Knh
Bundeskanzlerin Angela Merkel (r, CDU) und der Präsident des FC Bayern München, Uli Hoeneß präsentieren am Donnerstag (13.09.2012) im Bundeskanzleramt in Berlin Trikots und Ball mit der Aufschrift "Geh deinen Weg". Alle Bundesliga-Vereine werden am 3. Spieltag auf ihre übliche Trikotwerbung verzichten und die Spieler mit speziellen Shirts aufs Feld schicken: Mit der Aufschrift «Geh deinen Weg» wollen die Vereine das gleichnamige Projekt der Deutschlandstiftung Integration unterstützen. Foto: Kay Nietfeld dpa +++(c) dpa - Bildfunk+++ pixel
Angela Merkel und Uli HöneßPicha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert, amesema kwamba watu wengi nchini Ujerumani wamefadhaishwa na Hoennes, na hivyo ndivyo alivyo pia Kansela Merkel.

Kwa mujibu wa Seibert, Kansela Merkel amefadhaishwa zaidi kutokana na ukweli kwamba Hoeness amekuwa kielelezo chema kwa Ujerumani, kwani sio tu kwamba anaongoza klabu bora kabisa ya mpira, bali pia amekuwa akiunga mkono jithada kadhaa za maendeleo, ukiwemo mradi wa kuwajumuisha wageni kwenye jamii ya Ujerumani.

Mwishoni mwa wiki, Hoeness alinukuliwa na gazeti la kila wiki la Focus akisema kwamba aliripoti mwenyewe kwa mamlaka juu ya akaunti yake ya fedha kwenye benki moja nchini Uswisi hapo mwezi Januari.

Waendesha mashitaka wamekiri kwamba wameanzisha uchunguzi huo kufuatia ripoti iliyopelekwa kwao na Hoeness mwenyewe kupitia mshauri wake wa masuala ya fedha .

Hoeness hatajiuzulu

Hata hivyo, Hoeness, mwenye umri wa miaka 61, amesema hana mpango wowote wa kujiuzulu kutokana na tuhuma hizo za kukwepa kodi. Badala yake, rais huyo wa Bayern Munich, ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya timu hiyo, ameliambia gazeti la Sport Bild Plus, atahudhuria kweye mechi ya nusu fainali ya Champions League kati ya timu yake na Barcelona hapo kesho.

Rais wa Bayern Munich, Uli Hoeness (kushoto) na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (wa pili kushoto).
Rais wa Bayern Munich, Uli Hoeness (kushoto) na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (wa pili kushoto).Picha: picture-alliance/dpa

Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Munich, Ken Heidenreich, amethibitisha kuendelea kwa uchunguzi dhidi ya Höness, ingawa hakutaja kiwango cha fedha kinachohusika wala muda ambao uchunguzi huo utachukua.

Mwenyewe Hoeness, ambaye pia ni mmiliki mwenza wa kiwanda cha kusindikia nyama, amekataa kuingia undani wa suala hili, lakini ameahidi kutoa ushirikiano wowote unaohitajika kwa waendesha mashitaka.

Ripoti hizo za kukwepa kodi ndizo zilizohanikiza kwenye vyombo vya habari nchini Ujerumani na Hoeness amenukuliwa na gazeti la Münchener Merkur, kwamba atajitetea kisheria dhidi ya vyombo vya habari viinavyomtuhumu.

Höness, ambaye mwenyewe ni mchezaji wa zamani wa Ujerumani ya Magharibi, amekuwa msemaji mkubwa kwenye soka ya Ujerumani, Bundesliga. Alikuwa meneja wa kwanza kijana kabisa kwenye Bundesliga, baada ya kuchukua nafasi hiyo akiwa na miaka 27 tu, kufuatia jeraha lililohitimisha uchezaji wake uwanjani.

Baada ya zaidi ya miaka 30 akiwa kama meneja wa kibiashara wa Bayern Munich, mwaka 2009 alimrithi Franz Beckenbauer kama rais wa timu hiyo. Chini ya uongozi wake, klabu hiyo imekuwa na mafanikio zaidi kuliko klabu zote za mpira nchini Ujerumnai na moja ya klabu tajiri kabisa duniani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman