1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa ulinzi wa NATO wakutana

Saumu Mwasimba
15 Februari 2017

Kwa mara ya kwanza waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis kukutana na wenzake wa NATO katika mkutano muhimu mjini Brussels

https://p.dw.com/p/2XbRl
Brüssel Nato-Hauptquartier
Picha: picture-alliance/dpa/J. Warnand

Katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO amesema muungano huo wa kijeshi utaingiwa na mashaka ikiwa itathibitika kuwa kweli ripoti zinazosema kwamba Urusi imekiuka mkataba wa enzi za vita baridi kwa kuziweka tayari  meli zake za makombora. Mashirika ya kijaasusi ya Marekani yametoa tathmini kwamba makombora ya Urusi yamekuwa yakifanya kazi tangu mwaka jana na kuna uwezekano mkataba wa mwaka 1987 wa kuzuia makombora ya kuingilia kati ya Nuklia ya masafa marefu umekiukwa.

Jens Stoltenberg amesema hatua ya kuzingatia makubaliano ya kudhibiti silaha ni muhimu sana na hasa linapokuja suala linalohusu mikataba inayosimamia silaha za Kinyuklia.Ikiwa Urusi haifuati mkataba huo litakuwa ni suala linalozusha wasiwasi mkubwa kwa muungano huo amesema Stoltenberg.Kauli ya katibu mkuu huyo wa NATO mjini Brussels imekuja kabla ya kuongoza mkutano wa kwanza wa mawaziri wa ulinzi wa jumuiya hiyo na waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis.

Belgien NATO US Sicherheit Jim Mattis und Michael Fallon
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Jim Mattis akiwa na mwenzake wa Uingereza Michael FallonPicha: picture alliance/AP Photo/V. Mayo

Stolttenberg amebaini ikwamba washirika wote wa NATO wataonesha mshikamano katika mazungumzo hayo ya kwanza na waziri huyo wa ulinzi wa Marekani James Mattis hii leo licha ya kwamba wasiwasi umeendelea kuwepo juu ya msimamo wa rais Donald Trump kuhusu Jumuiya hiyo.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Mattis ameshasema kwamba anaiunga mkono NATO kinyume kabisa na mashaka yaliyooneshwa na kiongozi wake Trump na amekuwa na msimamo thabiti kuhusu Urusi kuliko ilivyo kwa rais huyo ambaye mtazamo wake unawatia mashaka makubwa washirika wa NATO wa nchi za Ulaya Mashariki na hasa zilizo wanachama  wa jumuiya hiyo.

Federica Mogherini und Jens Stoltenberg
Picha: Reuters/F. Lenoir

Stolltenberg akizungumza na waandishi habari  wakati akiwasili kuhudhuria mkutano huo wa siku mbili mjini Brussels alisema watakachokisisitiza katika mkutano huo ni umuhimu wa kusimama pamoja na kulindana  na pia kutaka kupata hakikisho la kujitolewa kwa dhati Marekani katika Umoja huo wa kijeshi.Kauli hiyo ya Stolltenberg ameitowa baada ya kuulizwa ikiwa anahisi kujiuzulu kwa mshauri wa mambo ya usalama wa ndani wa ikulu ya White House kutokana na hatua yake ya kuwasiliana na Urusi ni dalili inayooenesha mkorogano  uliopo katika utawala wa Trump.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Mattis wakati akiwa katika ndege kuelekea Brusels alisema kwamba kuondoka kwa Flynn hakutosababisha athari yoyote katika ujumbe wa Marekani kwa NATO.Lakini pamoja na ujumbe wa kuwepo mshikamano Mattis amejiandaa kuzitia msukumo nchi nyingine 28 wanachama wa  mfungamano huo wa kijeshi  kutimiza wajibu wao wa kuongeza bajeti ya matumizi ya kijeshi licha ya nchi nyingi za Ulaya kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.Kwa upande mwingine lakini inaonesha kwamba hata Stoltenberg binafsi ameshasalimu amri katika shinikizo hilo la Marekani ambapo kabla ya mkutano huu wa leo alisikika kusema kwamba kuimarisha bajeti ya ulinzi ni suala muhimu linalopewa kipaumbele.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman