Mawaziri wa ulinzi watathimini mapambano dhidi ya IS
26 Oktoba 2016Mawaziri hao wa ulinzi walikuwa wanakutana mjini Paris jana, kutathmini hali ya vita dhidi ya kundi hilo baada ya zaidi ya miaka miwili ya mashambulio ya anga,mafunzo pamoja na ushauri kwa wanajeshi wanaopambana katika vita vya kuukomboa mji wa Mosul.
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alikuwa akikutana na mawaziri wenzake pamoja na waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter katika kutathmini kazi iliyofanywa na muungano huo katika muda wa miaka miwili iliyopita dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu. Mbali na kuratibu msaada wao kwa majeshi yanayokaribia kuukomboa mji wa Mosul , mawaziri hao walijadili pia hali ya kampeni kama hiyo upande wa Syria na kusema wanatayarisha mpango kwa ajili ya kuutenga mji wa Raqa.
Ufaransa ina nia ya kutaka kuutenga mji wa Raqa , ambako wapiganaji wa IS wapatao 3,000 hadi 4,000 ikiwa ni pamoja na jumla ya raia karibu 300 wa Ufaransa ambao kurejea kwao nchini Ufaransa wakati Dola la Kiislamu litakapoporomoka ni hali inayofikiriwa kuwa kitisho kikubwa cha kitaifa.
Wakati mawaziri hao wakikutana, rais wa Ufaransa Francois Hollande ameonya kwamba , kukombolewa kwa mji wa Mosul sio mwisho wa mapambano dhidi ya kundi hilo.
"Kile kilichopo sasa ni hali ya baadaye ya kisiasa ya mji huo, jimbo hilo na Iraq, na nchi zilizomo katika muungano pia zinapaswa kusaidia katika utekelezaji katika kuiongoza serikali ambayo itajumuisha makundi yote katika mji wa Mosul. Makabila yote pamoja na makundi ya kidini yatawakilishwa. Na amani iliyotarajiwa itakuwapo."
IS yaendelea kupambana
Likitaka kuondoa mtazamo kutoka kampeni ya mapambano dhidi ya mji wa Mosul , kundi la IS lilifanya mashambulio katika mji wa kaskazini wa Kirkuk na mji wa magharibi wa Rutba katika siku za hivi karibuni.
Wapiganaji hao wa Jihadi walikamata vitongoji viwili katika mji wa Rutba , lakini maafisa wamesema kwamba tangu jana Jumanne vitongoji hivyo vimerejeshwa katika udhibiti wa majeshi ya serikali.
Maafisa waandamizi wa Marekani na Iraq wameripoti kwamba viongozi wa IS tayari wanajaribu kuondoka kutoka Mosul na kwenda katika mamlaka ya kikhalifa upande wa Syria.
Lakini afisa ambaye yuko karibu an waziri wa ulinzi wa Ufaransa Le Drian amesema wapiganaji mia chache wa kundi la IS hivi karibuni walihamia katika eneo la maigano, wakiimarisha nguvu ya wenzao wapatao 3,000 hadi 5,000 wanaopambana kuulinda mji wa Mosul. Kundi la IS limeonesha uwezo mkubwa wa mapambano , na pia kurejea nyuma wakati wakishambuliwa kwa nguvu.
Lakini madai yao ya kutaka kuunda mamlaka ya Kikhalifa yakikosa uhalali kila wakati wanapopoteza eneo, IS imekuwa ikileta upinzani mkubwa katika mapambano katika mji wa Mosul.
Mji huo ndipo alipo kiongozi mkuu wa IS Abu bakr al-Baghdadi aliyetangaza mamlaka ya Ukhalifa katika ardhi iliyotekwa kati ya Syria na Iraq mwezi Juni , 2014 na kukombolewa kwa mji huo kutasababisha mwisho wa kundi hilo kudhibiti ardhi katika upande wa Iraq.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Iddi Ssessenga