1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marifu watasaidiwa na kamera uwanjani

6 Julai 2012

Eti mpira ulikuwa nyuma ya mstari au la? Suala hili kuu liko karibu kujibiwa..Vyombo vya kiufundi vitatumika kumaliza udhia,linasema FIFA lililowaruhusu pia wanawake wa Kiislam wajitande hijab wanapokuwa uwanjani.

https://p.dw.com/p/15SRK
Pambano kati ya Ujerumani na Uingereza katika kombe la dunia mwaka 2010Picha: picture-alliance/dpa

Taasisi ya kimataifa ya IFAB mjini Zurich imepitisha maamuzi hayo baada ya majadiliano ya muda mrefu.Taasisi hiyo inayosimamia taratibu na desturi za shirikisho la kabumbu la kimataifa imetoa kwa hivyo ruhusa ya kuwepo mfumo wa kiufundi utakaomuonyesha rifu kama mpira umekiuka mstari au la.Ni mapinduzi hayo katika sheria za dimba na shughuli za marifu ambao hadi wakati huu walikuwa wakitegemea macho yao tu pamoja na msaada wa wasaidizi wao uwanjani.

Macho yote hayo hayakutosha kama ilivyodhihirika katika michuano ya hivi karibuni ya fainali za kombe la Ulaya-UEFA,EURO 2012 nchini Poland na Ukraine pale rifu aliposhindwa kulikubali goli bayana la Ukraine dhidi ya Uengereza au katika pambano la kombe la dunia mwaka 2010 kati ya Ujerumani na Uingereza.

FIFA Sepp Blatter Torlinientechnologie
Mwenyekiti wa FIFA Sepp BlatterPicha: Reuters

Makosa kama hayo sasa yataepukwa kwa kuruhusiwa kuwepo kamera kadhaa uwanjani-kamera kama zile zinazotumika katika michuano ya Tennis ya kimataifa.Kamera hizo zitakuwa zikifuatilizia yanayotokea uwanjani na kutuma onyo kwa marifu pindi goli likiingia.

Mwenyekiti wa shirikisho la kabumbu la kimataifa FIFA,Sepp Blatter anasema:"Nnaamini wakati umewadia kupata njia za kuwasaidia marefarii.Lakini Tekonolojia ya Goli kama limeingia au la inalihusu suala hilo tu...Nnataka kusema tangu mwanzo tekonolojia hiyo haihusu kinachotokea uwanjani...."

Teknolojia hiyo itafanyiwa majaribio katika michuano ya mwezi Decemba nchini Japan,michuano ya Confederation Cup mwaka 2013 na kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil.

Uamuzi mwengine uliopitishwa na shirikisho la kabumbu la kimataifa FIFA mjini Zurich unahusiana na kuondolewa marufuku ya wanasoka wa kike kufunga vitambaa vya kichwa-Hijab.Wanachama wote wa taasisi ya Ifab wameunga mkono kanuni hiyo mpya ambayo tokea hapo ilikuwa ikitumika katika michezo mengine mfano wa Rugy au Taekwondo.

Hawk-Eye Kamera: Mojawapo ya kamera zilizofanyiwa vipimo
Hawk-Eye Kamera: Mojawapo ya kamera zilizofanyiwa vipimoPicha: dapd

Mkutano mwengine wa Ifab umepangwa kuitishwa mwezi October mwaka huu kuzungumzia vielelezo mfano rangi ya Hijab na kadhalika.Alikuwa mwanamfalme Ali Bin Al Hussein wa Jordan,makamo mwenyekiti wa shirikisho la kabumbu la kimataifa FIFA na mwanachama wa kamati kuu ya FIFA aliyeendesha kampeni kutaka marufuku hayo yabatilishwe.

Na hatimae barani Afrika orodha ya timu zitakazochuana katika mashindano ya kombe la Afrika mwaka 2013 nchini Afrika Kusini imeshabainika.Katika orodha hiyo,Vigogo wawili wa dimba Afrika magharibi,Côte d'Ivoire na Senegal watateremka pamoja uwanjani kuania nafasi ya kushiriki fainali za kombe la mataifa barani Afrika, huku mabingwa watetezi Zambia wakipangiwa kupimana nguvu na Uganda .

Mwandishi: Sten-Ziemons,Andreas/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Khelef