1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji bado yanaendelea Irak

30 Machi 2007

Takriban watu 400 wameuwawa nchini Irak katika muda wa siku tatu zilizopita kufuatia mashambulio yanayoelemea misingi ya kidini.

https://p.dw.com/p/CHH6

Wapiganaji wenye msimamo mkali wanaendeleza mashambulio licha ya vikosi vya Marekani kujizatiti katika operesheni ya usalama katika mji wa Baghdad.

Mashambulio ya mabomu yanalenga hasa maeneo ya masoko katika sehemu zinazokaliwa na Washia upande wa kaskazini mwa mji wa Baghdad yanakiuka mwito uliotolewa na waziri mkuu wa Irak Nuri al Malik wa kuwepo ushirikiano katika kupambana na ongezeko la umwagikaji damu hali inayotishia kuigawa Irak.

Ijapokuwa maafisa wa Marekani na wa Irak wanadai kuwa machafuko yamepungua katika mji wa Baghdad na pamoja na kuwepo takriban askari 80,000 kwa ajili ya kudhibiti amani katika mji wa Baghdad jana wapiganaji wawili wa kujitoa muhanga walijilipua kwa mabomu katika soko mashuhuri la mkoa wa Al Shaab karibu na mji wa Sadr na kuwauwa watu 82.

Saa moja kabla ya shambulio hilo kulitokea milipuko mingine kwanza bomu lililotegwa ndani ya gari na kisha bomu lililotegwa kando ya barabara katika mji wa Khalis, watu 43 waliuwawa na wengine kadhaa wakajeruhiwa.

Mwanajeshi mmoja wa Marekani ameuwawa kufuatia shambulio la bomu la kutegwa kando ya barabara kusini mwa Baghdad kwa mujibu wa habari za jeshi la Marekani nchini Irak.

Wakati huo huo wanajeshi wa Irak wakisaidiwa na wanajeshi wa Marekani wamegundua mabomu kadhaa yakutegwa kando ya barabara na silaha zingine katika msako uliofanyika wiki mbili zilizopita.

Jeshi la Marekani pia limesema kuwa limemkamata mtuhumiwa kutoka Iran anaeshukiwa kuhusika na uingizaji wa mabomu ya kutegwa barabarani nchini Irak.

Mtuhumiwa huyo amezuiliwa na wanajeshi wa Marekani na wenazo wa Irak katika mji wa Sadr, anaaminika kuhusiana na mtandao wa makundi yenye msimamo mkali yanayo endeleza mashambulio dhidi ya majeshi ya Irak na yale ya Marekani.

Ijapokuwa taarifa hiyo haikutaja majina ya makundi yenyewe lakini hivi karibuni jeshi la Marekani nchini Irak lilinyooshea kidole makundi ya Iran Revolutionary na Qads kuhusika na uingizaji wa silaha kwa ajili ya kuwasaidia wapiganaji wa Kishia nchini Irak.

Wanakijiji wanadai kuwa mtu huyo anaezuiliwa na majeshi ya Marekani na yale ya Irak ni mwanamume mwenye umri wa miaka 58 baba mwenye watoto sita na ambae hana kazi.

Wamesema msako huo ulianza kama saa nane usiku na ulilenga nyumba nne, wakati huo huo wanakijiji hao wamesema pia kuwa askari wa Marekani na wale wa Irak wamechukua fedha, tarakilishi na simu za mikononi kutoka kwenye nyumba hizo.

Hadi sasa wanajeshi 3,245 wa Marekani wameuwawa tangu nchi hiyo ilipoivamia Irak mwaka 2003.