1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika ya Kijerumani yajenga barabara Kongo Mashariki

Nikola Klein / Maja Dreyer27 Agosti 2007

Mwaka mmoja uliopita raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo walipiga kura na kuuimarisha mfumo wao mpya wa Kidemokrasi. Hata hivyo, tunaendelea kupata habari juu ya mapigano, mauaji, uporaji na ubakaji kutoka eneo la Mashariki mwa nchi hiyo. Pamoja na juhudi za kijeshi zinazoendelea, kuna mashirika kadhaa yanayopigania maisha ya kawaida yawe kweli ya kawaida tena, mfano ni shirika la kupambana na njaa duniani, Welthungerhilfe.

https://p.dw.com/p/CHjZ
Maeneo mengi Kongo Mashariki hayawezi kufikiwa
Maeneo mengi Kongo Mashariki hayawezi kufikiwaPicha: picture-alliance/dpa

Baada ya vita kumalizika rasmi na uchaguzi kufanyika, bado eneo la Mashariki linaendelea kukabiliwa na matatizo mengi. Kwani eneo hilo ambapo idara za serikali hazina nguvu nyingi tena ni lenye mali ghafi nyingi. Ndiyo sababu, makundi mengi ya wanamgambo, wakiwa ni wa ndani au wa kutoka nje, wanapigania mamlaka.

Georg Dörken ni wa shirika la Kijerumani la kupambana na njaa duniani "Welthungerhilfe" naye anaeleza hali ilivyo: "Pale ambapo vita vilianza mwaka 1996 bado kila siku kunatokea mauaji. Bado wanawake wengi wakiwa 1000 au hata zaidi ya 3000 hubakwa kwa mwezi, bado kuna viongozi wa makundi ya wanamgambo ambao kila mmoja wao ana maslahi yake. Wengine wanapigana dhidi ya serikali, wengine wanataka kuchimba madini fulani na kuiuza kwa njia isiyo halali.”

Ni jambo linalotokea mara kwa mara kuwa wanamgambo wanavishambulia vijiji, huwaua wakaazi na kupora mali zao. Wako wanaonusurika na hukimbia na kutafuta msaada kutoka mashirika ya kutoa misaada kama shirika la “Welthungerhilfe”. Lakini wakishapata msaada na vitu fulani vya matumizi ya kila siku, hurudi makwao, pengine wanamgambo wanawashambulia tena na tena ni wakimbizi wanaohitaji msaada.

Licha ya kutoa msaada kama chakula au madawa, shirika la “Welthungerhilfe” lina lengo kubwa zaidi, yaani kuleta usalama. Mkakati wake ni kujenga barabara. Sehemu kubwa ya miundo mbinu ya mabarabara ya Kongo imeharibika chini ya utawala wa Mobutu. Kutokana na hayo, vijiji na maeneo mengine makubwa hayana njia kwendea sehemu nyingine ya Kongo au kusafirishia bidhaa. Kupitia barabara mpya wakimbizi wanatarajiwa kuweza kurudi makwao na vilevile zitawawezesha wakulima kusafirisha bidhaa zao na kuziuza nje kwa bei nafuu.

Goerg Dörken anaeleza zaidi: “Kwa vile barabara iko, wakulima wanapata bei nzuri zaidi. Kwa sababu ya barabara bei ya kilo 50 ya maharagwe inapanda kwa mara tano au sita. Kwa hivyo, wakaazi wanapata fedha zaidi, hivyo wanaweza kulipa mahitaji mengine kama elimu na vitu vingine vingi.”

Hivyo, shirika la “Welthungerhilfe” linataka kuhakikisha kuwa wakaazi wajitegemee. Pengine, siku za usoni, nchi nzima ya Kongo itaweza kunufaika na barabara hizo, kwani mbali na kuwa eneo lenye mali ghafi vile vile ardhi ni nzuri sana. Kama Bw. Dörken anavyoeleza shirika lake linataka kuimarisha sekta ya ukulima ili bidhaa zake ziuzwe pia Kinshasa.

Mradi mkubwa kwa sasa hivi ni kujenga barabara kutoka Goma mpaka Kisangani kwenye mto wa Kongo. Barabara hii itakuwa na urefu wa kilomita 700. Huko Kisangani bidhaa zinaweza kuwekwa kwenye meli na kusafirishwa hadi Kinshasa. Sehemu kubwa ya barabara imeshakamilishwa bila ya kazi kusumbuliwa na wanamgambo. Kwani hatimaye watu wote watanufaika kutokana na barabara hiyo mpya.