1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa nje wa Ujerumani na Marekani Moscow

15 Mei 2007

Mawaziri wa nje wa Marekani dr.Rice na wa Ujerumani Steinmier wana ajenda tofauti leo huko Moscow.Wazi ni kuwa kunay mvutano kati ya kambi ya magharibi na Russia.

https://p.dw.com/p/CB48

Mawaziri wa nje wa Marekani Dr.Condoleezza Rice na wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, wana mazungumzo leo na rais Wladmir Putin wa Russia, mjini Moscow kila mmoja akiwa na ajenda yake.Wakati bibi Condoleeza Rice aliwasili Moscow jana ,Bw.Steinmier, anaondoka leo Berlin kuelekea Moscow kwa niaba ya Umoja wa Ulaya,Ujerumani ikiwa wakati huu mwenyekiti wake.

Mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Russia uliopangwa kufanyika ijumaa hii katika mji wa Samara umo mashakani.Umegubikwa na hitilafu nyingi kuanzia marufuku ilioweka Russia juu ya bidhaa za nyama kutoka Poland,mwanachama wa UU hadi mabishano na Estonia kwa uamuzi wake wa kuling’oa sanamu la ukumbusho wa vita vya pili vya dunia kutoka shina la mji mkuu wake Tallin.

Bw.Steinmier aliungama jana kwamba, Russia na UU haziyumkiniki kuafikiana katika mkutano huo wa kilele wa ijumaa hii kuanza majadiliano juu ya ushirikiano mkubwa kati yao katika sekta mbali mbali kama biashara,nishati,haki za binadamu na sera za nje.

Sadfa ya kufanyika ziara hizi mbili wakati mmoja-ile ya Dr.Rice nah ii ya Steinmier mjini Moscow yabainisha wasi wasi ilionao kambi ya magharibi kwa Russia katika kipindi ambacho rais Putin amechukua msimamo mkali zaidi mbele ya Marekani na hata Umoja wa Ulaya.

Russia ikiwa ina neema wakati huu wa fedha kutoka mafuta yake ya petroli n a ikianza kujitutumua upya kama dola kuu wakati ambapo Marekani imenasa katika matope nchini Irak,imearifu haitaamrishwa la kufanya na waziri huyo wa nje wa Marekani anaekutana leo kwa mazungumzo na rais Putin-mada kuu ikiwa mpango wa Marekani wa kuegesha makombora Ulaya ya kati .

Hii inaonekana na Moscow ni kufufua vita baridi ikihisi azma hasa ya makombora hayo kuegeshwa nchini Poland na Jamhuri ya Czech, ni dhidi yake.

Mada nyengine ambayo Marekani inazungumza na Russia ni mpango wa UM unaoungwamkono na Marekani kuipa uhuru Kosovo baada ya miaka 8 jimbo hilo la Yugoslavia ya zamani linalodaiwa na Serbia kutawaliwa na UM.Swali la hatima ya Kosovo litazungumziwa pia na Bw.Steinmier kama mweenyekiti wa sasaa wa Baraza la mawaziri la UU.

Mkutano wa kilele wa ijumaa hii, ulikuwa uwe kilele cha uwenyekiti wa Ujerumani wa UU.Ishara njema pekee ilioibuka, ni mualiko alioutoa waziri wa nje wa Russia, Lavrov kwa Bw.Steinmeier aende Moscow kwa mashauriano.Lakini, baada ya mashauriano aliokuwa nayo mjini Brussels, makao makuu ya UU ,Bw. Steinmier ameonesha shaka shaka iwapo mkutano huo wa kilele utafanyika kabisa na ukifanyika iwapo utaleta maafikiano yoyote muhimu kuhusu ushirikiano baina ya Russia na UU.Bw.Steinmeier:

“Maandalio ya mkutano huo kwa jicho la tofauti nyingi zilizoibuka si rahisi.Kwa sababu kinyume na matarajio yangu, hatutafika mbali kukubaliana mkutano huo ufanyike juu ya kuunda ushirika na mapatano ya ushirikiano.”

Mzozo juu ya nyama ya Poland iliopigwa marufuku kuingia Russia unaangaliwa na duru ya Tume ya Ulaya kuwa ndio shina la balaa hili lote.Poland imewekewa marufuku kuuza nyama yake Russia tangu mwishoni mwa 2005 .Kwa kadiri marufuku hayo hayakondolewa,Poland haiku tayari kushiriki katika mazungumzo ya UU kuwa na ushirika na Russia.

Bw.Steinmeier tena:

“”Hadi utakapofanyika mkutano huo wa kilele tutajitahidi kuleta ufumbuzi juu ya mgogoro wa nyama ya Poland,sitaweza lakini kuwaahidi kwamba tutautatua mzozo huu.”