1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May akabiliwa na shinikizo la kujiuzulu

Sylvia Mwehozi
9 Juni 2017

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ametakiwa kujiuzulu baada ya kupoteza wingi wa viti bungeni, na hivyo kuifanya nchi hiyo kutokuwa na uhakika wakati mazungumzo ya kujiondoa Umoja wa Ulaya yakikaribia kuanza. 

https://p.dw.com/p/2eONH
Großbritannien Wahlen 2017 May
Picha: Reuters/T. Melville

Kulingana na matokeo katika majimbo 647 yaliyokwisha hesabiwa, hakuna chama kilichoko katika nafasi ya kushinda wingi wa viti 326 vinavyohitajika katika bunge lenye viti  650.

Chama cha Conservative kimeshinda viti 316 huku chama pinzani cha Labour kikinyakua viti 261 na chama cha Scottish National Party kiko nafasi ya tatu na viti 35. Kabla ya kufanyika uchaguzi huo Conservative ilikuwa na viti 330 na Labour ikiwa na viti 229. Hii inamaanisha Conservative kitahitaji uungwaji mkono wa vyama vidogo ili kuongoza.

Matokeo hayo ni aibu kwa Waziri Mkuu Theresa May ambaye aliitisha uchaguzi wa mapema kwa matumaini ya kuimarisha mamlaka yake ya kumuwezesha mchakato wa majadiliano ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya. Hata hivyo vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa kiongozi huyo "hana mpango wa kujuzulu" na atatoa hotuba yake baadae leo.

May ambaye amechaguliwa tena kwa wingi wa kura katika jimbo lake la Maidenhead amesema Uingereza inahitaji utulivu kwa sasa.

"Wakati tunasubiria matokeo ya mwisho, ninajua kama nilivyosema, nchi inahitaji kipindi cha utulivu na matokeo yoyote yatakavyokuwa, Conservative itahakikisha inatimiza wajibu wake wa utulivu ili kwa pamoja kama nchi tusonge mbele asante," amesema Waziri Mkuu May.

London Labour Führer Jeremy Corbyn
Kiongozi wa chama cha Labour Jeremy CorbynPicha: Getty Images/C. Furlong

Kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn naye amechaguliwa tena katika jimbo lake la London lakini akamtaka May kujiuzulu akisema "anapaswa kupisha serikali ambayo ina uwakilishi wa kweli wa watu wote katika nchi hiyo" na kwamba wako tayari kuwatumikia wananchi waliowaamini. Matokeo haya yamewafadhaisha wote waliomuona kiongozi huyo wa Labour kuwa kama sumu. Chama hicho kilijiongezea umaarufu katika wiki za miwsho za kampeni.

"Ni matokeo mazuri kwa chama cha Labour kwasababu watu walipiga kura kwa matumaini. Vijana kwa watu wazima wote waliungana jana, wakajitokeza kwa wingi, na kuipatia labour kura nyingi na walifanya hivi kwasababu wanataka kuona mambo yanafanywa kwa tofauti na wanataka matumaini katika maisha yao," amesema kiongozi huyo. 

Kuna tetesi kuwa chama cha Democratic Union DUP cha Ireland ya kaskazini ambacho kimeshinda viti 10 katika bunge kinaweza kukiunga mkono chama cha Conservative katika uundaji wa serikali, ingawa wanasiasa wa chama hicho hawajatoa maelezo yoyote kuhusu hilo.

Matokeo hayo yamekuwa na mshangao mwingi ambapo naibu waziri mkuu wa zamani na kiongozi wa zamani wa chama cha Liberal Democrats Nick Clegg ameshindwa katika jimbo lake la Sheffield.

Thamani ya  sarafu ya pauni ilianguka dhidi ya dola ya Kimarekani na sarafu ya Euro katika masoko ya fedha ya kimataifa, wakati wawekezaji wakihoji nani  hatimaye ataongoza  mchakato wa mazungumzo ya Brexit.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman