1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya uchaguzi yatia moyo Ufaransa

Oumilkheir Hamidou
24 Aprili 2017

Mada mbili kuu zimehanikiza magazetini Ujerumani hii leo: Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais nchini Ufaransa na mkutano mkuu wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia mjini Cologne.

https://p.dw.com/p/2bn3R
Frankreich Wahl Emmanuel Macron Rede in Paris
Picha: Reuters/F. Tessier

Tunaanzia Ufaransa ambako vyama vikuu vya kisiasa, wahafidhina na wasoshial democrat  vimepigwa kumbo katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais na kuwafungulia njia wagombea wawili ambao misimamo yao ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inatofautiana moja kwa moja. Hata hivyo matokeo ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais yametuliza nyoyo za wafaransa walio wengi na pia viongozi  wengi wa Umoja wa Ulaya linaandika gazeti la "  Badische Neueste Nachrichten":" Ulaya iliyotetemeshwa kwa mara nyengine tena na zoezi la kupiga kura, imeshusha pumzi-balaa lililokuwa likifikiriwa lingetokea, limeepukwa. Ushindi wa Marine Le Pen na Jean-Luc Mélanchon ungezusha zilzala barani Ulaya: Pindi kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia anaeuchukia Umoja wa ulaya na kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kushoto anaeuangalia kwa jicho la wasi wasi umoja huo wangeingia duru ya pili, basi juhudi za miongo za kuujenga kwa dhati umoja wa Ulaya baada ya vita zingekuwa kazi bure. Kwa bahati nzuri ni Emmanuel Macron, mwanasiasa kijana anaetetea umuhimu wa Umoja wa ulaya ndie anaejikuta mstari wa mbele katika duru hiyo ya pili ya uchaguzi inayowarejeshea matumaini na hali ya kujiamini viongozi wa Ulaya. Ushindi wake katika duru ya kwanza ni ushahidi kwamba kujitambulisha na Ulaya kunaweza kumpatia mtu ushindi katika uchaguzi.

Umoja wa Ulaya washusha pumzi

Gazeti la "Westfälische Nachrichten" linatathmini hali ingekuwa ya aina gani pindi Le Pen na Mélanchon wangeingia duru ya pili. Gazeti hilo linaendelea kuandika: "Si haba wafaransa wameuepushia Umoja wa Ulaya balaa la kuwaona Le Pen  na Mélanchon wakiingia duru ya pili. Kwasababu pindi wangeingia wote wawili katika duru ya pili basi matokeo yake yangekuwa kujitoa Ufaransa katika Umoja wa ulaya-Frexit-Balaa kubwa hilo-Ingawa pia ni balaa kumuona mfuasi wa  siasa kali za mrengo wa kulia akilinyemelea kasri la Elysée. Akifanikiwa kuingia itamaanisha mwisho wa urafiki kati ya Ujerumani na Ufaransa. Matumaini makubwa anawekewa Emmanuel Macron aliyemaliza wa  kwanza katika duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi."

AfD yazidi kuelemea kulia

Mkutano mkuu wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, Chaguo Mbadala kwa Ujerumani, AfD umemalizika jana  mjini Cologne. Mwenyekiti mwenza wa chama hicho Frauke Petry ameachwa kando na badala yake kuteuliwa wanasiasa wawili wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia Alice Weidel na Alexander Gauland kuongoza orodha ya majina kuelekea uchaguzi mkuu unaokuja. Kuhusu matokeo ya mkutano huo mkuu linaandika gazeti la "Flensburger Tageblatt": "Kimoja ni dhahir, chama cha AfD kimeamua kufuata siasa kali zaidi za mrengo wa kulia tangu mkutano wao mkuu ulipomalizika mjini Cologne. Hata hivyo hakuna sababu ya watu kuingiwa na hofu, kinyume kabisa. Maamuzi yaliyopitishwa Cologne kuhusu  uongozi na ratiba yatawatisha badala ya kuwavutia wapiga kura. Na pia uamuzi wao wa kutopendelea kushiriki serikalini siku za mbele. Kimoja ni dhahir AfD wataendelea kuwepo lakini hawatoweza kushawishi kwa namna yoyote ile maamuzi humu nchini na wako mbali kabisa na kuifikia ile sifa ya kugeuka chama kikubwa kinachoungwa mkono na wananchi.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlanadspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga