1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Ujerumani wamekamilisha ziara Tanzania na kuelekea Afrika Kusini

9 Aprili 2010

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, ametoa mwito kwa nchi za Afrika Mashariki zisimame kidete katika kupambana na uharamia katika pwani zao.

https://p.dw.com/p/MrSt
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle  ametoa mwito kwa  nchi  za Afrika Mashariki zisimame  kidete katika kupambana na uharamia katika pwani zao.

Waziri Westerwelle amesema hayo nchini Tanzania , kituo cha kwanza  cha ziara yake ya siku tano barani Afrika.

Katika ziara yake, waziri  wa mambo ya nje Guido Westerwelle  anaongozana  na waziri wa misaada ya maendeleo, Dirk Niebel.Hii ni ziara ya kwanza ya pamoja  ya  mawaziri hao barani Afrika.

Baada ya kuitembelea  Tanzania leo watakuwa Afrika Kusini. Watamaliza ziara yao ya siku  tano barani Afrika  kwa kuitembelea Djibouti kwenye pembe ya Afrika.

Lengo la kutekeleza sera  ya ufanisi  zaidi ya mambo ya nje kwa  makubaliano baina  ya wizara hizo mbili limewekwa katika mkataba wa serikali ya mseto ya Ujerumani. Lengo hilo ni muhimu hasa kuhusu nchi zinazoendelea na  zinazokabiliwa na migogoro  ambapo wahisani na wadau  wengine wanatekeleza ajenda   tofauti.

Barani Afrika pana nchi  nyingi kama hizo- vyombo vya habari kwa sasa vinaripoti sana hasa juu ya Somalia, nchi  inayozingatiwa katika sera za nje za nchi za Ulaya na za Afrika kadhalika. Suala la Somalia  pia limejadiliwa kwenye mazungumzo baina  ya waziri Westerwelle na viongozi wa Tanzania.

Matukio ya  sasa yanaonyesha jambo moja wazi:  umaskini,migogoro katika  ugavi wa raslimali,na  maendeleo duni ni sababu zinazoweza kuchangia katika  kuleta vurumai katika eneo   zima.Uharamia unaotendeka kwenye pembe ya Afrika na  Ghuba ya Aden ni miongoni  mwa mifano.

Maharamia  wanaziteka nyara meli ili kudai vitita vya fedha wanazotumia  kwa  ajili  ya kugharimia  vita vya nchini  Somalia.

Mawaziri wa Ujerumani  na wa Tanzania wameeleza wasiwasi wao juu ya mgogoro wa Somalia.

Waziri wa mambo ya nje wa  Tanzania, Bernard  Membe,  amesema,

"Mizizi ya mgogoro wa Somalia  hasa ni  ya kiuchumi.Na  tunatoa mwito  kwa jumuiya  ya kimataifa ihusiane  na  Somalia kama inavyohusiana   na nchi nyingine  ambamo migogoro inazuka. Nchi hizo zinahitaji usalama na mashirika yanayochangia  katika kuleta mageuzi.Lakini   asasi  hizo zifanye kazi nchini  Somalia, usalama utahitajika. Na hiyo ndiyo  sababu  tunatoa mwito  kwa  nchi zilizoahidi  kuchangia   askari zipeleke askari hao  nchini Somalia. Nchi  hizo  ni  pamoja na Nigeria, Ghana, Malawi na Senegal"

Kwa upande wake, Tanzania ipo tayari kutoa mafunzo kwa polisi wa  Somalia kwa msaada wa  Ujerumani.

Mawaziri  wa Tanzania  na wa Ujerumani pia wamejadili  suala la uharamia.

Waziri Westerwelle amesema  harakati  za kupambana na  uharamia ni jambo la manufaa  kwa wote.

"Ni kwa maslahi ya  nchi  zetu kuendesha harakati  dhidi  ya  uharamia.  Kwani sote tunategemea  kuwepo kwa   biashara huru duniani inayoleta  manufaa  kwa  kila upande"

Katika ziara yao ya siku tano  barani Afrika mawaziri wa Ujerumani wa mambo ya nje, Guido Westerwelle, na wa ushirikiano  wa maendeleo,  Dirk Niebel,  leo wameanza ziara nchini Afrika Kusini.

Mwandishi:Ute Schaeffer/Mtullya, Abdu

Mpitiaji: Miraji Othman