1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya uchaguzi kutangazwa kesho Afghanistan

Oumilkher Hamidou24 Agosti 2009

Waafghanistan wasubiri kwa hamu matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais

https://p.dw.com/p/JHQ5
Tume ya wasimamizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa UlayaPicha: DW

Patashika zimehanikiza nchini Afghanistan siku moja kabla ya matokeo ya mwanzo ya uchaguzi wa rais kutangazwa,huku watetezi wawili wakuu,rais anaemaliza wadhifa wake Hamid Karzai na mpinzani wake mkuu Abdullah Abdullah,kila mmoja akidai kuongoza matokeo ya uchaguzi huo.

Kamisheni ya uchaguzi ya Afghanistan imesema matokeo ya mwanzo ya uchaguzi wa rais ulioitishwa alkhamisi iliyopita yatatangazwa kesho jumanne.

Kambi zote mbili,ile ya Hamid Karzai na ya waziri wake wa zamani wa mambo ya nchi za nje Abdullah Abdullah,zimekua zikidai,kila moja inaongoza matokeo ya uchaguzi huo, wa pili katika historia ya Afghanistan-kwa hoja wamepokea ripoti za kuaminika kutoka kwa wachunguzi wao vituoni.

Tangu wakati huo patashika zimezagaa:Abdullah Abdullah ameituhumu kambi ya Karzai kufanya udanganyifu uliokithiri huku rais Karzai akififiisha na kutoa mwito wa kuwepo amani na umoja:

"Msipigane,msifanye ghasia"

Tuhuma za udanganyifu uliokithiri,idadi ya wastani kama si ndogo ya watu walioteremka kupiga kura, na ukosefu wa wasimamizi katika baadhi ya majimbo,ni miongoni mwa mambo yanayoutia ila uchaguzi huo na kuwapa nguvu wale wanaoashiria uwezekano wa kufikiwa masikilizano kati ya mafahali hao wawili.

"Mabwana hawa wanasaka njia za kusikilizana kistaarabu" amesema hayo balozi mmoja wa magharibi.

Kwa mujibu wa duru hizo za kibalozi majadiliano yanaendelea kisiri siri ili kumshawishi Abdullah Abdullah akubali kushindwa tangu duru ya mwanzo ili badala yake akabidhiwe wadhifa muhimu serikalini.

Tangu muda sasa nchi za magharibi zimekua zikiishinikiza serikali ya Afghanistan ibuni wadhifa wa waziri mkuu.

Msimu wa kiangazi mwaka huu Abdullah Abdullah aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba Hamid Karzai alishauri kumkabidhi wadhifa huo,pindi akikubali kutopigania kiti cha rais.

"Matokeo ya mwanzo ya uchaguzi yatakayotangazwa kesho yanaweza kua matukio ya pirika pirika hizo" amesema mwanadiplomasia huyo wa magharibi.

Lakini kamisheni ya uchaguzi haijatangaza bado habari zozote,hata idadi ya walioteremka kupiga kura ambayo wachunguzi wa kimataifa wanaamini haikufikia asili mia 50,haijulikani.

Barack Obama Reform Plan
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: AP

Licha ya vitisho na visa vya matumizi ya nguvu vilivyofanywa na wataliban,rais wa Marekani Barack Obama amesifu moyo wa waafghanistan walioteremka vituoni na kusema:

Nnaamini mustakbal mwema ni wa wale wanaotaka kuijenga Afghanistan na sio wale wanaotaka kuivuruga."

Mwandishi :Hamidou Oummilkhheir/AFP

Mhariri:M.Abdul Rahman