1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kufufua mkataba wa nyuklia na Iran yafanyika

7 Aprili 2021

Maafisa wa Iran na wawakilishi wa madola yenye nguvu wamefanya kile walichokitaja kuwa mazungumzo ya "manufaa" mjini Vienna kujaribu kufufua mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 ambao utekelezaji wake umetetereka. 

https://p.dw.com/p/3reWb
Österreich Wien |  Atom-Konferenz
Wawakilishi wa Iran na madola yenye nguvu wakishiriki majadiliano mjini Vienna Picha: Askin Kiyagan/AA/picture alliance

Kwenye mazungumzo hayo ya mjini Vienna pande zote mbili zimesema kwa nyakati tofauti kuwa majadiliano yalikuwa ya kujenga lakini bado ni mapema mno kujadili matokeo yake.

Mratibu mkuu wa majadiliano kutoka Umoja wa Ulaya Enrique Mora aliandika kupitia ukurasa wa Twitter kwamba kuna ishara zote za mshikamano na nia ya kutatua mkwamo uliopo kupitia njia za kidiplomasia na kwamba mjadala ulikuwa wa manufaa.

Maneno sawa na hayo yametolewa pia na mkuu wa mazungumzo ya nyuklia wa Iran Abbas Araqchi alipozungumza na kituo cha televisheni cha nchi yake.

Mazungumzo hayo ya siku ya Jumanne yaliijumuisha Iran na mataifa yaliyosalia kwenye mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 ambayo ni Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, China na Urusi chini ya uratibu wa Umoja wa Ulaya.

Wawakilishi wa Marekani ambayo hadi mwaka 2018 ilikuwa sehemu ya mkataba huo hawakujumuika na wajumbe wengine kwenye chumba cha  mashauriano lakini walipatiwa taarifa baada mazungumzo kumalizika

Hatua ya awali ya mazungumzo inatia moyo 

Iran Atomabkommen l  Schwerwasser-Produktionsanlage im zentraliranischen Arak
Mradi wa nyuklia wa Iran unatiliwa mashaka na madola makubwa duniani.Picha: picture alliance/AP/ISNA/A. Khamoushi

Wajumbe wa pande zilizohudhuria majadiliano hayo wamekubaliana kuunda vikosi kazi viwili vitakavyojadili vikwazo ambavyo Marekani inaweza kuviondoa na maeneo ambayo Iran inaweza kupunguza shughuli zake za nyuklia.

Wawakilishi wa mataifa ya Ulaya yaliyotia saini mkataba wa nyuklia na Iran wanajaribu kuzishawishi Marekani na Iran kurejea kwenye utekelezaji wa mkataba huo ambao uliondoa vikwazo dhidi ya Iran kwa sharti kwamba nchi hiyo ipunguze shughuli kwenye mradi tata wa nyuklia.

Lakini mambo yalikwenda mrama baada ya utawala wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump uliiondoa nchi hiyo kwenye mkataba huo mwaka 2018 na kurejesha vikwazo vya kiuchumi kwa Iran hatua iliyolazimisha Tehran kuacha kutekeleza masharti ya makubaliano na kuanza tena kurubisha madini ya Urani.

Kila upande wakiri kuwa mambo hayatokuwa mepesi 

Iran Atomabkommen
Picha: picture-alliance/epa/D. Calma

Ingawa mataifa hayo hasimu yaan Marekani na Iran yamekwishasema kwamba hayatarajii mafanikio ya haraka kuhusu mvutano uliopo, serikali zote mbili lakini zimesema mashauriano ya awali mjini Vienna yanatia moyo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Ned Price aliwaambia waandishi habari mjini Washington kuwa wameyakaribisha mashauriano hayo ya awali aloyataja kuwa muhimu lakini amesisitiza kwamba nchi hiyo inaamini mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yatakuwa magumu.

Kauli yake inafuatia msimamo ulioelezwa na Iran kuwa bado haiko tayari kukutana ana kwa ana na Marekani kwa ajili ya mashauriano.

Maafikiano yoyote yatakayowezesha Iran kuachana na mpango wake wa nyuklia yatasaidia sana kupunguza mvutano kwenye kanda ya Mashariki ya Kati hususani kati ya Iran na hasimu wake Israel pamoja na mataifa mengine ya kiarabu yenye waislamu wengi wa Sunni kama Saudi Arabia wanaotiwa shaka na uwezekano wa Tehran kutengezea silaha za nyuklia.