1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Ujerumani kujadli kuuzwa kwa kampuni ya Opel

4 Mei 2009

Mawaziri wa uchumi na Mambo ya Nje wa Ujerumani, leo hii wanakutana na mkurugenzi mtendaji wa kundi la makampuni la Fiat la Italia kujadiliana juu ya mpango wa kampuni hiyo kuinunua kampuni ya tanzu ya Opel

https://p.dw.com/p/HjKb
Waziri wa Uchumi wa Ujerumani zu GuttenbergPicha: dpa/picture-alliance

Kampuni hiyo ya Fiat imesema kuwa inataka kuinunua kampuni ya Opel na kuiunganisha na kimarekani ya Chrysler, katika mipango yake ya kuunda kampuni mpya.


Katika taarifa yake iliyoitoa jana siku moja kabla ya mkutano huo wa leo huko mjini Berlin, kampuni ya Fiat imesema kuwa inataka kununua makampuni tanzu ya General Motors yaliyoko barani Ulaya na kuanzisha kampuni kubwa kabisa duniani la kutengeneza magari madogo na malori.


Fiat imesema kuwa kampuni hiyo mpya itakuwa na uwezo wa kuingiza mapato ya kiasi cha euro billioni 80 kutokana na mauzo ya magari zaidi ya milioni sita kwa mwaka.


Kampuni mama ya General Motors mbali ya kuwa na kampuni ya Opel ya Ujerumani pia ina miliki kampuni ya Vauxhall iliyoko Uingereza na nyingine ya magari ya Saab iliyoko Sweden.


Akizungumzia juu ya mipango ya kutaka kuinunua kampuni ya Opel, Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Karl-Theodor zu Guttenberg, amesema serikali ya Ujerumani iko tayari kujadiliana na Fiat.

´´Serikali ya shirikisho kwa mara nyingine iko tayari kwa majadiliano juu ya mtizamo huo.Muhimu kuwa makampuni hayo yamekubaliana, kwani serikali ya shirikisho haina hisa´´.

Waziri huyo wa Uchumi wa Ujerumani pia alisema kuwa kile ambacho serikali yake inashughulikia ni kuona ajira za kampuni hiyo ya Opel hazipotei.


Ameunga mkono mipango ya kampuni hiyo ya Fiat pindi itakapoinua Opel kuhakikisha kuwa viwanda vyote vya kampuni hiyo ya Opel vilivyopo Ujerumani vinafanyakazi.


Hata hivyo wakosoaji kwa mfano wanaona hasara itakayotokea kutokana na makampuni hayo mawili yanayotengeneza bidhaa ya aina moja yaani magari kushindana katika soko.


Pia wafanyakazi wa kampuni ya Opel wamebakia na wasi wasi juu ya majaaliwa yao kama anavyothibitisha Mkuu wa ufundi katika kiwanda cha Opel mjini Bochum Rainer Einenkel ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya usimamizi ya kiwanda hicho.

´´Tutakuwa na matatizo makubwa kama tutajiunga na Fiat.Tunajua kuwa ni kampuni inayotengeneza magari mazuri.Tunataka vile vile tuwe na majaaliwa mazuri na tuna wasi wasi, kama kwa kujiunga na Fiat tutafanikiwa kwa sababu mpaka sasa hatujapokea fikra yoyote kuhusiana na hatua hiyo´´.

Fiat Opel Fusion
Picha: dpa/picture-alliance

Wakati ambapo Kiongozi wa kampuni hiyo ya Fiat akijianda na mazungumzo na mawaziri wa Ujerumani huko Berlin hii, leo, kampuni nyingine ya kutengeneza magari ya Magna yenye viwanda nchini Canada na Austria imeunganisha nguvu na kampuni ya kutengeneza magari ya Kirusi pamoja na benki ya Urusi Sberbank kutaka kuinunua kampuni ya Opel.


Kampuni ya Opel, General Motor ya Marekani imekumbwa na hali ya fedha pamoja na kupigwa jeki na utawala wa Rais Obama lakini hali bado inaonekana kuwa ngumu.

Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri:Josephat Charo