1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbinyo zaidi kwa utawala wa Ukraine kuhusu Timoschenko

27 Aprili 2012

Rais wa Ukraine, Viktor Yanukovych, amesema atachunguza kutendewa vibaya kwa waziri mkuu wa zamani aliye kifungoni, Yuliya Timoshenko.

https://p.dw.com/p/14lqs
Yuliya Timoshenko
Yuliya TimoshenkoPicha: picture-alliance/dpa

Mgomo wa kususia kula unaoendeshwa na waziri mkuu wa zamani wa Ukraine aliye kifungoni, Yulia Timoshenko, huenda ukawa ni hatari kwa maisha yake, japokuwa mgomo huo uko katika hatua zake za mwanzo, hii ukitilia maanani hali yake dhaifu ya kimwili na kisekolojia. Jambo hilo limeelezwa na daktari wa kijerumani ambaye alimfanyia uchunguzi hapo jana. Wakati huohuo, rais wa Ukraine, Viktor Yanukovych, jana alisema: serikali yake itayachunguza madai yaliotaja kwamba Bibi Timoshenko alitendewa vibaya gerezani. Haya yanatokea wakati mbinyo hapa Ulaya unazidi kuwekewa watawala wa Ukraine kutokana na mkasa wa mwanasiasa huyo.

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck
Rais wa Ujerumani Joachim GauckPicha: dapd

Rais Viktor Yanukovych wa Ukraine alitoa ahadi hiyo jana baada ya madai kwamba Bibi Timoschenko alipigwa na kupata majaraha gerezani kuzidi kuwafikia watu mbalimbali wenye uzito wa kisiasa hapa Ulaya. Alitoa ahadi hiyo baada ya Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck, kuamua kutohudhuria mkutano wa marais wa nchi za Ulaya ya Kati mwezi ujao huko Ukraine; hiyo ni aina ya kulalamika juu ya kuwekwa gerezani Bibi Timoshenko. Kwa mujibu wa gazeti la Financial Times la hapa Ujerumani ni kwamba wasaidizi wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wamewaambia wawakilishi wa serikali ya Ukraine kwamba Kansela ametishia kutokwenda katika mkutano huo kutokana na kisa hicho cha Bibi Timoshenko

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Hans-Peter Friedrich
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Hans-Peter FriedrichPicha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa Rais Gauck wa Ujerumani alisema rais huyo hajaamua kwenda kuangalia mechi zitakazochezwa na timu ya kandanda ya taifa ya Ujerumani wakati wa kuwania ubingwa wa nchi za Ulaya mwaka huu, ambapo Ukraine pamoja na Poland ndio watakuwa wenyeji wa tamasha hilo. Timu ya Ujerumani itacheza mechi tatu katika duru ya kwanza huko Ukraine.

Huku mbinyo zaidi ukiwekewa Ukraine, kamishina wa Umoja wa Ulaya juu ya sheria, amesema amevunja mpango wake wa kutaka kuhudhuria mchezo wa kwanza wa Euro 2012 hapo Juni tisa, na uamuzi huo unatokana na namna Bibi Timoschenko anavotendewa. Naye waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Hans-Peter Friedrich, alisema jana pembezoni mwa mkutano na wenzake wa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya kwamba yeye atakuwa na shida kuhudhuria michezo ya kandanda ya ubingwa wa Ulaya, huku akijuwa kwamba kilomita chache kutoka mahala kunapofanywa mashindano hayo, kuna mtu ambaye hatendewi kwa mujibu na kanuni ambazo nchi za kistaarabu duniani zimekubaliana miongoni mwao. Pia aliliambia gazeti la Ujerumani kwamba angalau atataka aonane na Bibi Timoshenko.

Rais Yanukovych wa Ukraine amesema binafsi amemuamuru wakili mkuu wa serikali, Viktor Pshonka, aliangalie dai la Bibi Timoshenko kwamba alipigwa, na kwamba anatarajia kupata jibu madhubuti hivi karibuni.

Hapo juzi, washirika wa Bibi Timoshenko walitoa taarifa ya Bibi Nina Karpachyova, ambaye ni mwakilishi wa bunge kuhusu haki za binadamu, ikisema kwamba Bibi Timoshenko alipata mapigo katika mikono yake na tumboni pale alipolazimishwa kupelekwa hospitali. Inaripotiwa alianza kususia kula, akilalalmika namna alivotendewa. Maafisa katika jela ambako Bibi Timoshenko amewekwa wayakanusha madai hayo. Ripoti ya madaktari wa kijerumani waliomuangalia bibi huyo inasema Bibi Timoshenko, ambaye anaaminiwa ana matatizo katika tindi ya mgongo, anahofia madaktari wa gerezani watamdhuru kwa makusudi.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Bibi Timoshenko alipewa kifungo cha miaka minane gerezani kwa makosa ya kutumia vibaya wadhifa wake. Kesi ya pili inayohusu mashtaka ya yeye kwamba alifanya udanganyifu katika ulipaji wa kodi katika miaka ya tisini ilianza wiki iliopita. Yeye amekanusha mashtaka hayo na amesema anaandamwa na kufanyiwa kisasi cha kisiasa na hasimu wake, Rais Viktor Yanukovych. Rais huyo wa Ukraine amesema yeye anaunga mkono utawala wa sheria.

Mwandishi: Miraji Othman/ Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef