1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maziwa makuu wakubaliana kuhusu madini

Admin.WagnerD24 Februari 2020

Nchi za maziwa makuu zimekubaliana kuwa na utaratibu unaofanana katika kuwasajili wawekezaji wa sekta ya madini ili kuondoa ushindani miongoni mwa nchi wananchama.

https://p.dw.com/p/3YHNq
Mineral Coltan / Koltan
Picha: Imago Images/photothek/M. Gottschalk

Mwaka 2004 ulianzishwa ushirika wa ukanda wa nchi za maziwa makuu ICGLR wakiwa na makubaliano katika maeneo kumi na moja ikiwemo itifaki ya uzuiaji wa uvunaji haramu wa rasilimali ikiwemo madini.

Itifaki hiyo inatoa sababu kwa nchi ya Tanzania ambayo hivi karibuni imefanya maboreshi kadhaa ya sheria zake za madini kuwa mwenyeji wa mkutano wa pili ambapo katika awamu hii wameangazia mbinu za kukabiliana na utoroshwaji madini kuelekea nje ya mataifa hayo.

Mwenyekiti wa mawaziri wa madini katika ukanda huo ambae pia ni waziri wa madini wa Uganda Sara Opendi ameuambia mkutano kuwa mbali na kukubaliana kuwekeza katika rasilimali watu, vifaa na hata elimu kuna haja wakati huu kuwa na utaratibu unao fanana katika usajili wa wawekezaji ili kuzuia ushindaji kati ya nchi na nchi unaotoa mwanya kwa wahalifu kutekeleza azma yao ya utoroshwaji wa rasilimali hiyo.

baadhi ya nchi wanachama kama vile Tanzania na DRC zimetajwa kuwa ni miongoni mwa mataifa yalio ndani ya ukanda huo yanayopoteza mamilioni ya dola kutokana na utoroshwaji wa madini,huku kwa taifa la DRC biashara hiyo ikitajwa kufadhili makundi mbalimbali ya uhalifu yenye kumiliki silaha na matokeo ya kuhatarisha amani ya raia.

Mtendaji mkuu wa ICGLR balozi Zacharia Muita akizungumza katika kilele cha mkutano huo amesema mikakati ya ushirikiano kati ya nchi wananchama ndio inayotazamiwa ili kulinda rasilimali na usalama katika ukanda huo.

Hata hivyo macho ya wachambuzi wa masuala ya kiuchumi mbali na kuona mfumo wa sera zinazoranda kuwa kiini cha kukabiliana na utoroshwaji wa madini bado wanapigia chepuo kukabiliana na hali ya rushwa katika ukanda huo ambao nayo imetajwa kuwa ni sababu ya kushamiri kwa vitendo hivyo.

Tanzania kupitia waziri mkuu wake Kassim Majaliwa ameuambia mkutano huo uliobeba kauli mbiu ya uwekezaji na ushirikiano endelevu katika sekta ya madini kuwa, katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali kupitia sekta ya madini imeweza kukusanya sh. bilioni 242.53 sawa na asilimia 51.5 ya lengo la mwaka la kukusanya sh. Bilioni 470.89.