1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazishi ya muandishi vitabu wa kirusi Soljenitsyne

Hamidou, Oumilkher5 Agosti 2008

Warusi wamuaga shujaa aliyesubutu kuukosoa utawala wa zamani wa Usovieti

https://p.dw.com/p/Eqmn
Jeneza na picha ya muandishi vitabu Alexander SoljenitsynePicha: AP


        Maiti ya muandishi habari wa kirusi Alexander SOLJENITSYNE  imewekwa katika ukumbi wa chuo kikuu cha sayansi hii leo kupokea heshma za mwisho kabla ya kuzikwa katika kiunga cha makaburi cha DONSKOI mjini Moscow hapo kesho.


Jeneza alimolazwa mshindi huyo wa tuzo ya fasihi ya Nobel,limeachwa wazi na kuwekwa katika vigazi ili kuuwezesha umati wa watu,tangu raia wa kawaida mpaka viongozi mashuhuri ,kumuaga kwa siku nzima hii leo.


Watu wasiopungua 200,wengi wao wakiwa wazee,wanaongozana mbele ya jeneza lililopambwa,pakiweko picha kubwa ya Alexander Soljenitsyne.


Mwili wake umefunikwa mauwa na mengine kupambwa chini ya jeneza linalozungukwa na wanajeshi wa kikosi cha heshima.


Waziri mkuu Vladimir Putin alikua miongoni mwa viongozi wa serikali waliofika kumpa heshma za mwisho muandishi vitabu huyo.


Alexander Soljenitsyne  aliyefariki dunia usiku wa jumapili kuamkia jumatatu akiwa na umri wa miaka 89,aliukosoa vikali utawala wa Usovieti hapo zamani na kuandika maovu yote katika vitabu vyake ikiwa ni pamoja na kile alichokipa jina "Visiwa vya Gulag na banda la wenye kensa."


Vitabu vyake vilimpatia zawadi ya fasihi ya Nobel mnamo mwaka 1970 kabla ya kupokonywa miaka minne baadae uraia wake wa kirusi na kufukuzwa nchini mwake.Aliiishi miaka 20 uhamishoni nchini Ujerumani,Uswisi na baadae nchini Marekani kabla ya kurejea Urusi katika mwaka 1994.


Kifo chake kimezusha huzuni kote ulimwenguni.Mwanawe anasema kifo chake kimesababisha hasara sio tuu kwa familia bali kwa Urusi nzima.



Rambi rambi zinamiminika kutoka kila pembe ya dunia.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice amesifu  kile alichokiita "sauti moja wapo muhimu ya karne ya 20 katika mapambano dhidi ya tawala za kimabavu."