1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji nchini Guinea

29 Septemba 2009

Guinea inaomboleza, Umoja wa Afrika, AU, pamoja na Jumuiya ya Kimataifa wamesikitishwa na kutoa shutuma zao.

https://p.dw.com/p/JtGH
Kapteni Moussa Dadis Camara apingwa kuwania urais uchaguzi ujao.Picha: AP

Watu 87 wanaripotiwa kuuwawa nchini humo baada vikosi vya usalama kuwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakiandamana kumpinga kiongozi wa kijeshi aliyechukuwa madaraka kwa nguvu Desemba mwaka jana.

Yote yalianza pale waandamanaji walipokusanyika katika uwanja mmoja wa michezo, unaojulikana kama Septemba 28, uliopewa jina hilo mwaka wa 58 pale Guinea ilipopata uhuru wake kutoka Ufaransa. Waandamanaji hao walikuwa hapo kuandamana dhidi ya Kapteni Moussa Dadis Camara asithubutu kusimama kuwania urais katika uchaguzi utakaofanyika mwaka ujao.

Utawala wa kijeshi nchini Guinea ulikuwa umeyapiga marufuku maandamano hayo, lakini bado watu walifika wakiwa wamebeba mabango yaliyokuwa na maneno, Dadis chini, na chama tawala pia chini.

Ilipofika alasiri uwanja huo ulikuwa umegeuzwa kuwa uwanja wa mauti. Vikosi vya usalama vinaripotiwa kuingia uwanjani humo kuukabili umati wa watu, na kuanza kufyatua risasi, bila ya kuchagua. Matokeo yake kiasi cha watu 87 wakauwawa.

Camara akizungumza na kituo kimoja cha redio cha Ufaransa, alisema bado anasubiri ripoti rasmi kujua idadi kamili ya watu waliokufa. Kwa uhakika najua kuna vifo vimetokea, lakini bado nasubiri kupewa ripoti rasmi; hata hivyo nimesikitika sana na naomba msamaha, alisema Camara.

Camara alichukuwa madaraka baada ya mapinduzi ya kijeshi, Desemba mwaka jana muda mfupi tu baada ya kifo cha rais Lansana Conte aliyeitawala Guinea kwa muda mrefu.

Lakusikitisha zaidi ni ripoti ambazo zinasema wanajeshi wameanza kuondoa maiti za watu katika uwanja huo ili kuficha maafa hayo. Duru za polisi zinasema wanajeshi waliingia katika uwanja huo wa Septemba 28 na kuanza kuikusanya miili ya waathiriwa.

Kiasi cha maiti 47 zilipelekwa katika kambi moja ya kijeshi, katika mji huo mkuu wa Conakry. Hii ni kulingana na duru hizo za polisi.

Shirika la msalaba mwekundu linasema baada ya kutekeleza mauaji hayo makamanda wa kijeshi waliagiza maiti zote zikusanywe na kupelekwa katika Kambi ya kijeshi inayojulikana kama Alpha Yaya Diallo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameshutumu matumizi hayo ya nguvu, akisema ameshtushwa mno na umwagaji huo wa damu. Ufaransa iliyoitawala Guinea pia ilitoa sauti zake za shutuma. Ufaransa iliutolea wito utawala huo wa kijeshi kusikiliza sauti za raia wake, kwani wana haki ya kuwateua viongozi wanaowataka.

Ban Ki Moon in Jordanien
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ashtushwa na mauaji yaliyotokea Guinea.Picha: picture-alliance/dpa

Marekani, kupitia afisa wake mmoja, ilisema ina wasiwasi kuhusiana na utovu huu wa usalama mjini Conakry. Viongozi wawili pia wa upinzani walikamatwa katika maandamano hayo. Camara alikuwa ameahidi hatogombania urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Januari mwakani, lakini wachambuzi wa mambo wanasema Camara ana nia ya kushiriki katika uchaguzi huo.

Mwandishi: Munira Muhammad/ DPAE

Mhariri:Othman