1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchuano ya awali ya uchaguzi wa Marekani

5 Novemba 2008

Wademocrats wawania kuyadhibiti mabaraza yote mawili ya bunge

https://p.dw.com/p/Fnde
Wagombea Urais ohn McCain na Barack ÓbamaPicha: picture-alliance/dpa

Matokeo ya uchaguzi wa Rais yameanza kutangazawa yakizusaha kiwewe miongoni mwa wafuasi wa wagombea wawili Barack Obama wa Democrats na John McCain wa chama cha Republican.

Matokeo ya kwanza yalimpa ushindi Obama wa jimbo la Vermont huku McCain akinyakua la Kentucky.

Mbali na Obama kushinda jimbo la Vermont, Wademocrats pia walinyakua mapema ushindi wa kiti cha Seneti katika jimbo la Virginia, kiti ambacho awali kilikua mikononi mwa Warepublican.

Uchaguzi huu unatajwa kuwa ni wa kihistoria, ikijitokeza idadi kubwa kabisa ya wapiga kura kuwahi kuonekana kuripotiwa hali nzuri ya hewa takriban kote nchini Marekani. Moja ya majimbo ambako kulionekana milolongo mirefu mno ya wapiga kura ni California.

Tayari kumetokewa malalamiko upande wa Warepublican , huku mgombea wao John McCain akisema kwamba atafungua mashitaka kulalamikia kuchelewa karatasi za kupigia kura kwa watumishi wa jeshi wasiokuwepo ili waweze kupiga kura mapema. Malalamiko yaliotumwa katika mahakama ya wilaya mashariki mwa Virginia yanadai kura hizo zote zihesabiwe kama zilizoharibika.

Mbali na uchaguzi huo wa Rais, Wademocrats wanamatumaini ya kuongeza wingi wao katika mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani Congress-yaani Baraza la waakilishi na lile la Seneti. Matumaini hayo hasa yanatokana na umaarufu wa Barack Obama na kushuka vibaya kwa heba ya Rais George W.Bush ambaye ni Mrepublican na anayemaliza muda wake.

Inakadiriwa wafanyakazi milioni 1.3 katika sekta hiyo ya jeshi la Marekani wanahaki ya kupiga kura kwa kutumia hoja ya kutokuwepo maeneo yako, ikiwa wako sehemu yoyote ya Marekani kikazi.

Kuna zaidi ya 180.000 nchini Irak na Afghanistan.Haikuweza kufahamika ni wangapi wanahaki ya kupiga kura katika jimbo la Virginia. Mbali na malalmiko hayo uchaguzi uliendelea kwa raia wa kawaida kama ilivyopangwa , kukitokeza ishara za mchuano mkali na wapiga kura kugawika.

Wakati matokeo yakizidi kumiminika, Obama alishinda pia jimbo la New Hempshire ambalo katika kura za kusaka mgombea wa Wademocrats alipoteza jimbo hilo kwa mpinzani wake Hillary Clinton wakati McCain alishinda kwa upande wa chama chake cha Republican. Kwa uchaguzi huu wa Rais tayari uchunguzi wa maoni ya wapiga kura ulionyesha Obama akiongoza kwa pointi 10 mbele ya McCain.

Chini ya utaratibu wa uchaguzi wa Marekani ni kura za jopo la uchaguzi katika kila jimbo zinazoamua, kutokana na uakilishi wa jimbo husika. Kuweza kushinda Urais mgombea anahitaji kunyakua kura 270. Hadi sasa Obama ana kura 174 na McCain 49.

Kwa upande mwengine inaelekea Wademocrats wamo njiani kujinyakulia ushindi utakaowawezesha kulidhibiti bunge yaani Baraza la Congress. Wakishinda pia katika jimbo la New Hempshire.

Mbali na hayo lakini ,Yeyote atakayeshinda na kuwa rais wa 44 wa taifa hilo kubwa ataweka historia. Obama atakua Mmarekani wa kwanza mweusi kuwa rais wa nchi hiyo na ikiwa ni McCain atakua rais mwenye umri mkubwa kabisa kuchaguliwa katika kipindi cha kwanza.Obama ana umri wa miaka 47 na McCain miaka 72.