1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Mauaji ya Sheikh Rogo: Alama ya ukatili au sura nyengine ya vita dhidi ya ugaidi?

Vidio iliyotumwa mitandaoni mara tu baada ya kuuawa kwa mhadhiri wa Kiislamu wa Mombasa, Sheikh Aboud Rogo Mohamed, inaelezea shaka ikiwa mauaji haya ni alama ya ukatili au ni sura nyengine ya vita dhidi ya ugaidi.

Sheikh Aboud Rogo Mohammed

Sheikh Aboud Rogo Mohammed

Hali mjini Mombasa ilichelewa kutulia baada ya mauaji ya Sheikh Aboud Rogo, Jumatatu ya tarehe 27 Agosti 2012. Mpaka katikati ya wiki, tayari watu watatu zaidi walikwishapoteza maisha yao, ambao walitajwa kuwa polisi waliokuwa wakijaribu kutuliza ghasia za baada ya kifo cha Sheikh Rogo.

Siku moja baada ya mauaji hayo, shirika la kutetea haki za binaadamu, Human Rights Watch, likatoa taarifa ya kutaka uchunguzi wa haraka ufanyike dhidi ya mauaji ya Sheikh Rogo, pamoja na kulaani mauaji hayo na vurugu za baada ya mauaji.

"Tunataka uchunguzi wa kina juu ya kile ambacho kimemtokea Sheikh Rogo. Tunadhani ni lazima tukio hili lichunguzwe na hatua zichukuliwe." Alisema Ben Rawlence, Afisa wa Utafiti wa Shirika hilo alipozungumza na DW kwa njia ya simu akiwa jijini Nairobi.

Mashaka katika maisha ya Sheikh Rogo

Machafuko mjini Mombasa baada ya mauaji ya Sheikh Aboud Rogo.

Machafuko mjini Mombasa baada ya mauaji ya Sheikh Aboud Rogo.

Lakini kabla ya kuingia kwenye uhusiano wa mauaji haya dhidi ya Sheikh Rogo na uvunjaji wa haki za binaadamu na au sehemu nyengine ya vita dhidi ya ugaidi, hebu turudi nyuma kidogo kwenye siku za mwisho za maisha yake kuelekea mauaji yake.

Sheikh Aboud Rogo alikuwa kwenye orodha ya vikwazo vya Marekani tangu mwezi Julai kwa madai kuwa alikuwa akijihusisha “na vitendo ambavyo ama moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja vinahatarisha amani, usalama au utulivu wa Somalia," hasa hasa kwa kutoa mafunzo na kukusanya fedha kwa ajili ya al-Shabaab.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo pia lilimuwekea vikwazo vya kusafiri na kuzuia mali zake mwezi huo huo wa Julai, likidai kuwa alikuwa ametoa "msaada wa kifedha, vitu, mafao au ufundi kwa al-Shabaab."

Kwa mujibu wa Baraza hilo, Sheikh Rogo alikuwa ndiye "kiongozi mkuu wa kiitikadi" wa kundi la Hijra la Kenya, ambalo pia linajulikana kama Kituo cha Vijana wa Kiislamu, na ambalo Umoja wa Mataifa unalichukulia kuwa mshirika wa karibu wa al-Shabaab kwa Kenya.

Miongoni mwa ushahidi wa Umoja wa Mataifa kwa tuhuma zake dhidi ya Sheikh Rogo, ni mhadhara alioutoa mwezi Aprili katika Msikiti Jamia wa Nyeri, ambapo vidio hii inayopatikana mtandaoni, inaonekana kuhimiza watu kushirikiana na al-Shabaab kwa jina la kuilinda dini ya Kiislamu.

Mahala pamoja kwenye vidio hiyo, Sheikh Rogo anawaita wanajeshi wote wa Kenya waliokwenda kupigana vita dhidi ya al-Shabaab nchini Somalia kuwa ni makafiri, hata kama wamezaliwa na majina ya Kiislamu.

"Hivi ikiwa Omar wa huku (Kenya) anapigana na Omar wa kule (al-Shabaab) na huyu wa al-Shabaab anataka dini ya Mungu isimame, huyu wa Kenya hataki, nani ni kafiri hapo?" Anauliza kwenye mhadhara huo.

Polisi ya Kenya na Sheikh Rogo

Machafuko na mashambulizi mjini Mombasa baada ya mauaji ya Sheikh Aboud Rogo.

Machafuko na mashambulizi mjini Mombasa baada ya mauaji ya Sheikh Aboud Rogo.

Polisi nchini Kenya walimkamata Sheikh Rogo mwezi Januari mwaka huu, kwa tuhuma za kumkuta na silaha kinyume na sheria. Alipelekwa mbele ya mahakama ya Mombasa tarehe 14 Agosti kwa mashitaka ya kupanga mashambulizi katika maeneo ya umma. Aliyakana mashitaka dhidi yake na kuachiwa kwa dhamana hadi tarehe 15 Oktoba, ambapo kesi yake ilikuwa isikilizwe tena. Lakini akauawa takribani wiki tatu kabla ya tarehe hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, Sheikh Rogo alikuwa ameliarifu jeshi la polisi nchini Kenya, mnamo tarehe 24 Julai, kwamba maisha yake yalikuwa hatarini na kwamba alihitaji ulinzi.

Ripoti hiyo aliiwasilisha pia kwenye Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Kenya na pia mahakama ya nchi hiyo. Kwenye taasisi hizo zote, Sheikh Rogo aliripoti kwamba watu waliojidai kuwa polisi walikuwa wamejaribu kumteka nyara yeye na mwenzake, Abubakar Sharif Ahmed.

"Huyu Sheikh Rogo alikuwa amefikishwa mahakamani Mombasa na alikuwa na kesi nyengine Nairobi, lakini alikuwa ameweka taarifa polisi kwamba maisha yake yako hatarini na anahitaji ulinzi. Hata kama alikuwa na kesi ya tuhuma za ugaidi, hakupaswa kuuwa tu mitaani." Anasema Ben Rawlence wa Human Rights Watch.

Kauli ya Serikali ya Kenya

Watu wakiwa wameubeba muili wa Sheikh Aboud Rogo baada ya kuuawa mjini Mombasa.

Watu wakiwa wameubeba muili wa Sheikh Aboud Rogo baada ya kuuawa mjini Mombasa.

Kilichopelekea hasa mauaji haya ya Sheikh Rogo, kitachukuwa muda mrefu kujulikana, lakini tayari mashirika ya haki za binaadamu ya ndani na nje ya Kenya yanaelekeza vidole vyao kwa mamlaka nchini Kenya, kwamba hata kama hazihusiki moja kwa moja, bado zina wajibu wa moja kwa moja wa kuwalinda raia wake, na katika hili kufanya uchunguzi wa kina.

Waziri Mkuu Raila Odinga alilitolea maelezo jambo hilo, akisema kwamba waliofanya mauaji hayo ni maadui wa Kenya ambao wanataka kuiingiza nchi hiyo kwenye mapambano ya kidini.

"Sisi kama serikali hatukubaliani kabisa na mauaji haya ya kinyama dhidi ya Bwana Rogo. Tumemuagiza kamishna wa polisi ahakikishe kuwa wahusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo." Alisema Odinga.

Tayari mwendesha mashitaka mkuu wa Kenya ametangaza kuundwa kwa tume maalum kuchunguza mauaji ya Sheikh Rogo. Lakini kwa watu ambao wameathirika kwa njia moja ama nyengine na kile kinachoitwa vita vya Kenya dhidi ya ugaidi wa kundi la al-Shabaab la Somalia, matumaini yao kwa tume hiyo yako mashakani.

Mmoja wa watu hao ni Al-Amin Kimathi, Mwenyekiti wa Jukwaa la Waislamu la Haki za Binaadamu nchini Kenya, ambaye anasema hana "sababu ya kuiamini serikali", kwani si mara moja wala mbili mauaji kama haya kutokea na wala hakukuwa na hatua zilizochukuliwa.

Je, kuna uhusiano kati ya jeshi la Kenya kuwapo Somalia na mauaji ya Sheikh Rogo?

Aboud Rogo Mohammed katika picha hii ya Julai 2003 akizungumza na wafuasi wake akiwa mahakamani nchini Kenya.

Aboud Rogo Mohammed katika picha hii ya Julai 2003 akizungumza na wafuasi wake akiwa mahakamani nchini Kenya.

Kenya ilipeleka wanajeshi wake nchini Somalia mwaka jana, kwa lengo la kupambana na wanamgambo wa al-Shabaab, ambao Kenya inawatuhumu kwa kufanya mashambulizi ndani ya ardhi yake, ikiwemo pia utekaji nyara wageni na wafanyakazi wa mashirika ya misaada.

Al-Shabaab yenyewe inadaiwa na inajinasibu kuwa na mafungamano makubwa na al-Qaida, mtandao wa kigaidi unaochukuliwa na Marekani na mataifa ya Magharibi kama adui nambari moja.

Inapokuja staili ya mataifa hayo ya Magharibi, hasa Marekani inayojichukulia kuwa kinara wa kupambana na ugaidi duniani, kuwaondosha washukiwa wao kwa staili hii ya mauaji si jambo la kushangaza.

Lakini kwa taifa kama Kenya, Ben Rawlence wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, haoni uhusiano wa moja kwa moja wa sura hizi mbili za kupambana na ugaidi.

"Siwezi kusema kwamba Kenya inafuata mtindo huo wa Marekani. Hata Marekani yenyewe haiwezi kumuua raia wake nchini mwake. Na sisi hatuwezi kujua kuwa ni kweli serikali imehusika, lakini mahakama na sheria za Kenya zipo. Mtuhumiwa anapaswa kupelekwa mahakamani na kuhukumiwa kisheria. Si kuuawa mitaani."

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Shirika la Haki za Binaadamu liliyaita mauaji ya Sheikh Rogo kama ni uhalifu unaohitaji uchunguzi wa haraka na usioegemea upande wowote. Na wakati huo huo, kuwataka polisi kutumia sheria katika kukabiliana na waandamanaji baada ya kifo hicho.

Matukio mengine kabla ya kifo cha Sheikh Rogo

Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga.

Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga.

Mauaji ya Sheikh Rogo yalitanguliwa na matukio kadhaa ya utekaji nyara na mauaji dhidi ya watu waliokuwa wameshitakiwa kwa kutoa mafunzo au tuhuma nyengine kuhusiana na al-Shabaab.

Kwa mujibu wa taarífa ya Jukwaa la Haki za Binaadamu kwa Waislamu, mnamo mwezi Machi mwaka huu, mhadhiri mwengine wa Kiislamu, Samir Khan, aliyekuwa pia akikabiliwa na mashitaka ya kuwa na silaha kinyume na sheria na kutoa mafunzo kwa ajili ya al-Shabaab, na rafiki yake Mohammed Qassim, walitolewa kwenye basi mjini Mombasa na watu waliojitambulisha kama polisi.

Mwili wa Khan ulikuja kugundulika siku kadhaa baadaye katika mbuga ya Tsavo ukiwa umekatwakatwa vibaya huku hatima ya Qassim ikiwa hadi sasa haijuilikani.

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, mwanzoni Polisi ya Kenya ilikuwa imewaambia waandishi wa habari kuwa Khan alikuwa ameshikiliwa na Kikosi Maalum cha Kupambana na Ugaidi, lakini baadaye wakakana kumshikilia.

Mara kadhaa, wakili wa Sheikh Rogo, Mbugua Mureithi, alikuwa amesema mteja wake alilalamikia kufuatwafuatwa na polisi, na hata kumtaja afisa mmoja wa polisi ambaye alimtishia kwamba wao, polisi, wangelitafuta njia ya kumalizana naye. Al-Amin Kimathi, ambaye mwenyewe si mgeni wa kutiwa misukosuko na polisi, anasema kwamba hayo hayashangazi.

"Binafsi nimeshawahi kuambiwa kwamba 'sisi tutawashugulikia watu hawa (watuhumiwa wa ugaidi) kwa njia nyengine, maana tunajua kuwa mahakamani hatuwashindi.'" Anasema Kimathi.

Maswali yasiyo majibu

Wanajeshi wa Kenya nchini Somalia.

Wanajeshi wa Kenya nchini Somalia.

Wakati Wakenya na dunia wakisubiri majibu kwa mauaji dhidi ya Sheikh Aboud Rogo na machafuko yaliyotokea baada ya hapo, majibu ya kutekwa na hatimaye kutoweka kwa watu akina Samir Hashim Khan, Mohamed Bakhit Qassim, Sylvester Opiyo, Jacob Musyoka, Jeremiah Onyango Okumu, Stephen Mwanzia Osaka, Omar Shaib na Salim Abubakar ndani ya kipindi hiki cha mwaka huu mmoja, bado hayajapatikana. Kwa mujibu wa Jukwaa la Haki za Binaadamu la Waislamu nchini Kenya, matukio yote hayo yaliripotiwa kwenye vyombo vya dola.

Lakini je, ni sadfa tu kwamba kwa njia moja ama nyengine, wote hawa walikuwa katika kesi zinazohusishwa na mafungamano na kundi la al-Shabaab? Vipi kuhusu washukiwa wengine wenye kesi mfano wa za akina Sheikh Rogo hivi sasa nchini Kenya?

Mwandishi: Mohammed Khelef/DW Kiswahili
Mhariri: Josephat Charo

Sauti na Vidio Kuhusu Mada