1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya uchaguzi yaahirishwa kutolewa Sudan.

Abdu Said Mtullya20 Aprili 2010

Marekani imesema uchaguzi wa Sudan haukuwa wa haki.Lakini Sudan imekanusha madai hayo.

https://p.dw.com/p/N1Sp
Matokeo ya uchaguzi wa Sudan yatachelewa kutolewa.Picha: AP

Chama tawala nchini Sudan National Congress Party kimepinga madai yaliyotolewa na Marekani kwamba uchaguzi wa rais uliofanyika nchini humo wiki jana haukuwa huru wala wa haki.

Hatahivyo msemaji wa chama hicho ameeleza kuwa Sudan ipo tayari kushirikiana na Marekani.

Baada ya Umoja wa Ulaya,Marekani sasa pia imesema kuwa uchaguzi wa bunge na wa rais uliofanyika wiki jana nchini Sudan haukuwa huru wala wa haki.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Philip Crowley ameeleza kuwa uchaguzi huo haukutimiza viwango vya kimataifa. Ameeleza kwamba kwa muda mrefu Marekani ilikuwa na wasiwasi juu ya mazingira ambapo uchaguzi ulifanyika.

Hapo awali wajumbe wa Umoja wa Ulaya waliokuwa wanausimamia uchaguzi huo pia walisema palikuwa na mapungufu. Wamesema hasa kusini mwa Sudan kasoro zilijitokeza.

Lakini msemaji wa chama kinachotawala,nchini Sudan National Congress Party bwana Ibrahim Ghandoor amekanusha madai hayo.Amesema kigezo muhimu katika kutimiza viwango vya kimataifa ni kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanyika kwa haki na katika mazingira huru na Sudan imetekeleza kigezo hicho. Msemaji huyo pia ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Sudan ipo tayari kushirikiana na Marekani .

Watu wa Sudan walipiga kura kuanzia tarehe 11 hadi 15 ili kuwachagua wabunge na rais.

Uchaguzi huo ni wa kwanza kufanyika baada ya miaka 24 ambapo wajumbe wa vyama vingi walishiriki.Hata hivyo baadhi ya wajumbe wa vyama muhimu waliususia uchaguzi huo.Washindani muhimu, Sadiq al Mahdi kutoka chama cha Umma Party na Yasser Arman wa chama cha Sudan Peoples Liberation Movement,SPLM walijitoa hata kabla ya kuanza kufanyika kwa uchaguzi.

Uchaguzi huo pia ulikabiliwa na kasoro katika kukimu mahitaji kadhaa. Vituo vya kupigia kura vilichelewa kufunguliwa ; majina ya wastahiki yalikosewa tahijia na mengine hayakuorodhoreshwa kabisa.

Katika matukio mengine, visanduku vya kupigia kura vilipelekwa kwenye vituo ambavyo havikuwa sahihi.

Hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Philip Crowley ameeleza kuwa Marekani inatambua umuhimu wa uchaguzi huo katika utekelezaji wa makubaliano ya amani-CPA yaliyomaliza vita vya miaka mingi baina ya Sudan ya kaskazini na ya kusini.

Lakini China,mshirika mkubwa wa Sudan imesema uchaguzi ulifanyika katika mazingira ya amani.

Wakati huo huo habari kutoka mji mkuu wa Sudan Khartoum zinasema kuwa tume ya kitaifa ya uchaguzi itachelewesha kutangazwa matokeo ya uchaguzi kwa muda usiojulikana.

Matokeo hayo yalitarajiwa kutolewa leo. Mkuu wa tume hiyo bwana Hadi Mohammed Ahmed amesema tume yake haiwezi kutaja siku ya uhakika kwa sababu zeozi la kuhesabu kura ni gumu sana.

Lakini hesabu za hadi sasa zinaashiria ushindi mkubwa kwa chama cha rais Omar al Bashir-National Congress Party-NCP

Mwandishi Mtullya Abdu/DAAE/AFPE/

Mhariri/Abdul-Rahman.