1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri zaidi wateuliwa Kenya

25 Aprili 2013

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza majina ya mawaziri wapya 12. Miongoni mwao ni mwanadiplomasia Raychelle Omamo aliyepewa wadhifa wa waziri wa ulinzi. Bado wizara mbili hazijapewa viongozi.

https://p.dw.com/p/18NLZ
Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya
Uhuru Kenyatta, Rais wa KenyaPicha: Getty Images

Uteuzi uliotangazwa leo unatimiza idadi ya mawaziri 16 kati ya 18 ambao wataunda baraza la kwanza la mawaziri tangu kuchaguliwa kwa Uhuru Kenyatta kuwa rais.

Wanasiasa wa muda mrefu Charity Ngilu na Najib Balala wamo kwenye orodha iliyotangazwa leo. Ngilu ataiongoza wizara ya ardhi, huku Balala akielekea katika wizara ya madini na migodi. Michael Kamau ndiye waziri mpya wa usafirishaji, wakati mtaalamu wa maswala ya uchumi, Phyllis Chepkoskey Kandie, akipewa wizara ya utalii. David Chirchir amekabidhiwa wizara ya nishati na mafuta.

Maswali juu ya ukabila

Baraza jipya limezusha maswali juu ya namna wengi wa mawaziri walioteuliwa wanavyotoka katika makabila ya Kikuyu na Kalenjin, ya rais Uhuru Kenyatta na makamu wake, William Ruto. Akijibu maswali ya waandishi wa habari juu ya wasiwasi huo, Rais Kenyatta amesema wamejaribu kuweka uwakilishi wa majimbo yote ya nchi kwa kadri ya uwezo wao. ''Kwa bahati mabaya baraza hili sio kubwa kama yale yaliyotangulia,'' alisema Kenyatta.

Makamu wa rais wa Kenya William Ruto
Makamu wa rais wa Kenya William RutoPicha: AP

Jumanne wiki hii, Rais Kenyatta alikuwa ameteua waziri wa fedha, waziri wa mambo ya nchi za nje, waziri wa habari na waziri wa afya. Wizara ambazo bado zinasubiri kujua watakaoziongoza ni ile ya utumishi, usalama wa kijamii na huduma kwa umma, pamoja na wizara ya mambo ya ndani na tawala za majimbo.

Wasiwasi juu ya uteuzi nusu nusu

Maswali yamekuwa yakiulizwa kuhusu sababu ya kulitangaza baraza la mawaziri hatua kwa hatua. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Kenya Bobby Mkangi, ameiambia DW kuwa changamoto kubwa inatokana na utekelezwaji wa makubaliano kati ya rais Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto, ambayo yanasema vyama vyao vitagawana madaraka nusu kwa nusu.

Amina Mohamed ni miongoni mwa mawaziri wapya, anayeongoza wizara ya mambo ya nje
Amina Mohamed ni miongoni mwa mawaziri wapya, anayeongoza wizara ya mambo ya njePicha: Getty Images

Kabla ya kupitishwa rasmi, mawaziri wateule watachunguzwa na kamati ya bunge, inayowajumuisha maspika wa bunge na seneti pamoja na wabunge kutoka mabaraza hayo mawili. Hata hivyo, muungano wa kisiasa wa Jubilee wa rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake unao wingi wa wabunge katika mabaraza hayo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/ Interview

Mhariri: Josephat Charo