1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matamshi ya chuki katika mitandao ya kijamii Kenya

Wakio Mbogho2 Novemba 2017

Katika mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook, matamshi ya chuki na taarifa za uzushi imekuwa desturi. Wataalam wanaonya kuhusu hisia za mgawanyiko nchini humo hasa wakati baadhi ya wakenya wanapohisi kunyimwa haki.

https://p.dw.com/p/2mt5v
Kenia Wahlen - Ausschreitungen in Nairobi
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Nchini Kenya wakati uchaguzi umemalizika na mshindi kutangazwa. taifa hilo bado limo katika mivutano ya kisiasa inayotishia  mgawanyiko mkubwa kutokana na matamshi ya chuki  yanayozidi kusambazwa katika mitandao ya kijamii.

Mgogoro huu wa kisiasa nchini Kenya umekuwepo tokea kampeni za uchaguzi hadi sasa wakati uchaguzi umemalika, na licha ya juhudi za kusitisha uhasama uliopo, bado hakuna dalili ya suluhu kamili. Katika mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook, matamshi ya chuki na taarifa za uzushi imekuwa desturi. Kila uchao vitambulisho vipya vinabuniwa ambapo wafuasi wa upinzani ama wanaoiunga mkono serikali wanavitumia kushinikiza maoni na misimamo yao na hata kushambuliana.

Malezo kuhusu usalama wa mitandao kutumia vibonzo
Malezo kuhusu usalama wa mitandao kutumia vibonzoPicha: picture-alliance/Tagesspiegel/K. Kleist-Heinrich

Baadhi ya vitambulisho hivi maarufu ni kama #Luolivesmatter, #Wembeniuleule, #NRMK, #ChebukatiBurnsKenya, #ElectionBoycottke na #Kenyanshavoted. Kamishna katika tume ya uwiano na uatangamano NCIC, Prof Gitile Naituli anasema Wakenya wengi wanatumia chombo hiki kijielezea hasa wale wanaotofautiana na matukio ya uchaguzi uliokamilika nchini, kwa kukosa njia nyingine ya kujieleza. Ingawa hakubaliani na taarifa na matamshi yanayosambazwa kwenye mitandao hii, anakiri kwamba imekuwa vigumu kukidhibiti chombo hiki.

Swali la iwapo wakenya wako tayari kusonga mbele na kuyasahau matukio ya uchaguzi ni jambo nyeti. Wataalam wanaonya kuhusu hisia za mgawanyiko nchini hasa wakati baadhi ya wakenya wanapohisi kunyimwa haki. Muungano wa mashirika ya kijamii jijini Nairobi hivi karibuni walielezea hofu kufuatia matukio ya uchaguzi wa urais uluiokamilika waliosema ulishuhudia idadi ndogo sana ya wapiga kura.

Waandamanaji Kawangware Oktoba 28, 2017
Waandamanaji Kawangware Oktoba 28, 2017Picha: Reuters/T. Mukoya

Kulingana nao ni maeneo ya bonde la ufa na kati pekee yaliyoandikisha zaidi ya asilimia 50 ya watu waliopiga kura, hatua ambayo wanasema inatilia shaka zoezi hilo lote. Peter Kuria, mtaalam kutoka shirika la kijamii la Nakuru Human Rights Network, anaeleza kwamba matukio ya uchaguzi nchini yameibua migawanyiko kati ya wananchi pamoja na taasisi mbalimbali.

Prof Gitile Naituli anaonya kwamba serikali inafaa itambue na ikiri kwamba kuna tatizo katika taifa hili na kisha itoe fursa ya kuwasikiza viongozi wote wa kisiasa, la sivyo itakuwa vigumu kutekeleza zoezi la uchaguzi wa mwaka 2022 nchini.

Zoezi la  uchaguzi mpya  nchini Kenya lilitekelezwa  katika hali ya mvutano mkubwa wa kisiasa kati ya  chama tawala Jubilee na muungano wa upinzani NASA.Uhuru Kenyatta akachaguliwa tena kama rais kwa muhula wa pili.

Mwandishi: Wakio Mbogho

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman.