1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schulz aachia wadhifa wa waziri wa mambo ya kigeni

Sekione Kitojo
10 Februari 2018

Martin Schulz amekataa kuchukua wadhifa wa waziri wa mambo ya kigeni katika serikali mpya itakayoongozwa na kansela Merkel ambayo baada ya kufikia makubaliano kuundwa serikali hiyo wiki hii.

https://p.dw.com/p/2sRFp
Martin Schulz verzichtet auf Außenminister-Posten
Picha: Reuters/H. Hanschke

Martin Schulz, kiongozi anayeondoka madarakani katika chama cha Social Democratic SPD nchini Ujerumani, hatachukua  wadhifa wa waziri wa mambo ya kigeni aliopewa katika serikali mpya ya Ujerumani, akisalim amri kwa mbinyo mkubwa  kutoka ndani ya chama chake kabla ya kura muhimu inayotarajiwa kupigwa na chama cha SPD kuhusiana na makubaliano yaliyofikiwa ya kuunda serikali ya mseto na kansela Angela Merkel.

Berlin Koalitionsverhandlungen von Union und SPD
Kansela Angela Merkel (kushoto) pamoja na kiongozi wa SPD Martin Schulz(kulia)Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

"Natangaza  kwamba  sitajiunga  na  serikali  ya  muungano na  wakati  huo huo napenda  kutoa  matumaini  yangu kwamba  hali  hii  itamaliza  mjadala unaonihusu  ndani  ya  chama  cha  SPD," Schulz  alisema  katika  taarifa siku ya Ijumaa(09.02.2018). Schulz amekabiliwa  na mapambano  ndani  ya SPD kwa kukubali kwake  kuchukua  wadhifa huo  wa juu  wa  kidiplomasia baada  ya  kuahidi  kwamba  hatakuwa sehemu  ya  baraza  la  mawaziri  la Merkel.

Tangazo  hilo  jana  Ijumaa  lilikuwa  ni pigo  jingine  kwa  rais  huyo  wa zamani  wa  bunge  la  Umoja  wa  Ulaya  mwenye  umri  wa  miaka  62, ambaye  siku  mbili  zilizopita alitangaza  kuwa  anajiuzulu  kuwa  kiongozi  wa chama  cha  SPD na  kumkabidhi  madaraka  hayo  kiongozi wa  wabunge wa  chama  hicho Andrea Nahles.

Hatua  hiyo  pia  inakuja  chini  ya  wiki  mbili kabla  ya  kura  itakayopigwa  na wanachama  463,723  wa  chama  cha  SPD  juu  ya  iwapo  kujiunga  ama kutojiunga  na  serikali  ya  muungano  itakayoongozwa  na  Merkel.

Koalitonsverhandlungen SPD CDU CSU
Andrea Nahles kiongozi wa wabunge wa SPD bungeniPicha: Reuters/H. Hanschke

Aliwasili  kama  shujaa

Schulz alikuwa amechaguliwa mwaka  mmoja  uliopita  kwa asilimia  100 kukiongoza  chama  hicho  cha  siasa  za  wastani za  mrengo  wa  kushoto. Aliwasili  kama  shujaa  katika medani  ya  kisiasa  nchini  humo Januari mwaka  jana, akiahidi  kwamba atamwangusha  Merkel  kama  kansela  na kukiongoza  chama  cha  SPD  katika  ushindi.

Baada  ya  kupanda  kwa  haraka  katika  uchunguzi  wa  maoni  ya  wapiga kura , uchunguzi wa  maoni  hayo  ulionesha  uungwaji  mkono  wa  kile vyombo  vya  habari  vya  Ujerumani  ilichokieleza  kuwa  ni  treni  ya  Schulz inayopungua  nguvu  kwa  haraka  kabla  ya  kukiongoza  chama  hicho kufikia  kipigo cha  kihistoria mwezi Septemba.

Baada  ya  hapo  alifanya makosa  kadhaa  makubwa ya  kisiasa. Kwanza aliondoa  kabisa  uwezekano  wa  kuunda  muungano  mpya  na  Merkel na baadaye  akakataa  kabisa  kujiunga  na  baraza  lake  la  mawaziri.

Koalitionsverhandlungen von Union und SPD  Martin Schulz
Kama shujaa wa SPD Martin Schulz aliingia madarakani kukiongoza cha hicho Januari 2017Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Miezi  michache  baadaye  alilazimika  kufuta uamuzi  wake  wa   kujiunga tena  pamoja  na  Merkel  baada  ya  kuvunjika  kwa  mazungumzo  ya kuunda  serikali  mwezi  Novemba  na  chama  cha  walinzi  wa  mazingira pamoja  na  kile  kinachopendelea  biashara  cha  Free Democrats  FDP.

Uungwaji  mkono waporomoka

Baada  ya  kupata  asilimia  20.5  tu ya  kura  katika  uchaguzi  wa  mwezi Septemba , uungwaji  mkono  wa  chama  cha  SPD ulishuka  hadi  asilimia 17, kwa  mujibu wa  uchunguzi  wa  maoni  ya  wapiga  kura  uliochapishwa wiki  hii, ambapo asilimia  72  ya  wale  walioulizwa wanapinga  Schulz kujiunga  na  serikali  mpya.

Kiongozi  muhimu  wa  kundi  la  SPD limemtaka  Sigmar Gabriel  kubakia kuwa  waziri  wa  mambo  ya  kigeni  baada  ya  Schulz kuachana  na mipango  yake  ya  kuchukua  wadhifa  huo.

Deutschland Koalitionsverhandlungen von Union und SPD | Außenminister Sigmar Gabriel
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Sigmar GabrielPicha: picture-alliance/dpa/B. Pedersen

Sigmar Gabriel anapaswa  kubakia  kuwa  waziri  wa  mambo  ya  kigeni. "Bila hivyo  sitaelewa kitu", aliandika  katika  ukurasa  wa  Twitter Johannes Kahrs, mbunge  wa  chama  cha  SPD  na  msemaji wa  kundi  la  wabunge  wa chama  hicho  bungeni, kundi  linalojulikana  kama  Seeheimer. "Uamuzi  wa Martin Schulz unapaswa  kutambuliwa  na  anastahili  heshima  ya  juu kabisa,"  alisema  Andrea Nahles.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae

Mhariri: Bruce Amani