1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Syria yatumbukia mashakani

25 Januari 2016

Mazungumzo ya amani ya Syria yaliyotarajiwa kuanza leo jijini Geneva yamekwamishwa na tofauti kuhusu ni nani anayepaswa kukaa katika meza ya mazungumzo

https://p.dw.com/p/1HjIs
USA Russland John Kerry mit Sergej Lawrow Syrien Gespräche in Zürich
Picha: Getty Images/AFP/J. Martin

Saudi Arabia, Uturuki na Urusi, pamoja na waasi wa Syria na Wakurdi, wote wanatofautiana. Suala la ni nani anastahili kukaa kwenye meza ya mazungumzo limeangazia ugumu uliopo katika kuendeleza mchakato wa kutafuta amani ya Syria ambao ulitarajiwa kuanza leo katika mazungumzo ya Geneva, lakini sasa utacheleweshwa, au hata kufutwa, baada ya miezi mingi ya shughuli ngumu za kidiplomasia.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry amesema anataraji kuwa kutakuwa na “uwazi” katika kipindi cha saa 24 hadi 48 kuhusu mazungumzo ya amani akisema kuwa ni vyema kuyachelewesha kwa siku kadhaa kuliko yasambaratike hata kabla ya kuanza.

Grenzkontrolle an jordanischer Grenze zu Syrien
Majeshi ya Serikali ya Syria yameukomboa mji wa RabiaPicha: Getty Images/AFP/K. Mazraawi

Kerry amewaambia wanahabari akiwa ziarani Laos kuwa amekubaliana na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura kuwa mialiko kwa ajili ya mazungumzo hayo haipaswi kutumwa hadi pale “tofauti zote zilizopo zitakapotatuliwa”.

Kerry ameongeza kuwa mustakabali wa mazungumzo hayo umo mikononi mwa pande husika za Syria.

Serikali ya Syria inasema iko tayari kuhudhuria, lakini Kamati Kuu ya Mazungumzo katika mazungumzo hayo, ambayo inayajumuisha makundi ya kisiasa na wapinzani wa Rais Bashar al-Assad, inasema haitahudhuria hadi pale serikali itasitisha mashambulizi yake, iondowe vizuizi, na iwaachilie huru wafungwa – hatua ambazo zimetajwa kwenye azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema mazungumzo hayo yajayo yanapaswa kuwajumuisha waasi wa Kiislamu, lakini sio magaidi na Waislamu wenye itikadi kali. Steinmeier alinukuliwa na gazeti la Frankfurter Allgemeine Sontagszeitung kuwa ni vigumu sasa kuyapata makundi yenye misimamo ya wastani baada ya zaidi ya miaka mitano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, machafuko makubwa na kusambaa kwa ukatili.

Ndani ya Syria kwenyewe, wanajeshi watiifu kwa serikali wakiswaidiwa na mashambulizi ya angani ya Urusi, wameukomboa mji wa mwisho uliokuwa mikononi mwa waasi katika mkoa wa pwani wa Latakia. Televisheni ya taifa ya Syria imesema jeshi, likishirikiana na wapiganaji wanaoiunga mkono serikali, walichukua udhibiti wa mji wa Rabia jana Jumapili baada ya mapambano makali na waasi.

Ulikuwa ushindi wa pili wa kimkakati kwa majeshi ya serikali katika mkoa wa Latakia katika muda wa chini ya wiki mbili, baada ya kuukomboa mji wa Salma mnamo Januari 12.

Shirika linalofuatilia haki za binaadamu la Syria, limesema mji wa Rabia ulikombolewa baada ya majeshi ya serikali kuuzingira na kukamata vijiji 20 vya eneo hilo. Limeongeza kuwa ndege za kivita za Urusi zilichangia katika mafanikio hayo kupitia mashambulizi ya anga.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga