Matokeo ya michezo katika Juma. | Michezo | DW | 27.10.2006
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Matokeo ya michezo katika Juma.

Miongoni mwayo Bundesliga kutimua tena vumbi Jumamosi hii

Mkamerun Pierre Wome anayechezea Werder Bremen akimtoka Claudio Pizzaro wa Bayern Munich Jumamosi iliopita. Bremen ilishinda mabao 3-1.

Mkamerun Pierre Wome anayechezea Werder Bremen akimtoka Claudio Pizzaro wa Bayern Munich Jumamosi iliopita. Bremen ilishinda mabao 3-1.

Kandanda la Ujerumani:

Kilabu ya Hertha Berlin hatimae imepewa ushindi na chiama cha soka cha taifa DFB dhidi ya kilabu ya Stuttgarter Kickers kusimamishwa mpambano wa timu hizo mbili wa kuwania kombe la Ujerumani. Kamati maalum ya chama cha soka nchini iliipa Hertha ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu hiyo ya daraja la tatu abaada ya mshika kibendera kupigwea na kikombe cha plastiki kilichojaa pombe, ambacho kilivurumishawa na shabiki mmoja wa Stuttgarter Kickers wakati wa apambano hilo Jumatano iliopita.

Tukio hilo lilitokea katika dakika ya 81 ya mchjezo. Muamuzi ambaye awali alikua tayari ameshawatoa nje wachezaji wawili, mmoja kutoaka kila timu, aliumaliza mchezo dakika 9 kabla ya wakati, huku hertha inayocheza ligi ya daraja la kwanza Bundesliga ikiongoza mabao 2-0.

Polisi walisema jana kwamba mtu mmoja wa miaka 38 ametiwa nguvuni. Mtu huyo anafahamika kuwa ni mmoja wa wahuni wa soka, lakini kwa miaka 10 hadi 15 hivi hakuwa mwana harakati. Mtu huyo aliyeachiwa baaadae anakabiliawa na mashitaka ya kujeruhi.

Kocha wa Stuttgarter Kickers Robin Dutt alisema kisa hicho ni janga kwa kilabu yake, akiongeza” tunajaribu mno kuweka sifa nzuri ya kilabu lakini ghafla anazuka mtu kuichafua.”

Ligi kuu ya Ujerumani Bundesliaga, inatimua tena vumbi leo jioni baada ya michuano ya kombe la Ujerumani katikati mwa wiki. Nurenberg inumana na Borrusia Dortmund, Bayern Munich iliopokonywa usukani na Bremen wiki iliopita abaada ya kulazwa mabao 3-1 leo inaumana na Eintracht Frankfurt nyumbani Munich wakati Monchengladbach itaikaribisha Bayer Leverkusen.

Cottbus inacheza na Hertha Berlin, Hambur inayoendelea na juhudi za kujikwamu kutoka nafasi tatu za mkiani itakua nyumbani ikicheza na Hannover na Bochum inachuana na Wolfsburg. Hapo kesho Jumapili Arminia Bielefeld itachuana na Alemania Aachen wakati Schalke iliiopanda hadi nafasi ya pili wiki iliopita itakua ugenini kutoana jasho na Stuttgart

Wakati huo huo Mchezaji wa Schalke Mbrazil Lincoln atakua nje ya uwanja wa mazoezi kwa majuma mawili kutokana ana matatizo ya misuli, aliyoyapata wakati wa mazoezi. Lincoln kwa hivyo hatokuwemo katika kikosi cha kesho cha Schalke wakati itakapoumana na Stuttgart. Schalke bila shaka itakua inawania ushindi baaada ya kuwa pointi sawa na Bremen wiki iliopita na zote mbili kushika uongozi huku Bremen ikitangulia kwa wingi wa magoli.

Hata hivyo Schalke ilitolewa katika michuano ya kombe la Ujerumani ilipokandikwa na timu ya daraja la pili FC Cologne mabao 4-2. Mbali na Lincoln pia Schalke inakumbwa na pigo jengine- Mruguay Rodriguez anayecheza nafasi ya ulinzi aliumia wakati wa mchuano na Cologne na mchezaji wa kiungo Kobiashvili ana maumivu ya paja.

