1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya NATO yachangia wanajeshi zaidi Afghanistan

Sekione Kitojo4 Desemba 2009

Mataifa 25 wanachama wa jumuiya ya NATO wameahidi leo kutuma wanajeshi wengine 7,000 nchini Afghanistan , wakiunga mkono mkakati mpya wa rais Barack Obama .

https://p.dw.com/p/KqXc
Katibu mkuu mpya wa NATO Anders Fogh Rasmussen .Picha: AP

Mataifa 25 wanachama wa jumuiya ya NATO wameahidi leo kutuma wanajeshi wengine 7,000 nchini Afghanistan , wakiunga mkono mkakati mpya wa rais Barack Obama na kuongeza kasi ya juhudi za kimataifa za kupambana na Taliban.

Mbali ya kuwa ni muhimu, ahadi ya kupatiwa wanajeshi hao , imeshindwa kufikia kiasi cha wanajeshi 10,000 ambao maafisa wa wizara ya ulinzi walitarajia na kiasi hicho cha wanajeshi kitakwenda katika kutoa mafunzo tu ya wanajeshi wa Afghanistan ili kuchukua jukumu la ulinzi wa usalama wa nchi hiyo.

Kufuatia mkutano na mawaziri wa mambo ya kigeni wa NATO, katibu mkuu wa jumuiya hiyo Anders Fogh Rasmussen amesema kuwa amepokea ahadi za kupata wanajeshi wa ziada, kukiwa na uwezekano wa nchi nyingi zaidi kuchangia katika jumla hiyo ya wanajeshi katika muda wa miezi michache ijayo.

ISAF itakuwa na takriban wanajeshi 37,000 zaidi mwakani 2010 kuliko mwaka huu.

Mataifa yanachukua jukumu la kutimiza ahadi zao. Hii ni hatua ya mshikamano na itakuwa na athari kubwa katika mapambano. Kwasababu nchi za ISAF zimekubaliana kuhusu ramani mpya ya njia kwa ajilki ya kazi hii. Ndio kutakuwa na wanajeshji zaidi, lakini pia kuna mtazamo mpya katika kuwalinda raia wa Afghanistan.

Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa rais Obama hapo Desemba mosi ya kutuma wanajeshi 30,000 zaidi wa Marekani nchini Afghanistan , akijaribu kubadilisha mwelekeo katika vita vya miaka minane sasa na kuweza kuwavunja nguvu Wataliban ambao wamekuwa wakipata nguvu zaidi katika mwaka mmoja uliopita.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton ameyataka mataifa wanachama wa NATO na washirika wake nchini Afghanistan kuunga mkono mkakati mpya ili kupambana na wapiganaji na kuimaliza kazi kwa pamoja.

Hivi ni vita vyetu, kwa pamoja. Na ni lazima tumalize pamoja, amewaambia mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi wanachama wa NATO mjini Brussels, baada ya rais Barack Obama wa Marekani kuamuru kutumwa wanajeshi 30,000 zaidi nchini Afghanistan na kuwataka washirika kuchukua hatua kama hiyo.

Marekani haitawataka wengine kufanya kitu ambacho hatuko tayari kufanya wenyewe, amesema Hillary Clinton wakati jeshi la kimataifa la kutoa msaada ISAF linapata shida kuweza kuwavunja nguvu wapiganaji wa Taliban na al Qaeda.

Wakati wanajeshi hao wa ziada wanawakilisha juhudi za ziada , lakini ahadi hizo ni lazima zioane pia na mpango wa Uholanzi na Canada wa kuwaondoa wanajeshi wao 4,900 katika mwaka 2010 na 2011, kutokana na raia wa nchi hizo kuzidi kupinga vita hivyo.

NATO inahitaji kundi la wataalamu zaidi ya 200 wa kutoa mafunzo kwa polisi na jeshi ili kuimarisha jeshi la Afghanistan ili kuweza kuchukua jukumu la ulinzi na kuweza kuruhusu majeshi ya kigeni kuondolewa.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton , ambaye alikuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na katibu mkuu wa NATO Rasmussen , amesema kuwa Marekani inahitaji misaada kadha, ikiwa ni pamoja na msaada wa kiraia pamoja na mafunzo ya wanajeshi , ili kuitayarisha Afghanistan kuchukua jukumu la kuielekeza nchi hiyo vile inavyotaka.

Mwandishi ; Sekione Kitojo / RTRE/AFPE.

Mhariri : Mohamed Abdul Rahman