1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauwaji ya Winnenden

Oumilkher Hamidou23 Machi 2009

Kilio cha familia za wahanga kwa wanasiasa na jamii kwa jumla

https://p.dw.com/p/HHh6
Mishumaa na mauwa kuwakumbuka wahanga wa mauwaji katika shule ya sekondari ya WinnendenPicha: AP



Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha zaidi na  mjadala kuhusu kampuni la magari la Opel na jinsi unavyoitikisa serikali kuu ya muungano mjini Berlin. Na bila ya shaka msiba wa Winnende ambako ibada ya kuwakumbuka wahanga wa mauwaji katika shule moja ya sekondari ya mji huo mdogo wa kusini mwa Ujerumani ilifanyika mwishoni mwa wiki hii.


Tuanzie Winnenden ambako gazeti la GENERAL-ANZEIGER linaandika.


"Kila wakati ambapo ripoti kuhusu yule kijana aliyecharuka na kuuwa katika shule ya sekondari ya Winnenden zinapozidi kujulikana ndipo napo watu wanapozidi kuamini kwamba kweli hatua zilihitajika.Kwasababu hiyo hiyo,ndio maana,wakuu wa kanisa,kansela Angela Merkel na rais wa shirikisho Horst Köhler wameonya katika hotuba zao watu wawe macho,wasipuuze;dalili za mabadiliko mabaya watu wasizidharau,watu wawe tayari kusaidia wanapoona mtu anapohitaji  msaada,badala ya kumpa kisogo:"


Hayo ni maoni ya GENERAL ANZEIGER nalo gazeti la MÜNCHNER MERKUR linazungumzia risala iliyoandikwa na familia za wahanga.Gazeti linaendelea kusema.


"Sote tunabidi tutafakari kwa kina jinsi ya kukabiliana na zana zinazoshawishi matumizi ya nguvu.Kwasababu michezo ya hatari ya mauwaji na matumizi ya nguvu si jambo linaloweza kukubalika katika jamii iliyostaarabika.Na tasnifu hii si ya leo:huo ndio ukweli wa mambo.Kipya hata hivyo ni ule ukweli kwamba,picha za kutoka Winnenden zitasalia milele nyoyoni mwa jamii."


Gazeti la ALLGEMEINE ZEITUNG la mjini  Mainz linaandika:


"Familia za wanafunzi waliouliwa zimetoa onyo bayana kwa kushikilia sheria za kumiliki silaha zizidishwe makali na hatua kali pia zichukuliwe dhidi ya michezo inayochochea mauwaji na matumizi ya nguvu.Kilio chao kimepindukia mwito wa maadili,ni shinikizo kwa wote wale wanaowajibika kisiasa.Jamii pia inapaswa kuwajibika.Wanaonya dhidi ya desturi hatari ya kupuuzwa mambo na kujiambia "aah tokea hapo hakuna kitakachobadilika."


Mustakbal wa kampuni la magari la Opel nao pia umewashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.Gazeti la BADISCHEN NEUESTEN NACHRICHTEN linaandika:


Chama cha SPD kimejibwaga katika uwanja hatari katika mapambano ya kuania kampuni la Opel.Fikra ya kujihusisha moja kwa moja  serikali katika kupigania mustakbal wa kampuni hilo,kama anavyohoji hiivi sasa waziri wa ajira Olaf Scholz,sio tuu ni kizungumkuti kikubwa cha kisiasa bali hata kiuchumi fikra hiyo italeta mashaka.


Muandishi: Hamidou Oummilkheir/DPA


Mhariri:Abdul-Rahman Mohammed