Naye mshambuliaji hatari Muargentina Diego Kilimowicz, atakua nje ya chaki kwa majuma matatu hadi manne baada ya uchunguzi wa pili kuonyesha ana majeraha makubwa zaidi kuliko ilivyofikiriwa awali. Kilomowicz anayechezea Wolfsburg hakuonekana uwanjani tangu Septemba 14 akiwa na matatizo ya misuri ya mguu. Wolfsburg wako nafasi ya tatu kutoka mkiani katika Bundesliga , ikiwa na pointi 7 tu kutokana na mechi 8, kabla ya pambano la leo na Bochum.

Naye mchezaji wa kimataifa wa Jamhuri ya Cheki David Jarolim amerefusha mkataba wake na Hamburg hadi 2010. Jarolim anayecheza nafasi ya kiungo aliwasili kujiunga na klilabu hiyo ya kaskazini mwa Ujeruamani 2003, baada ya awali kuichezea Bayern Munich 1997-2000 na Nuremberg 2000-2003. Mpaka sasa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 ameshaichezea mara sita timu ya taifa ya Cheki. Mbali na Jarolim, Hamburg imetangaza pia kumrefushia mkataba mlinda mlango Sascha Kirschtein mwenye umri wa miaka 26 hadi 2011.

Nje ya Ujerumani , Manchester United inayoongoza katika ligi kuu ya England Premier League, leo itatoana jasho na bolton wanderers. Bolton ambayo ni wagumu kufungwa nyumbani, wanawania kulinda heshima hiyo, huku Kocha wa MANU Sir Alex Furguson akikusudia kumaliza udhia na kujiweka nafasi nzuri zaidi katika uongozi wa ligi hiyo. Bolton iko nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo. Manchester United ilichukua uongozi wa Primier League wiki iliopita baada ya kuibwaga Liverpool, ikiwaacha Chelsea nafasi ya pili kwa tafauti ya magoli.

Mchezaji wa Aston Villa Stilian Petrov atakaribishwa tena kujiunga na timu ya taifa ya nyumbani Bulgaria iwapo atabadili mawazo juu ya kujiondoa katika michuano ya kimataifa.

Akiwa na umri wa miaka 27 Petrov aliyekua nahodha wa timu ya taifa aya Bulgaria aliishituwa timu hiyo alipotangaza anastaafu michuano ya kimataifa siku moja baada ushindi wa timu hiyo wa bao 1-0 dhidi ya Lexembourg katika mchuano wa kundi G wa kuwania tiketi ya fainali za kombe la ulaya 2008. Ushindi huo uliisogeza Bulgaria katika nafasi ya pili, ikiwa nyuma ya Uholanzi.

Kocha Tristo Stoichkov alisema mlango uko wazi kwa Petrov ikiwa ataamua kurudi tena katika timu ya taifa.

Mchezaji huyo alinukuliwa akisema hataki kuichezea timu ya taifa chini ya kocha Stoichkov. Mchuano mwengine wa Bulgaria katika kinyanganyiro cha pombe la Ulaya utakua Machi 28 mwakani itakapoumana na Albania.

Barani Afrika Shirikisho la kandanda la kimataifa FIFA wiki hii lilipitisha uamuzi wa kuifungia Kenya kushiriki katika mashindano yote yatakayosimamiwa na Shirikisho hilo. Uamuzi huo unatokana na chama cha kandanda nchini Kenya KFF kushindwa kutekeleza maagizo ya FIFA juu ya mzozo kati ya chama hicho cha soka KFF na ligi kuu nchini Kenya. Hatua hiyo imewashtuwa na kuwasikitisha mashabiki wa soka katika taifa hilo la Afrika mashariki .

Na wakati Afrika kusini ikiendelea kujiandaa na mashindano ya kandanda ya kombe la dunia 2010, rais Thabo Mbeki wa nchi hiyo amesisitiza tena nia ya nchi yake kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa na kuondoa wasi wasi kwamba huenda maandalizi yasikamilike kwa wakati unaotakiwa.

Mbeki alikua akizungumza katika semina ya siku mbili Juma hili iliyoandaliwa na Shirikisho la kandanda duniani FIFA mjini Cape Town na kuhudhuriwa na mawaziri wa serikali, wadau, wafadhili , waakilishi wa vyama vya wafanyakazi na wafanya biashara. Rais Mbeki alisema maandalizi ni pamoja na viwanja vinavyohitajika, ukarabati na ujenzi wa miundo mbinu zaidi na mifumo ya mawasiliano pamoja na kuhakikisha usalama kamili.

 • Tarehe 27.10.2006
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHd3
 • Tarehe 27.10.2006
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHd3