1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matarajio ya amani yafifia Mashariki ya Kati

Miraji Othman2 Novemba 2009

Amani iko mbali Mashariki ya Kati

https://p.dw.com/p/KLbY
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hilary Clinton(kulia), na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu katika mkutano na waandishi wa habari mjini JerusalemPicha: AP

Wakati amani ya Mashariki ya Kati ikionekana hivi sasa kuwa mbali kuwahi kufikiwa kuliko wakati wowote mwengine, waziri mkuu wa Wapalastina, Salam Fayyad, ana mkakati mpya wa kuundwa dola ya Kipalastina bila ya kutegemea mashauriano yanayoungwa mkono na Marekani. Anasema mpango wake sio kwa Wapalastina kujitangazia wenywewe dola yao, lakini waunde hali halisi ya mambo ambayo itailazimisha jamii ya kimataifa idai kutolewe uhuru kwa Wapalastina. Mwishoni mwa wiki, kwa mshangao, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Bibi Hilary Clinton, alizitaka pande zote mbili, Israel na Wapalastina, zirejee katika meza ya mashauriano na akasema Wapalastina kushikilia kwamba Israel iwachane kabisa na kujenga makaazi ya Wayahudi katika ardhi za Wapalastina- jambo ambalo mwanzo lilikuwa linaungwa mkono na Marekani- isiwe ni shuruti kabla ya kuanzishwa tena mazungumzo ya amani yaliosimamishwa wakati wa Vita vya Gaza.

Salam Fayyad aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa, AFP, kwamba mpango wake ni wa kujenga na sio wa kubomoa, na msingi wake ni fikra ya kuunda hali halisi ilio nzuri. Alisema mpango wake huo hautoathirika na kile anachokiona kuwa ni kushindwa mwenendo wa amani, baada ya kupita miaka kumi na sita ya kuingia na kutoka au kutokana na upinzani wa Wapalastina wa kuanza tena kufanya mashauriano bila ya kusimamishwa ujenzi wa makaaziya Wayahudi katika ardhi za Wapalastina. Alisema ulikuwa wakati sasa wa kuudurusu upya mpango mzima wa mwenendo wa amani . Malengo ya mpango wake ni kuundwa taasisi za dola imara ya Kipalastina ifikapo mwaka 2011, bila ya kujali kama maendeleo yeyote yanafanyika katika mazunguzmzo na Israel.

Jumamosi iliopita, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Bibi Hilary Clinton, alizitaka pande zote mbili- Israel na Wapalastina- zirejee katika meza ya mashauriano na akasema kwamba kushikilia kwa Wapalastina kwanza Israel isitishe ujenzi wa makaazi ya Wayahudi katika ardhi za Wapalastina isiwe ni shuruti ya kurejewa mazungumzo ya amani. Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani alisema mjini Jerusalem:

"Hakujakuweko na sharti, maisha lilikuwa ni suala la mashauriano. Nini kile ambacho waziri mkuu Netanyahu alichotoa ni maelezo juu ya kujizuwia katika siasa ya ujenzi wa makaazi, ambayo ameyaelezea punde, kwa mfano, kwamba hakuna kuanzishwa ujenzi mpya ni jambo ambalo halijawahi kuweko, kufuatana na mfumo wa hali ya kabla ya mashauriano."

Tamko hilo la Hilary Clinton liliwafurahisha Wa-Israel wengi, naye waziri mkuu wao, Benjamin Netanyahu, alisema

"Dai la Wapalastina ni jipya, ni mabadiliko ya siasa, siasa ya Wapaalstina, na halisaidii sana kwa amani. Halisaidii kuyasukuma mbele mashauriano, kwa hakika, linatumiwa kama kisingizio, kama kikwazo cha kuzuwia kurejewa tena mashauriano. Sasa nikwambieni. Suala la makaazi, suala la ardhi, suala la mipaka, haya ni mambo yatakayofanyiwa mashauriano na yatabidi yasuluhishwe kwa ajili ya mkataba wa amani utakaofikiwa."

Watu wachache wanataraji waziri mkuu wa Israel , mwenye siasa kali , ataregeza kamba kuhusu suala la ujenzi wa makaazi ya Wayahudi bila ya kuweko mbinyo kutoka Marekani. Lakini Salam fayyad anasema uzuri wa mpango wake ni kwamba unaweza kwenda aidha katika njia hizo mbili. Yeye anataraji mwishowe kwamba jamii ya kimataifa itailazimisha Israel iondoke kutoka Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Jerusalem Mashariki, ardhi ambazo Israel ilizitwaa katika vita vya siku sita vya mwaka 1967.

Rais Mahmud Abbas wa Wapalastina alipokutana hapo kabla na Bibi Clinton huko Abu Dhabi, alisema:

Mahmud Abbas
Rais wa Wapalastina, Mahmud AbbasPicha: AP

"Tumezungumza hasa juu ya mwenendo wa amani na vipi tutaweza kuufufua. Msimamo wetu tumeusisitiza kwamba amani inahitaji kuregeza kamba, nako ni kusimamishwa ujenzi wa makaazi ya walowezi kufutana na mwenendo tuliokubaliana na waziri mkuu Olmert na waziri wa mambo ya kigeni Livni. Mwenendo huo unaanzia Israel kurejea katika mipaka ya mwaka 1967."

Kuhusu kurejea nyuma Marekani katika msimamo wake wa mwazo ambao uliishikilia Israel isitishe ujenzi wa makaazi ya Wayahudi, nchi nyingi za Kiarabu zimeonesha kuvunjwa moyo na hali hiyo, hivyo matumaini ya amani katika Mashariki ya Kati yanazidi kufifia.

Mwandishi: Miraji Othman/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdulrahman