1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya Kigaidi yaitikisa Cairo

24 Januari 2014

Watu wasiopungua wanne wameuwawa na dazeni kadhaa kujeruhiwa kufuatia mashambulio matatu ya mabomu karibu na vituo vya polisi katika mji mkuu wa Misri Cairo .

https://p.dw.com/p/1AwW4
Askari polisi atibiwa baada ya shambulio dhidi ya makao makuu ya polisiPicha: Reuters

Shambulio la kwanza limetokea katika uwanja yanakowekwa magari katika makao makuu ya polisi mjini Cairo pale mtu mmoja aliyeyatowa mhanga maisha yake alipojiripuwa akiwa ndani ya gari.

Kwa mujibu wa duru za idara za usalama watu wasiopungua wanne wameuwawa na wengine 70 kujeruhiwa.Shambulio hilo limebomowa ukuta wa jengo la usalama kunakokutikana kituo cha polisi na idara ya usalama wa taifa.Jengo la makumbusho ya sanaa ya kiislam nalo pia limebomoka.Askari polisi watatu ni miongoni mwa wahanga wa mashambulio hayo.Ripota wa shirika la habari la Uingereza-Reuters amesema mripuko umepelekea viyoo vya maduka ya karibu na hapo kuvunjika na vigae ,vyuma na mbao kutapakaa mita mia kadhaa kutoka mahala shambulio hilo lilikotokea.

Shambulio la pili limetokea katika kituo cha polisi cha Talbeya,katika eneo la Ihram huko Gizah karibu na Cairo,muda mfupi baada ya shambulio la bomu dhidi ya makao makuu ya polisi.Hakuna ripoti iliyotangazwa kuhusu hasara iliyopatikana.Na la tatu limetokea mbele ya ofisi ya polisi magharibi ya mji mkuu Cairo katika njia panda inayoelekea katika eneo la ihram la Gizah.

Televisheni ya taifa inasema mtu mmoja ameuwawa lakini ripoti hiyo bado haikuthibitishwa.

Ansar-Beit al-Maqdes ladai kuhusika na mashambulio

Polisi ya kuzuzwia fujo imewatawanya mamia ya wafuasi wa utawala mpya waliokuwa wakiwakaripia wafuasi wa rais aliyepinduliwa Mohammed Mursi kuwa nyuma ya mashambulio hayo.

Ägypten Verbot der Muslimbrüder
Chama cha Udugu wa kiislam chapigwa marufukuPicha: Reuters

Wakati huo huo kundi la itikadi kali Ansar-Beit al-Maqdes,lenye vituo vyake katika eneo la Sinai limedai kuhusika na mashambulio hayo.

Mashambulio haya yanajiri mnamo mkesha wa kuadhimisha miaka mitatu tangu mapinduzi yaliyomng'owa madarakani Hosni Mubarak.Maandalizi ya sherehe za kesho yanafanyika huku hali ikionekana kuwa tete na polisi na wanajeshi kutawanywa katika kila pembe ya Misri na hasa katika eneo la kati ya mji mkuu Cairo,unakokutikkana uwanja mashuhuri wa Tahrir.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman