1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Njia nyeupe kwa Obama

Liongo, Aboubakary Jumaa2 Juni 2008

Nchini Marekani mbio za kuwania uteuti wa chama cha Democrat nafasi ya kugombea urais wa Marekani, kati ya Bi Hillary Clinton na Barak Obama zinakaribia mwisho, huku Obama akiwa na nafasi kubwa.

https://p.dw.com/p/EBPj
Seneta Obama akihutubia mkutano wa kampeni zake huko Mitchell, janaPicha: AP

Pamoja na ushindi wa Seneta Clinton katika jimbo la Puerto Rico hapo jana, lakini kwa Obama amebakisha kura 47 tu kufikisha kura elfu mbili 118 kushinda nafasi hiyo.


Wasaidizi wa Obama wanaamini ya kwamba wiki hii itahitimisha safari ndefu ya mgombea wao kwa kupata ushindi na kuwa mgombea urais wa kwanza mwenye asili ya uafrika katika historia ya Marekani.


Majimbo ya Montana na Dakota ya Kusini yatapiga kura zake kesho ambapo Obama anahitaji kura 45 kutangazwa mshindi.


Lakini hata hivyo kwa upande wake, seneta Hillary Clinton amesema atapambana mpaka dakika ya mwisho na kutupilia mbali hisia na wito wa kumtaka kung´atuka katika mbio hizo.


Mgombea huyo ambaye ni mke wa rais wa zamani Bill Clinton anafanya hivyo kwa kile wachambuzi wa siasa za Democrat wanachokiona kuwa ni kumuwekea mbinyo Obama pale atakaposhinda amteue kuwa mgombea mwenza wa nafasi ya umakamu wa rais.


Akihutubia mkutano wa kampeni huko Dakota ya Kusini, Seneta Obama alimsifu mpinzani wake huyo akisema ni mchapakazi mzuri na hodari ambaye anaweza kuwa faida kubwa kwa chama hicho cha Democrat.


Msemaji wa Seneta Obama Robert Gibbs alitabiri kuwa wiki hii Obama atatangazwa mshindi na kutimiza kile nchi inachohitaji ambacho amesema ni mabadiliko.


Kauli mbiu ya kampeni za Obama ni tunaamini katika mabadiliko, ndiyo tunaweza.


Wakati huo huo mwenyekiti wa kamati ya taifa ya Democrat,Howard Dean amesema kuwa muda wa kuponya majeraha ya kampeni hizo umeanza baada ya ahadi za mwishoni mwa wiki kutoka kwa wagombea hao kudhamiria kuyabakisha majimbo ya Michigan na Florida katika himaya ya Democrat.


Hapo siku ya Jumamosi picha za televisheni zilionesha wafuasi wa Seneta Clinton wakitishia kumchagua mgombea wa Republican McCain.


Naye seneta wa jimbo la Florida Bill Nelson ambaye anamuunga mkono Bi Clinton alisema kuwa wakati wa sasa ni wa kutoa ujumbe wa umoja na kufufua mazungumzo ya njozi za kuwa na wagombea hao wawili katika kuwania urais wa Marekani dhidi ya mgombea wa Republican.


Wakati huo huo, Seneta Edward Kennedy leo hii anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kansa ya ubongo, na kuahidi kuwa atarejea tena katika kampeni za urais wa Marekani.


Seneta Kennedy ambaye anamuunga mkono Seneta Obama amesema kuwa anatarajiwa kufanyiwa upasuaji huo katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Duke.


Edwardy Kennedy ambaye ndiye pekee aliyehai katika familia ya aliyekuwa rais wa Marekani John F Kennedy amesema kuwa anategemea kuwa katika hali nzuri na kurejea katika kampeni kuhakikisha Barak Obama anakuwa rais ajaye wa Marekani.