1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya Uchaguzi Afghanistan kutangazwa wiki hii.

Halima Nyanza12 Oktoba 2009

Tume ya Uchaguzi nchini Afghanistan siku chache zijazo, inatarajia kutangaza uamuzi wake juu ya madai juu ya Udanganyifu wakati wa uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/K4Ll
Rais wa Afghanistan Hamid Karzai, je matokeo yatampa nafasi tena?.Picha: AP

Maafisa nchini humo wamesema kuwa uamuzi huo unaweza kutangazwa kabla ya mwisho wa wiki juu ya nani atakuwa Rais ajaye wa nchi au kama kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi kwa wagombea wakubwa wawili, Rais anayetetea nafasi yake Hamid Karzai na mpinzani wake mkuu, Abdullah Abdullah.

Wa Afghani walipiga kura Agosti 20 mwaka huu, kuchagua rais wa nchi hiyo, lakini uchaguzi huo ulitawaliwa na madai na madai ya kufanyika kwa udanganyifu, ambayo mengi yalimkabili Rais Hamid Karzai, ikiwemo uchunguzi uliofanywa na Waaangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya kutilia shaka robo ya kura zote au kura milioni 1.5 zilizopigwa.

Wakati maafisa nchini Afghanistan wakitangaza hayo, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Kai Eide amekiri kwamba Uchaguzi huo wa Rais wa mwezi Agosti, ulikuwa na udanganyifu mkubwa.

Ameyasema hayo jana katika mkutano wake na Waandishi wa Habari kujibu tuhuma zilizotolewa na msaidizi wake wa zamani Peter Galbraith kwamba alificha ushahidi wa vitendo vya udanganyifu katika uchaguzi huo, katika hali ya kumkingia njia ya ushindi Rais Karzai.

Peter Galbraith Afisa mwandamizi wa Marekani katika ubalozi wa umoja wa mataifa alipoteza kazi yake baada ya kuhitilafiana na viongozi wake kuhusiana na jinsi ya kulishughulikia suala la madai makubwa ya udanganyifu katika uchaguzi mkuu.

Bwana Karzai ameongoza katika matokeo ya wali ya uchaguzi huo kwa kupata asilimia 55 ya kura, huku mpinzani wake Abdullah Abdullah akipata karibu asilimia 28.

Dr Abdullah Abdullah
Dokta Abdullah Abdullah, mpinzani mkuu wa Rais Karzai.Picha: DW

Maandalizi yamekuwa yakifanywa kwa ajili ya kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi kati ya Rais Karzai na mpinzani wake huyo, ambapo wachambuzi wa mambo wanasema inapaswa kufanyika haraka iwezekanavyo kabla ya kuanza majira ya baridi, hali ambayo italeta ugumu wa maeneo mengi ya nchi hiyo kupitika.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: