1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungunzo juu ya Nuklia ya Iran

Saumu Ramadhani Yusuf7 Desemba 2010

Mazungumzo yameshindwa lakini nchi za Magharibi hazijavunjika moyo watakutana tena na Iran huko Uturuki

https://p.dw.com/p/QRmH
Rais Mahmoud Ahamdinejad,Picha: AP

Marekani imekiri kwamba mazungumzo ya Iran na nchi sita zenye nguvu duniani huko Geneva Uswisi yamekuwa magumu na ya wazi. Nchi tano wanachama wa kudumu ndani ya Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani zinaamini kwamba ni lazima Iran isimamishe kabisa urutubishaji wa madini ya Uranium kama ilivyopitishwa katika maazimio ya Umoja wa Mataifa,kabla ya kupatikana maelewano ya aina yoyote.

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka kutaja jina Marekani haikuwa na mazungumzo rasmi na Iran kando ya mkutano huo wa siku mbili huko Geneva lakini imefanikiwa kuwasilisha mapendekezo yake muhimu katika mgogoro huo wa Nuklia ya Iran.

Atomgespräch Iran Genf Flash-Galerie
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton, na mpatanishi wa Iran katika suala la Nuklia Saeed JaliliPicha: AP

 Upande mwingine Iran imesema suala la kuitaka isimamishe urutubishaji wa madini yake ya Uranium halikuwa suala la kujadiliwa katika kikao hicho cha siku mbili kilichomalizika hii leo kwasababu nchi hiyo haihitaji ufafanuzi wa kimataifa au idhini ya kimataifa ya kuwa na haki ya kupata nguvu za Nuklia. Mkuu wa Iran anayehusika na masuala ya Kinuklia Saed Jalili katika mkutano na waandishi wa habari amesema kwamba nchi yake haiwezi kukubali kulazimishwa kuingia katika mazungumzo ya kujadili juu ya haki yake ya kimsingi ya kuwa na Nuklia.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Cathrine Ashton ambaye ameziwakilisha nchi sita zenye nguvu katika mkutano huo yaani Uingereza China Ufaransa,Urusi na Marekani pamoja na Ujerumani na mpatanishi huyo wa Iran bwana Jalili wamekubaliana kufanya duru nyingine ya mazungumzo kama hayo kufikia mwishoni mwa mwezi Januari huko Istanbul nchini Uturuki.

Na pia Jalili amesisitiza kwamba hata katika mkutano huo suala la kuitaka Iran ikome  Kurutubisha madini ya Uranium haliwezi kuibuka,na badala yake kitakachozingatiwa ni  kuhusu ushirikiano wa pamoja katika masuala mbali mbali kwa ajili ya kufikia mtazamo sawa na sio kama ilivyotajwa na bibi Ashton katika taarifa yake kwamba kitakachogubika kikao hicho ni wasiwasi kuhusu mradi wa Kinuklia wa Iran.

Kwa mantiki hiyo imeonesha kwamba kuna hali ya kutoelewana iliyojitokeza katika kikao cha leo baina ya pande hizo mbili hasa kutokana na taarifa hizo mbili zilizotolewa zinatofautiana kuhusu mada ya mkutano ujao wa Istanbul juu ya Iran.

Wakati huohuo viongozi wa nchi za eneo la Ghuba wanaomaliza kikao chao cha siku mbili kilichoanza hapo jana huko Abu Dhabi wamezipongeza juhudi zinazochukuliwa na jumuiya ya Kimataifa kuelekea Iran na kusema kwamba nchi zote katika eneo hilo zina haki ya kuwa na nishati ya Kinuklia kwa ajili ya matumizi ya amani na yanayokwenda na viwango vya shirika la kimataifa la nguvu za Atomiki la IAEA.Aidha viongozi hao wametilia mkazo kwamba viwango hivyo vinabidi pia kuheshimiwa na nchi nyingine zote za Mashariki ya kati ikiwemo  Israel.

Mwandishi Saumu Mwasimba/ AFPE

Mhariri AbdulRahman