1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi dhidi ya IS yashika kasi

7 Novemba 2016

Vikosi vya wapiganaji wa kikurdi wa kundi la Pershmega walioko nchini Iraqi leo wameushambulia mji unaoshikiliwa na kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu, IS, ulioko KaskaziniMashariki mwa mji wa Mosul, Bashiqa.

https://p.dw.com/p/2SGWr
Irak Mossul Gogjali,  Häuserkampf  Irakische Armee
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Drobnjakovic)

Mashambulizi hayo ni sehemu ya mkakati wa kuwafurusha wapiganaji wa kundi hilo la Dola la Kiislamu nje ya mji huo, wakati ambapo majeshi ya Iraqi nayo yakianzisha mashambulizi ndani ya mji na wapiganaji wa jihadi katika eneo la jirani la Mashariki mwa Mosul. 

Kundi la kwanza la kikosi cha wapiganaji 2000 wa Pershmega liliingia kwene eneo la Bashiqa, wengi wao wakiwa na magari yaliyosheheni silaha na wengine wakitembea kwa miguu, baada ya mji huo kushambuliwa kwa mizinga.
  
Wapiganaji wa kundi la IS, wametaka kupunguza mashambulizi katika mji wa Mosul, ambao ni ngome pekee wanayoishikilia kwenye mapigano ambayo leo hii yanaingia wiki ya nne, huku kukiwa na mashambulizi ya mabomu ya kujitoa muhanga yaliyotegwa kwenye magari. Makamanda wa Iraqi wanasema kulikuwa na wapiganaji 100, waliokuwa mstari wa mbele katika eneo la Mashariki na wengine 140 eneo la Kusini.

Wapiganaji hao wa Kikurdi wameendelea kukabiliana na wapiganaji wa IS, wakati wakiendelea kusonga mbele kutoka maeneo mawili tofauti wakiusogelea mji wa Bashiqa, ulioko Mashariki mwa Mosul unaoshikiliwa na kundi hilo la kigaidi. Mashambulizi yaliyofanywa asubuhi hii ni sehemu ya mpango wa kuwafurusha IS kutoka Mosul, mji ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Iraqi.

Syrien SDF PK Sturm auf Rakka
Msemaji wa vikosi vya usalama vya Syria, Jihan Sheikh Ahmed akitangaza kuanza kwa mashambulizi ya kuuchukua mji wa Raqa, unaoshikiliwa na kundi la Dola la Kiislamu.Picha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Bashiqa inayoaminika kukaliwa na wapiganaji wengi wa IS iko Kilomita 13 Kaskazini Mashariki mwa Mosul. Wapiganaji hao wa IS bado wanashikilia eneo kubwa lililoko Kaskazini, Kusini na Magharibi mwa Mosul, na wameendelea kusogeleea maeneo yanaokaliwa na raia wengi ili kuwatumia kama ngao ya vita.

Hata hivyo kutoka vikosi vya pershmega, Brigedier General Iskander Khalil Ghardi amesema, taarifa za kiintelijensia zinaeleza kuwa hakuna wakaazi wengi waliosalia Bashiqa, na hivyo vikosi vyake vitazidi kusonge mbele.

Katika hatua nyingine, majeshi ya Syria yanayoungwa mkono na Marekani yameanzisha mashambulizi mapya ya kuurejesha mji wa Raqqa, ambao pia ni ngome ya wapiganaji wa IS nchini Syria. Mashambulizi hayo pacha, ya Mosul na Raqqa yanataraji kuondoa kabisa mfumo wa kimadhehebu uliotangazwa na kiongozi wa kundi la Dola la Kiilsamu, Abu Bakr al-Baghdad.

Baghadadi aliwaambia wafuasi wake kwamba hakuna kurudi nyuma katika vita hivyo na maadaui zao. 

Na huko Kusini mwa Mosul, majeshi ya usalama yamesema yameurejesha mji wa Hamman al Alil kutoka kwa wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu, ambao kulingana na maelezo yao, wapiganaji hao walikuwa wamewahifadhi raia wengi watakaowatumia kama ngome ya vita, huku wakiwatanguliza raia wengine mbele ya wapiganaji waliokuwa wakielekea Mosul ili kukabiliana na mashambulizi ya anga. 

Na eneo la Kusini mwa Mosul, taarifa za kijeshi zinasema Kikosi cha 16 cha jeshi lake kimefanikiwa kukirejesha kijiji cha Bawiza na kuingia kwenye eneo jingine, Sada, lililopo kwenye mipaka, Kaskazini mwa Mosul, hatua inayoongeza ugumu dhidi ya vikosi vya wapiganaji vya IS. 

Mwandishi: Lilian Mtono/ APE/ RTRE.
Mhariri:Yusuf Saumu