1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya uokozi wa Ugiriki yaendelea

Admin.WagnerD31 Julai 2015

Mawaziri wa fedha na uchumi wa Ugiriki wamekutana na wawakilishi wa wakopeshaji wa nchi hiyo leo, kwa mazungumzo kuhusu mpango mpya wa mabilioni ya uokozi, kuelekea muda wa marejesho ya mkopo kwa benki kuu ya Ulaya ECB.

https://p.dw.com/p/1G87G
Washington IWF Logo Symbolbild
Picha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Viongozi wa ujumbe wa taasisi nne zinazosimamia majadiliano hayo ambazo ni ECB, Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Shirika la fedha la kimataifa IMF na mfuko wa utulivu wa Ulaya ESM - walikuwa wanakutana na waziri wa fedha Euclid Tsakalotos, na waziri wa uchumi Giorgos Stathakis.

Mkutano huo unafuatia mazungumzo ya siku tatu kati ya timu za kiufundi juu ya masuala kadhaa yakiwemo sera ya kifedha, mafao ya uzeeni, ajira na mageuzi katika masoko ya bidhaa.

Vyombo vya habari vya Ugiriki viliripoti mapema wiki hii kwamba makundi ya kiufundi yanataraji kiwango cha pato jumla la ndani kunywea kwa hadi asilimia 3.3 mwaka huu wa 2015, kutokana kwa sehemu na usumbufu uliyosababishwa na udhibiti wa utoaji fedha nje ya nchi.

Waziri mkuu Alexis Tsipras akizungumza katika mkutano wa chama chake.
Waziri mkuu Alexis Tsipras akizungumza katika mkutano wa chama chake.Picha: Reuters/Y. Kourtoglou

Kwa mujibu wa afisa wa wizara ya fedha ya Ugiriki, wakopeshaji wanahoji kwamba mipango ya serikali kuweka kodi ya mshikamano ya asilimia 8 kwa mapatao yanayozidi euro lakini tano inapaswa kuondolewa kuepusha ukwepaji kodi.

Afisa huyo pia amebainisha kuwa mchakato wa mashauriano kuangalia upya sheria zinazoongoza soko la ajira unaanza pia ili kuwezesha kuwepo na mfumo mpya wa mapatano ya pamoja ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Hatua hizi zote zilikuwa sehemu ya masharti yaliyokubaliwa Julai 13 mjini Brussels kwa Ugiriki kupatiwa kiasi cha euro bilioni 86 katika ufadhili mpya.

Majadiliano kukamilika Agosti 18

Serikali ya Ugiriki imesema inalenga kukamilisha majadiliano na wakopeshaji ifikapo Agosti 18, siku mbili kabla ya muda inayotakiwa kulipa mkopo wa euro bilioni 3.2 kwa ECB. Kile kinachojulikana kama "hatua za awali" zilizodaiwa na wakopeshaji ili kuanzisha majadiliano ya uokozi, kimesababisha mpasuko ndani ya chama tawala cha Syriza, na kumlazimu waziri mkuu Alexis Tsipras kuzungumzia uwezekano wa uchaguzi wa mapema ikiwa wapinzani wa hatua za kubana matumizi wataendelea kupinga hatua hizo.

Chama hicho kilikubaliana kufanya mkutano mkuu wa dharura mwezi Septemba kujaribu kulinda umoja wa Syriza. Karibu wajumbe 17 wa kamati kuu ya Syriza walijiuzulu jana Alhamisi, wakiutuhumu uongozi kugeuka kuwa kundi la kisiasa linalounga mkono hatua za kubana matumizi.

Tsipras katika picha ya pamoja na wanawake wanaofanya usafi katika wizara ya fedha.
Tsipras katika picha ya pamoja na wanawake wanaofanya usafi katika wizara ya fedha.Picha: picture-alliance/dpa/S. Pantzartzi

Atetea mpango tata 'B' wa Grexit

Wakati huo huo, waziri mkuu Tsipras hii leo amekiri kuwa serikali yake ilikuwa imeandaa mpango wa dharura wa siri iwapo Ugiriki ingelaazimishwa kutoka katika kanda inayotumia sarafu ya euro, lakini amepinga tuhuma kwamba alipanga njama za kuirejesha nchi hiyo kwenye sarafu yake ya zamani ya drachma.

Mpango huo ulifichuliwa hivi karibuni na waziri wa zamani wa fedha Yanis Varoufakis, na ulihusisha mikakati ya kuvunja tarakimu za siri za kodi za raia ili kuunda mfumo mbadala wa malipo, na kusababisha mshtuko na ghadhabu nchini Ugiriki.

Tsipras ameufananisha mpango huo na nchi inayoandaa mifumo yake ya ulinzi kuelekea vita, akisema lilikuwa jukumu la serikali inayowajibika kuwa na mpango wa dharurua.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,dpae

Mhariri: Mohammed Khelef