1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya uchaguzi Senegal yachapishwa

Admin.WagnerD1 Machi 2012

Matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumapili nchini Senegal yametangazwa, na hakuna mgombea aliyeweza kupata asilimia 50 inayohitajika kuepusha duru ya pili. Rais Wade anapewa nafasi finyu kushinda duru hiyo.

https://p.dw.com/p/14CL5
Macky Sall, atakayetoana jasho na Abdoulaye Wade katika duru ya pili
Macky Sall, atakayetoana jasho na Abdoulaye Wade katika duru ya piliPicha: dapd

Kwa mujibu wa matokeo hayo ambayo yalitangazwa jana usiku, Rais Abdoulaye Wade anaongoza akiwa na asilimia 34.82 ya kura, ushindi ambao haukaribii kiwango cha asilimia 50 ambacho angehitaji ili kupata ushindi wa moja kwa moja. Anayekuja katika nafasi ya pili ni waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Macky Sall, ambaye amepata asilimia 26.57. Moustapha Niasse ambaye aliwahi pia kuwa waziri mkuu, yuko katika nafasi ya tatu na asilimia 13.2, naye Idrissa Seck ni wa nne akijikusanyia asilimia 7.86 ya kura zilizopigwa.

Hii ina maana kuwa duru ya pili ya uchaguzi itawashirikisha Abdoulaye Wade na Macky Sall. Wachambuzi wanasema nafasi ya Wade kushinda uchaguzi huu ilikuwa kubwa katika duru ya kwanza ambamo upinzani ulikuwa umegawanyika, kuliko kwenye duru inayofuata ambayo inaweza kuunganisha upinzani nyuma ya mtu wanayeshindana.

Rais Abdoulaye Wade anakabiliwa na kibarua kigumu katika duru inayofuata
Rais Abdoulaye Wade anakabiliwa na kibarua kigumu katika duru inayofuataPicha: dapd

Wade akabiliwa na changamoto kubwa

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Senegal, Babacar Ngeye, anasema vuguvugu lijulikanalo kama M23 ambalo liliundwa kupinga hatua ya Abdoulaye Wade kugombea mhula wa tatu, linaweza kumsaidia Macky Sall kupata ushindi dhidi ya Wade katika duru inayofuatia.

''Yuko katika nafasi nzuri kuliko katika duru ya kwanza. Hebu chukua mfano wa uchaguzi wa mwaka 2000, ambapo Wade hakuwa hata na asilimia 30, huku rais wa wakati huo Abdou Diouf akiwa na zaidi ya asilimia 40. Katika duru ya pili Wade alipata zaidi ya asilimia 56. Tuko katika hali sawa na ile, na Wade yuko hata katika nafasi mbaya zaidi kuliko ya Diouf wakati ule.'' Alisema Ngeye.

Kumomonyoka kwa ushawishi wa Abdoulaye Wade kulidhihirika siku ya uchaguzi alipozomewa na umati wa watu badala ya kushangiliwa kama ilivyokuwa kawaida. Utata juu ya hatua yake ya kukaidi katiba na kugombea muhula wa tatu ulikuwa suala muhimu kuliko mambo mengine yanayohusiana na sera za wagombea.

Kwa muda mrefu Senegal imeng'aa kama mfano wa demokrasia Afrika
Kwa muda mrefu Senegal imeng'aa kama mfano wa demokrasia AfrikaPicha: Reuters

Wade aliingia madarakani mwaka 2000 akiwa na ahadi chungu nzima za mageuzi ya kidemokrasia. Kwanza alipunguza muda wa muhula wa Urais kutoka miaka saba hadi mitano, baadaye mwaka 2008, akabadilisha mawazo na kufanya mabadiliko mengine yaliyoufanya tena muhula huo kuwa miaka saba. Aliirekebisha katiba mara 15, jambo ambalo liliwafanya wakosoaji kumtuhumu kuichukulia nchi na sheria zake kama mali yake binafsi.

Ahadi ya kuheshimu mageuzi

Macky Sall ameahidi kuwa iwapo atachaguliwa kuwa rais ataurejesha muhula wa urais kuwa wa miaka mitano, na kuweka kikomo cha mihula miwili tu.

'' Ninawaahidi wananchi wa Senegal kuwa nitaiheshimu ahadi hii. Rais sio mfalme, ni mtu ambaye kwa kipindi fulani anapewa dhamana ya kuiongoza nchi,'' alisema Macky Sall.

Maafisa wa Wade wameacha lugha ya kujitapa ambayo ilikuwa kawaida wakati wa kampeni. Mpwa wake ambaye ni mbunge amesema huu si wakati wa kuzungumzia ushindi wa kishindo bali ni wa kuwaendea wapiga kura kwa unyenyekevu, kwa vile hatimaye, ndio wenye kauli ya mwisho.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AP

Mhariri:Josephat Charo