1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Amani Yemen

John Juma23 Mei 2016

Watu 41 wameuawa Yemen kufuatia milipuko miwili. Kundi la Dola la Kiislamu limedai kutekeleza mashambulizi hayo. Haya yanajiri huku mazungumzo ya amani kati ya serikali na waasi yakianza upya baada ya kutibuka wiki jana.

https://p.dw.com/p/1It9Q
Eneo la shambulizi.
Eneo la shambulizi.Picha: picture-alliance/dpa

Milipuko miwili ambayo kundi la Dola la Kiislamu limedai kuhusika dhidi ya vikosi vya serikali ya Yemen mjini Aden imeua watu 41. Mashambulio hayo yanajiri baada ya operesheni kuu iliyofanywa na vikosi vya serikali dhidi ya makundi ya Jihad kusini na kusini mashariki ya Yemen.

Kulingana na afisa wa ngazi ya juu ya jeshi la Yemen Brigedia Generali Nasser al-Sarei, shambulizi la kwanza lilifanywa na mlipuaji wa kujitoa mhanga aliyeua watu 34 waliopanga foleni kujisajili katika kituo cha Badr. Shambulizi la pili likatokea ndani ya kambi ya jeshi ambako wanajeshi 7 waliuawa.

Mkaazi mmoja wa Aden ameelezea taswira ya eneo lililoshambuliwa kuwa mbaya sana, akisema ameona vipande vya miili ya watu vilivyokatika vikitapakaa mita kadhaa baada ya kulipuliwa.

Kupitia taarifa iliyochapishwa mtandaoni, kundi la Dola la Kiislamu ambalo limeziteka sehemu nyingi za Syria na Iraq limedai kutekeleza mashambulizi hayo Yemen, kando na mashambulizi yaliyoua zaidi ya watu 100 nchini Syria.

Vikosi vitiifu kwa rais Abedrabbo Mansour Hadi, ambavyo pia vinaungwa mkono na Saudi vinayakabili makundi mawili ya madhehebu ya Sunni na Shia, makundi ambayo yafuata itikali kali kidini.

Afisa wa Umoja wa Mataifa akihimiza mazungumzo.
Afisa wa Umoja wa Mataifa akihimiza mazungumzo.Picha: Getty Images/AFP/Y.Al-Zayyat

Mji wa Aden umeshuhudia mashambulizi mengi katika miezi ya hivi karibuni kutoka kwa mtandao wa A-Qaeda au Dola la kiislamu. Mapema mwezi huu polisi 47 waliuawa katika misururu ya milipuko karibu na eneo la Mukalla.

Mazungumzo ya amani

Mashambuli ya Aden yanajiri wakati mazungumzo kati ya serikali na waasi yakianza tena nchini Kuwait. Mazungumzo hayo yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa yalitibuka wiki jana.

Serikali ilitaka waasi na washirika wao watie saini kiapo cha kutambua makubaliano yaliofikiwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa yaliyowataka kujiondoa katika jiji kuu na ngome nyinginezo wanazozishikilia. Serikali iliwalaumu waasi kwa kutotimiza kikamilifu makubaliano hali iliyozua mkutano kuvunjika.

Hata hivyo waziri wa mambo ya kigeni nchini Yemen Abdulmalek al-Mikhlafi alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa serikali imekubali kufanya mazungumzo ya amani kama hatua ya mwisho. Ameongeza kuwa “tumevipitia vipengelee vyote. Hii ni hatua ya kwanza ya kupatikana kwa amani kamili itakayowezesha maamuzi ya 2016 kuanza kwa kujiondoa kwa waasi na kusalimimisha silaha na kukuza upya asasi za serikali”.

Naye Ismail Ould Cheikh Ahmed kupitia ukurasa wake wa Twitter aliisema mkutano wa wajumbe kutoka pande zote mbili wa Amani ya Yemen umeshaanza. Hii ni baada ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, Mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani na wajumbe maalum wa Umoja wa mataifa kuwashawishi kushiriki mazungumzo.

Eneo la Aden.
Eneo la Aden.Picha: Getty Images/AFP/S. Al-Obeidi

Mabomu yaliyoachwa kiholela

Shirika la kutetea haki za kibinadamu Amnesty International limesema mabomu ambayo yalirushwa na m´vikosi muungano vya Saudi na Yemen lakini hayakulipuka, yameathiri watu hasa watoto ambao wameuawa na wengine kulemazwa. Shirika hilo linahimiza usaidizi wa kimataifa kuyaondoa mabomu katika sehemu mbalimbali na vikosi hivyo kuacha kutumia mabomu hayo.

Kwenye taarifa yao, shirika hilo limesema “Nchi zenye ushawishi zinapaswa kuihimiza Saudi Arabia na washirika wake kukoma kutumia mabomu ambayo yamepigwa marufuku yasitumike kimataifa” limeongeza kuwa familia zipo katika hatari kuu ya kujeruhiwa vibaya na hata vifo wanaporudi kaskazini ya Yemen kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoafikiwa mwezi Machi. Tangu muungano wa vikosi vya Yemen na Saudi Arabia kuanza mashambulizi dhidi ya makundi yenye misimamo mikali Machi mwaka 2015, zaidi ya watu 6,500 wameuawa, milioni 2.8 wamepoteza makwao huku asilimia 82 ya wayemeni wakihitaji misaada. Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa.

Licha ya mashambulizi ya Yemen ikisaidiwa na Saudi Arabia, waasi wangali wanadhibiti maeneo yenye idadi kubwa ya wayemeni likiwemo maeneo ya milima ya kati na kaskazini na pwani ya bahari ya Shamu.

Mwandishi: John Juma /AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman