1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashindano ya riadha yaanza Barcelona Hispania

Josephat Nyiro Charo27 Julai 2010

Katika safu ya michezo, zaidi ya wanariadha mia saba wanakutana wiki hii mjini Nairobi Kenya kwa mashindano ya riadha wakiwemo wapinzani wa jadi Kenya na Ethiopia

https://p.dw.com/p/OW3y
Sherehe ya ufunguzi wa mashindano ya riadha mjini BarcelonaPicha: AP

Wanariadha mashuhuri wanakutana mjini Nairobi wiki hii kushiriki katika mashindano ya riadha yatakayofanyika chini ya ulinzi mkali hasa baada ya miripuko ya mabomu yaliyotokea katika mji mkuu wa Uganda Kampala.

Mabingwa wa bara hilo ikiwemo Kenya na Ethiopia watawahusisha wanariadha wao Linet Masai na Vivian Cheruiyot kupishana na Tirunesh Dibaba wa Ethiopia ambaye anarejea uwanjani baada ya kukosa mashindanoni kwa muda.

Jiji la Nairobi linaloandaa mashindano hayo kwa mara ya kwanza litashuhudia uwepo wa wachezaji 144 wakiwemo wanariadha na washiriki wa mashindano viwanjani. Kocha mpya, Stephen Mwaniki atakayekiongoza kikosi cha Kenya amekiri kwamba uwepo wa wanariadha hao kutaipa Kenya nafasi nzuri ya kuonyesha umaarufu wake kimichezo.

Mashindano hayo yatafanyika katika uwanja uliofanyiwa ukarabati wa Nyayo. Polisi nchini humo pia imesema itaunda kikosi maalum cha maafisa watakaowalinda wanariadha wakati wa mazoezi, wakati wa mashindano, yatakayochukua siku tano na pia katika mahoteli watakakopumzika.

Wanariadha wengi watatumia fursa hiyo ya mashindano kujitayarisha kwa mashindano ya jumuiya ya madola yatakayofanyika mjini New Delhi India mwezi Oktoba.

Na hapa Ulaya, Mrusi, Stanislav Emelyanov amefungua mashindano yalioanza ya riadha kwa kuibuka na medali ya dhahabu katika shindano la kutembea la kilomita 20. Mchezaji huyo mwenye umri wa mika kumi na tisa aliwashangaza wengi alipomaliza baada ya saa 1 na dakika 20.

Katika shindano la kuruka viunzi na maji, mita 400, Mrusi mwingine Natalya Antyukh alishinda kwa kumaliza baada ya sekunde 54.29 na akafuatwa na Mbulgaria Vania Stambolova.

Na tukiangazia dimba la kandanda, Timu ya Bolton imemsajili mchezaji wa kiungo cha kati, Marcos Alonso kutoka Real Madrid kwa kima cha pesa ambacho hakijatajwa. Mchezaji huyo matata mwenye umri wa miaka 19 amekubali kuichezea Bolton kwa miaka mitatu .

Na kwingineko, Meneja wa timu ya Rangers ya Scotland, Walter Smith amedhihirisha wazi hii leo kwamba ana nia ya kuwasajili wachezaji wawili wa Bafana bafana Bongani Khumalo na Katlego Mphela. Mazungumzo tayari yameanza . Khumalo mwenye umri wa miaka, 23 na Mphela wa miaka 24 wanaweza kuchukuliwa kwa kima cha Dola milioni 2.3 kila mmoja. Khumalo pia anasemekana kwamba ameivutia timu ya Tottenham.

Na hatimaye Mchezaji wa kati wa Ghana Kevin-Prince Boateng anatarajiwa kufika mahakamani mjini Berlin hapo kesho kwa tuhuma za kuyaharibu magari 12 na pikipiki, akiwa na mchezaji mwenzake wa zamani katika timu ya Hertha Berlin, Patrick Ebert, mwaka jana. Boateng hajathibitisha ikiwa ataenda mwenyewe mahakakani lakini mwenzake, tayari amelipa Euro 56,000 kama faini ya kuikamilisha kesi hiyo.

Mwandishi, Peter Moss /AFP

Mhariri, Sekione Kitojo.