1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Syria mashakani

16 Februari 2014

Msuluhishi wa kimataifa Lakhdar Brahimi ameyafunga mazungumzo ya ana kwa ana kati ya serikali ya Syria na upinzani Jumamosi(15.02.2014) bila ya kupata ufumbuzi wa kuyakwamua mazungumzo hayo ya amani.

https://p.dw.com/p/1B9mX
Msuluhishi wa kimataifa Lakhdar Brahimi
Msuluhishi wa kimataifa Lakhdar BrahimiPicha: picture-alliance/dpa

Mazungumzo ya Jumamosi ambayo yamechukuwa pungufu ya nusu saa yanauweka mustkakbali wa mchakato huo mashakani na hakuna tarehe iliowekwa kwa ajili ya duru ya tatu.

Baadaye Brahimi ambaye ni mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za Kiarabu kuhusu Syria aliuambia mkutano wa waadishi wa habari kwamba amependekeza ajenda ya duru nyingine ya mazungumzo wakati itakapofanyika ambayo kwanza italenga suala la kukomesha ghasia na ugaidi na baadae juu ya namna ya kuunda serikali ya mpito,asasi za kitaifa na usuluhsihi wa kitaifa.

Hata hivyo amesema kwa bahati mbaya serikali ya Syria imekataa na imekuwa kwanza ikitaka lishughulikiwe suala la kukomesha ugaidi na kugoma kushughulikia suala lolote lile jengine hadi hapo suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.

Aomba radhi

Ameomba radhi kwa duru hizo mbili za mazungumzo kushindwa kuzaa matunda ya maana.

Lakhdar Brahimi mjumbe wa kimataifa kwa Syria akizungumza na waandishi wa habari Geneva. (15.02.2014).
Lakhdar Brahimi mjumbe wa kimataifa kwa Syria akizungumza na waandishi wa habari Geneva. (15.02.2014).Picha: Reuters

Brahimi amekaririwa akisema "Nafikiri ni vizuri kila upande kurudi nyumbani na kutafakari wajibu wao kuona iwapo wanataka mchakato huo uendelee au la."

Ameongeza kusema "Sio vizuri kwa mchakato huo ,sio vizuri kwa Syria kwamba wamerudi tena kwenye duru nyengine ya mazungumzo na kutumbukia kwenye mitego ile ile ambayo wamekuwa wakihangaika kujinasua."

Lakini pia ameweka wazi kwamba hataki kuona kupoteza wiki nyengine au zaidi kabla ya kuanza tena kwa mazungumzo hayo.

Msuluhishi huyo mkongwe wa amani amesema mapumziko katika mazungumzo hayo yalikuwa yanahitajika.

Duru hii ya mazungumzo imedumu kwa siku sita mfululizo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa Ulaya yalioko Geneva wakati umwagaji damu ukiendelea kwa wananchi wa Syria huko nyumbani.

Kipindi cha mpito

Msemaji wa upinzani Louay Safi amewaambia waandishi wa habari mazungumzo mapya ya amani ya Syria yatakuwa hayana maana iwapo serikali ya nchi hiyo itaendelea kugoma kujadili kipindi cha kisiasa cha mpito.

Louay al-Safi msemaji wa upinzani wa Syria.
Louay al-Safi msemaji wa upinzani wa Syria.Picha: imago/Xinhua

Amesema duru ya tatu bila ya kuzungumzia serikali ya mpito itakuwa ni kupoteza wakati.

Mjumbe mwengine wa upinzani katika mazungumzo hayo Anas al-Abdeh amesema upande wake umeikubali agenda iliopendekezwa na Brahimi lakini kugoma kwa serikali kuizingatia kumeyaweka mashakani mazungumzo ya duru ya tatu.

Ameongeza kusema pale tu watakapojuwa kwamba wana mshirika wa kweli katika mazungumzo hayo ambaye ana utashi wa kuzungumza kuhusu ufumbuzi wa kisiasa ndipo kutakapokuwa na duru nyengine.

Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema leo idadi ya vifo kutokana na mzozo huo wa miaka mitatu imefikia 140,000.

Inaripotiwa kwamba zaidi ya watu 3,400 wameuwawa mwezi huu wakati mazungumzo hayo ya amani yakiendelea mjini Geneva.

Brahimi anatarajiwa kushauriana na Marekani na Urusi wadhamini wakuu wa mkutano huo wa amani na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon pamoja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuona namna ya kuendelea mbele na mazungumzo hayo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AP/Reuters

Mhariri:Caro Robi