1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini kuanza

Mjahida2 Januari 2014

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ethiopia imesema pande mbili hasimu za Sudan Kusini zinakutana leo kwa mara ya kwanza mjini Addis Ababa kwa mazungumzo ya amani.

https://p.dw.com/p/1AkH8
Mwanajeshi wa Sudan Kusini
Mwanajeshi wa Sudan KusiniPicha: Reuters

Ethiopia imejivika jukumu la kuhakikisha pande hizo mbili hasimu zinajadili mpango wa kuleta amani Sudan Kusini. Hata hivyo juhudi hizo zimegubikwa na mapigano yanayoendelea katika baadhi ya maeneo nchini humo.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ethiopia amesema kwamba mazungumzo hayo yanatarajiwa kuanza hii leo huku mazungumzo rasmi ya upatanishi yakiwa hayajulikani yataanza lini.

Kulingana na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Hilde Johnson, ni jambo la kuleta matumaini kuona kwamba makundi yote mawili hasimu yanapeleka wajumbe wake kwa mazungumzo ya amani baada ya mapigano yaliosababisha maelfu kuuwawa huku zaidi ya watu 200,000 wakikimbia makaazi yao.

" Tumeshuhudia visa vibaya vya ghasia katika wiki mbili za mapigano na tunafahamu kwamba iwapo hakuna mtu yeyote atakayewajibishwa basi kuna hatari ya kuendelea kwa ghasia zaidi," Alisema Hilde Johnson.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ethiopia Tedros Adhanom
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ethiopia Tedros AdhanomPicha: picture-alliance/dpa

Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa Hilde Johnson ameendelea kusema kwamba kitu wanachojaribu ni kuzuwiya mapigano zaidi, ndio maana wametuma vikosi vyao kusaidia kushika doria katika makambi.

Amesema kitu wanachokifanya kwa sasa ni kutafuta silaha zozote zilizopo na kuhakikisha kuwa kambi ni salama na pia ulinzi umeimarishwa.

Mapigano Sudan Kusini yalianza Desemba 15 wakati rais wa nchi hiyo Salva Kirr alipomshutumu makamu wa rais wa zamani Riek Machar, kwa kujaribu kumpindua. Machar alikana vikali madai hayo na hali ilichochoea mapigano kati ya Kabila la Dinka anakotokea Rais Salva Kirr na kabila la Nuer la Riek Machar.

Rais Salva Kirr atangaza hali ya hatari

Wakati huo huo rais Kirr ametangaza hali ya hatari katika majimbo mawili ya Unity na Jonglei maeneo ambayo vikosi viloivyotiifu kwa makamu wa rais wa zamani Riek Machar vinadhibiti.

Serikali ya taifa hilo jipya na changa duniani inaendelea kutuma jeshi lake mjini Bor kupambana na waasi na kujaribu kuudhibiti tena baada ya kutwaliwa na waasi siku ya Jumanne wiki hii.

Riek Machar na rais Salva Kirr
Riek Machar na rais Salva KirrPicha: Reuters

Mapigano yameendelea kusambaa na kufikia majimbo 10 huku maelfu ya watu wakiuwawa katika wiki mbili za mapigano.

Awali Rais Kirr alinukuliwa katika mahojiano aliofanya na shirika la utangazaji la Uingereza BBC, akisema kwamba wamekuwa wakipigana kwa muda mrefu kwa hivyo kitu kilicho muhimu sasa ni kutafuta suluhu ya mgogoro ili raia wa Sudan Kusini warejee makwao na kuishi kwa amani.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP/dpa

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman