Mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran kuanza leo Geneva | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.12.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran kuanza leo Geneva

Hakutarajiwi mafanikio makubwa wakati wa mazungumzo ya leo na kesho mjini Geneva na wanadiplomasia wanasema makubaliano ya kukutana tena kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo, yatakuwa ishara ya mafanikio

default

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton (kushoto) na mpatanishi mkuu wa Iran, Saed Jalili

Mazungumzo ya pande sita kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yanaanza leo mjini Geneva Uswisi baada ya kukwama kwa zaidi ya mwaka mmoja. Mkutano huo wa siku mbili utazileta pamoja Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani.

Mkutano huo wa siku mbili kati ya Wairan na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Bi Catherine Ashton anayeungwa mkono na Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani, utaashiria kumalizika kwa miezi 14 ya kusita kwa mazungumzo hayo, kwa sababu ya hatua ya Iran kukataa pendekezo la kuacha kurutubisha madini yake ya uranium ili ipewe nishati ya nyuklia.

Mpatanishi mkuu wa Iran katika mzozo huo wa nyuklia, Saed Jalili, aliwasili jana mjini Geneva, kwa duru mpya ya mazungumzo, akiwa ameandamana na naibu wake, Ali Begheri, na naibu waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Iran anayehusika na masuala ya Ulaya, Ali Ahani.

Ingawa mataifa sita yanakutana na Iran kwenye meza ya mazungumzo, ajenda ya mazungumzo haiko wazi. Siku chache zilizopita Iran ilitaka ajenda ya mazungumzo ielezwe kwanza kabla kuhudhuria mikutano katika siku za usoni.

Iran haitaacha mpango wake

Mwishoni mwa wiki iliyopita rais wa Iran, Mahmoud Ahamedinejad alisisitiza tena kwamba Iran haitakubali kuachana na mpango wake wa nyuklia na kusema mipango ya kurutubisha uranium sio suala la kujadiliwa. "Tunatumia tu haki yetu kwa mujibu wa mkataba wa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia. Hatuzidishi wala hatupunguzi hata kidogo."

Kwa mujibu wa mkataba wa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia, kimsingi Iran ina haki ya kutumia madini ya uranium kwa matumizi ya amani na kutumia ujuzi wa atomiki. Lakini sivyo kwa mataifa sita yanayosimamia mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran pamoja na shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia, IAEA, linaloishuku Iran kuwa inatumia mpango wake wa nyuklia kisiri kwa matumizi ya kijeshi.

Na ndio maana shirika la IAEA linataka lihurusiwe kuchunguza vinu vya nyuklia vya Iran bila kuwekewa vikwazo. Mwishoni mwa wiki iliyopita mkuu wa shirika hilo, Yukiya Amano alitaka kuwepo uwazi zaidi kutoka kwa Iran, ambayo mkuu wake wa ujasusi, Heydar Moslehi alilishutumu shirika la IAEA kwa kutaka kupeleka majasusi nchini Iran.

USA Außenministerin Hillary Rodham Clinton

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani Hillary Rodham Clinton

Akizungumza mwishoni mwa juma kwenye mkutano kuhusu usalama unaojulikana kama "Mdahalo wa Manama", nchini Bahrain, waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, alisema msimamo wa jumuiya ya kimataifa kuhusu Iran uko wazi.

"Muna haki kuwa na mpango wa nyuklia kwa matumizi ya amani. Lakini haki hiyo inakuja na jukumu la kutii mkataba mliosaini na kushughulikia kikamilifu wasiwasi wa dunia kuhusu shughuli zenu za nyuklia. Tunawahimiza mupitishe uamuzi huo kwa ajili ya watu wenu, mashilahi yenu na usalama wetu sote."

Hakuna matarajio makubwa

Wanadiplomasia hawatarajii mafanikio makubwa wakati wa mazungumzo ya leo na kesho mjini Geneva na wanasema makubaliano ya kukutana tena kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo, yatakuwa ishara ya mafanikio.

Mkutano wa Geneva unafanyika siku moja tu baada ya Iran kutangaza hapo jana kwamba imepiga hatua kubwa mbele katika mpango wake wa nyuklia, hivyo kuashiria kuwa haina nia ya kuachana na mpango wake huo, ambao inasisitiza ni kwa ajili ya matumizi ya amani ya uzalishaji wa nishati.

Mwandishi: Pick, Ulrich/ Nyiro Charo, Josephat

Mpitiaji: Hamidou Oummilkheir

 • Tarehe 06.12.2010
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/QQMd
 • Tarehe 06.12.2010
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/QQMd

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com