1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier: Jibu liko mikononi mwa Ukraine na Urusi

24 Juni 2015

Mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Ukraine wameelezea wasiwasi kuhusu hali ya usalama Mashariki mwa Ukraine na kutoa wito wa kusitishwa mapigano kuruhusu mchakato wa kisiasa kusonga mbele.

https://p.dw.com/p/1FmWt
Mawaziri wakizungumzia mzozo wa Ukraine mjini Paris
Mawaziri wakizungumzia mzozo wa Ukraine mjini ParisPicha: Getty Images/AFP/P. Kovarik

Mawaziri hao wamekutana katika juhudi za kujaribu kuyaokoa makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Ukraine, ambayo yalitiwa saini mjini Minsk-Belarus mwezi Februari. Akizungumza kwa niaba ya wenzake, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema wametaka mapigano yasitishwe mara moja katika eneo la Donbas, akimaanisha ukanda wa mashariki mwa Ukraine unaokabiliwa na vita.

Mwenzake wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier amesema anayo matumaini kwamba mapigano yatasitishwa katika mji wa Shyrokyne ulio umbali wa kilomita 23 mashariki mwa mji muhimu wa Mariupol katika jimbo la Donetsk.

Steimeier amesema, ''Ninayo matumaini kwamba usiku wa leo tumepiga hatua mbele, lakini tutategemea utashi wa Ukraine na Urusi kuweza kushirikiana. Si Ufaransa wala Ujerumani zenye uwezo wa kuutanzua mzozo huo, bali pande zinazohusika zinatakiwa kuheshimu makubaliano ya mjini Minsk.''

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Frank-Walter SteinmeierPicha: Reuters/Valentyn Ogirenko

Suluhisho mikononi mwa Urusi na Ukraine

Waziri Steinmeier ameendelea kusema kuwa suluhisho haliwezi kutokana na juhudi za kisiasa pekee, na kuongeza kuwa wanahitaji utaalamu wa kijeshi wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, OSCE, kuweza kupata mpango mzima wa namna mkataba wa Minsk ulivyokiukwa na vikosi vya serikali ya Ukraine pamoja na waasi wa mashariki wanaoegemea upande wa Urusi.

Mawaziri hao wamekutana mara kadhaa mnamo miezi michache iliyopita, kukiwa na shutuma za kukiukwa ma makubaliano ya kusitisha vita yaliyotiwa saini mjini Minsk. Mazungumzo yao bado hayajaweza kuleta tija, katika kushinikiza makubaliano hayo yatekelezwe kikamilifu.

Marekani kupeleka silaha nzito Ulaya Mashariki

Kuhusiana na mvutano kati ya Urusi na nchi za Magharibi uliosababishwa na mzozo huo wa Ukraine, Marekani imesema itaanza kupeleka silaha nzito nzito katika mataifa matatu ya Ulaya Mashariki, ambazo ni wanachama wapya wa Umoja wa Kujihami wa NATO.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Ashton Carter ameyatangaza hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na mawaziri wenzake wa ulinzi wa nchi hizo za eneo la Baltic. Carter amesema silaha hizo zitajumuisha vifaru, magari ya kivita pamoja na mizinga, na kuthibitisha kuwa Estonia, Lithuania, Latvia, Bulgaria, Romania na Poland zimekubali kuvipokea vikosi vitakavyozisindikiza silaha hizo.

Lettland, Übergabe von US-Militärtechnik
Vifaru aina ya Abrams ambavyo ni miongoni mwa silaha ambazo Marekani itazipeleka Mashariki mwa UlayaPicha: Reuters/I. Kalnins

''Ingawa hatutaki vita baridi vipya na Urusi, sembuse vile vya moto na nchi hiyo, tutasimama kidete kuwalinda washirika wetu'' amesema waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter.

Mkutano huo kati ya Carter na wenzake wa nchi za Baltic, umefanyika kwenye mkutano wa NATO wa ngazi ya mawaziri, ambao unafanyika leo katika mji mkuu wa Estonia, Tallinn.

Wachambuzi wanasema hatua hiyo ya Marekani, inatuma ujumbe kwa washirika wake pamoja na Urusi, kwamba bado nchi hiyo ni taifa kubwa, ambalo linao uwezo kijeshi kukabiliana na kitisho cha Urusi Mashariki mwa Ulaya.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/dpae

Mhariri: Iddi Ssessanga