1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya michezo katika Juma

Mohammed Abdul-Rahman4 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CHcE

Kandanda :

Kama ujuavyo mashindano ya vilabu barani ulaya kwa msimu huu, tayari yamefikia hatua ya fainali-zikiwa ni za kombe la vilabu bingwa mashindano yanayojulikana kama Champions League, na kombe la umoja wa vyama vya kandanda abarani Ulaya UEFA. Fainali inayosubiriwa kwa hamu ya Champions League itakua ni kati Liverpool ya England au ukipenda Uingereza na AC Milan ya Italia. Baada ya Liverpool kuwatoa wapinzani wao wa nyumbani Chelsea kwa mikwaju ya Penalty- mchuano uliowasisimua kuanzia mashabiki uwanjani hadi waliokua wakiuangalia katika runinga kote duniani na Manchester kuyaaga mashindano kwa kipingo cha mabao 3-0 katika mchezo wa pili na AC Milan. Fainali ya mashindano hayo itachezwa mjini Athens Ugiriki tarehe 23 mwezi huu.

Katika kombe la UEFA Sevilla ya Uhispania ndiyo itakayocheza fainali na kilabu nyengine ya nyumbani Espanyol. Sevilla iliitoa Osasuna pia ya Uhispania kwa ushindi wa mabao 2-1 kwa michuno yote miwili na Espanyol ikaifungisha virago Werder Bremen ya Ujerumani kwa jumla ya mabao 5-1 katika matokeo ya duru zote mbili, nyumbani na ugenini. Bremen ilikua timu ya mwisho ilisalia katika mashindano ya ulaya. Kombe hilo la UEFA limedhihirika kutawaliwa na vilabu vya Uhispania kwa maana ya kwamba vyovyote matokeo yatakavyokua kombe litakwenda nyumbani pale Sevilla itakapomenyana na Espanyol. Sevilla inayolishikilia kombe hilo, itajaribu kulitetea libakia nyumbani kwa mara ya pili mfululizo fainali hiyo itachezwa Glasgow- Scotland. Sevilla pia inawania kushinda ubingwa wa ligi na kombe la taifa msimu huu.Ingawa ni mara ya kwanza vilabu viwili vya uhispania vinachuana katika fainali ya kombe la UEFA, kwa jumla itakua mara ya sita kwa timu za uhispania kuumana katika fainali za vikombe vya ulaya .

Mmiliki wa kilabu ya AC Milan Silvio Berlusconi, anasema atafurahi kumrudisha Andrily Shevchenko, mshambuliaji hatari wa Ukrain kama ataamua kuiacha kilabu yake ya sasa ya Chelsea ya Uingereza. Mchezaji huo aliiacha AC Milan kujiunga Chelsea mwaka jana katika makubaliano ya kitita cha euro 45 milioni, lakini hadi sasa amefunga magoli mawili katika mechi nne za ligi , akishindwa kutia fora katika ligi kuu ya Uingereza.Schevchenko mwenye umri wa miaka 30, hakuwemo katika kikosi kilichochuana na Liverpool katika kombe la vilabu bingwa barani ulaya jumanne iliopita. Mchezaji huyo alichaguliwa mwanasoka bora wa Ulaya 2004 na hivi karibuni amekua akisumbuliwa na majeraha.

Habari kutoka Ufaransa zinasema mabingwa wa soka nchini humo Lyon wanaazimia kuwaasajili wachezaji watatu msimu ujao. Rais wa kilabu hiyo Jean Michel Aulas amethibitisha wakati huo huo jana kwamba Gerard Houllier ataendelea kuifundisha timu hiyo, na kwamaba huenda wachezaji saba hadi wanane wakaihama. Hata hivyo hakuwataja wachezaji watatu maarufu ambao Lyon inawasaka kujaza pengo la wachezaji watakaoihama.

Ligi kuu ya Ujerumani-Bundesliga:

Ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga inarudi tena mwishoni mwa juma hili, huku mashabiki wa timu tatu za usoni Schalke inayoongoza Stuttgart nafasi ya pili na Bremen katika nafasi ya tatu wakizidi kiwewe. Schalke inacheza nyumbani ikiikaribisha Nuremberg, Stuttgart pia iko nyumbani ikichuana na Mainz inayokabiliwa na hatari ya kushuka daraja, katika pambano linalotarajiwa kuwa kali. Nayo Bremen kesho itamenyana na Hertha Berlin mjini Berlin. Matokeo ya mwishoni mwa juma yatatoa sura halisi ya nani ana nafasi kubwa zaidi ya kuibuka bingwa kati ya Schalke, Stuttgart na Bremen.

Ubondia:

Mabondia wawili mashuhuri Mmarekani Oscar De La Hoya na mmarekani mwenzake Floyd Mayweather wanazipiga leo huko Las Vegas katika pambano a la kuwania ubingwa wa taji la utzani wa super welter la shirika la ndondi la World Boxing Council-WBC. Pambano hilo linalozingatiwa kuwa miongoni mwa pamabano ya kusisimua katika historia ya ndondi, linasubiriwa kukiwa na uhasama kati ya mabondia hao wawili. De La Hoya alisikika akitamka kawa majigambo“ Mimi simchukii mtu yeyote lakini tu simjali hata kidogo.“ Kwa upande wake Mayweather naye ameendelea kumtusi mpinzani wake akiyapinga madai kwamba na wivu na mafanikio ya De La Hoya ambaye anatajwa kuwa bondia aliyejipatia mafanikio makubwa kifedha miongoni mwa mabondia wasiokua wa wizani wa juu duniani.

Ama Alexander Munoz wa Venezuela anaendelea kusherehekea ushindi wake wa Alhamisi , baada ya kumwaga Nobuo Nashirio wa Japan na kulitwaa tena taji la ubingwa wa wizani wa fly katika shirika la ndondi la World Boxing Association-WBA kwa wingi wa pointi.

Riadha:

Bingwa wa dunia Jeremy Wariner amesema kwamba anaweza kutambuliwa kama mkimbiaji bora kabisa wa masafa ya mita 400, ikiwa atafanikiwa kuvunja rekodi ya sekunde 43. Mmarekani huyo mwenye umri wa miaka 23 ni miongoni mwa watakaoshiriki kartika mashindano ya leo mjini Osaka Japan, ya Shirikisho la kimataifa la wanariadha awa ridhaa-IAAF. Anayeshikilia rekodi ya dunia kwa sasa ni Michael Johnson awa Marekani kwa muda wa sekunde 43 nukta 18 aliyoiweka 1999, wakati muda bora wa Wariner binafsi ni sekunde 43 nukta 62.Mashindano ya riadha ya dunia mwaka huu, pia yatafanyika katika uwanja wa michezo wa Nagai huko Osaka kuanzia Agosti 25 hadi Septemba 2.