1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yazitaja Urusi na China kuwa kitisho kikubwa zaidi

Iddi Ssessanga
20 Januari 2018

Marekani imeziainisha China na Urusi kuwa kitisho kikubwa zaidi kwake, katika mkakati wa usalama wa taifa. Moscow imeitaja sera hiyo ya Washington kuwa ya "kibepari," huku China ikisema ni "fikra ya enzi za vita baridi."

https://p.dw.com/p/2rCTK
Kampfflugzeug US Lockheed Martin F22 Raptor
Picha: AFP/Getty Images/E. Jones

Akiwasilisha mkakati huo mpya, ambao unabainisha vipaumbele vya wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon kwa miaka kadhaa ijayo, waziri wa ulinzi Jim Mattis ameziita China na Urusi kuwa "madola yanayobadili itikadi ya kisiasa" yanayotafuta kuunda ulimwengu unaowiana na ruwaza zao za utawala wa mkono wa chuma."

Mkakati wa ulinzi wa taifa, unawakilisha ishara ya karibuni ya dhamira ya utawala wa rais Donald Trump kushughulikia changamoto kutoka Urusi na China, na wakati huo akishinikiza kuboresha uhusiano na Moscow na Beijing ili kuidhibiti Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia.

"Tutaendelea kutekeleza kampeni dhidi ya ugaidi ambayo tunashiriki wakati huu, lakini ushindani wa kuimarisha nguvu yetu, na siyo ugaidi, ndiyo kipaumbele cha usalama wetu wa taifa," Mattis alisema katika hotuba wakati akiwasilisha waraka wa mkakati huo, wa kwanza wa aina yake tangu alau mwaka 2014.

Unaweka vipaumbele kwa wizara ya ulinzi ambavyo vinatarajiwa kuakisiwa katika maombi ya matumizi ya ulinzi katika siku za usoni. Pentagon ilitoa toleo la kurasa 11 la waraka huo, ambalo halikutoa ufafanuzi juu ya mabadiliko kuelekea kukabiliana na China na Urusi yatakavyotekelezwa.

USA Verteidigungsminister James Mattis
Waziri wa ulinzi wa Marekani Jim MattisPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Martin

Mkakati wa makabiliano

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, akizungumza kupitia mkalimani katika mkutano wa waandishi habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, alisema Marekani ilikuwa inatumia mkakati wa makabiliano.

"Inasikitisha kwamba badala ya kuwa na majadiliano ya kawaida, badala ya kutumia msingi wa sheria ya kimataifa, Marekani inajitahidi kudhihirisha uongozi wao kupitia mikakati na dhana za ukabilianaji," alisema Lavrov na kuongeza kuwa Urusi iko tyari kwa mazungumzo na majadiliano kuhusu kanuni za kijeshi.

Ubalozi wa China nchini Marekani ilikosoa mkakati huo, ukisema Beijing inataka "ushikirano wa kimataifa" na siyo "udhibiti wa dunia." "Iwapo baadhi ya watu wanaiangalia dunia kupitia vita baridi, basi hatma yao ni kuangalia tu migogoro na makabiliano," alisema msemaji wa ubalozi huo katika taarifa.

Elbridge Colby, naibu katibu msaidizi anaeshughulikia mikakati na ujenzi wa jeshi, alisema wakati wa mkutano na maripota kwamba Urusi ilikuwa fidhuli zaidi katika utumiaji wa nguvu yake ya kijeshi kuliko China.

Urusi iliitwa kimabavu rasi ya Cremea kutoka kwa Ukraine mwaka 2014, na ikaingilia kijeshi nchini Syria kumsaidia mshirika wake, rais wa Syria Bashar al Assad. Lakini bado Moscow ilikuwa ikizuwiwa na rasilimali zake kiuchumi, alisema Colby.

China kwa upande mwingine ilielezwa kama inayopanda juu kiuchumi na kijeshi. China imeanzisha mkakati wa kuboresha jeshi lake, ambao Colby anasema ulikuwa "uingiliaji mkubwa wa maslahi yetu."

USS Carl Vinson (CVN-70) nukleargetriebener Flugzeugträger der United States Navy
mmoja ya meli za kubeba ndege za Marekani, USS Carl Vinson ikielekea Korea Kusini Aprili 2017.Picha: picture-alliance/Zumapress/M. Brown

Hakuna masharti ya kibajeti

Watalaamu walisifu hatua ya waraka huo kulenga vitisho vikubwa zaidi vya kiusalama kuliko orodha ndefu ya hatari katika baadhi ya mikakati ya zamani. Lakini bila kujua masharti ya kibajeti, ilikuwa vigumu kutathmini iwapo ulikuwa mkakati wa maana.

"Tusipoona hasa wapi pesa zilipo, unajua, kuna hatari kwamba huenda yote yakawa maneno tu," alisema Mara Karlin, mwanataaluma kutoka kituo cha ushauri cha Brookings na afisa mwandamizi wa usalama wakati wa utawala wa Obama.

Waraka huo pia uliiorodhesha Korea Kaskazini miongoni mwa vipaumbele vya Washington, ukigusia haja ya kuelekeza mifumo ya makombora ya kujihami ya Marekani dhidi ya kitisho kutoka Pyongyang, ambayo mbali na silaha zake za nyuklia, pia imetengeneza silaha za kibayolojia, kemikali na silaha nyingine za kawaida.

Waraka huo ulisema ushirikiano wa kimataifa utakuwa muhimu kwa jeshi la Marekani, ambalo mpaka sasa ndiyo lenye uwezo mkubwa zaidi duniani. Lakini pia ulisisitiza haja ya kugawana mzigo, katika hatua inayodhihirisha kukubaliana na ukosoaji wa Trump dhidi ya mataifa washirika, ambayo anasema wanatumia isivyo haki, hakikizo za usalama za Marekani.

Kuimarisha ushirikiano na washirika

Fiery Cross Reef Spratly Islands
China imejenga kisiwa katika bahari inayozozaniwa ya China Mashariki, ambako inatengeneza miundombinu ya kijeshi.Picha: picture alliance/AP Photo

Trump ameutaja muungano wa NATO kuwa "uliopitwa na wakati", lakini Mattis alisema Marekani itaimarisha ushirika wake wa jadi huku ikijenga ushirikiano mpya na kusikiliza zaidi mawazo ya mataifa mengine.

"Tutakuwa tayari kushawishiwa nao, kwa kutambua ukweli kwamba siyo mawazo mazuri yote hayatoki tu kwenye taifa lenye meli nyingi zaidi za kubeba ndege," alisema Mattis.

Wizara ya Pentagon inashughulikia pia waraka wa kisera kuhusu silaha za nyuklia za taifa hilo. Wakati Mattis hakuzungumzia suala hilo makhsusi, alisema kipaumbele ni kuzuwia.

"Ni namna gani tunahakikisha usalama na ufanisi wa uzuwiaji wa kinyuklia ili silaha hizo zisitumike kamwe? Ni uzuwiaji wa nyuklia, siyo uwezo wa kupigana vita isipokuwa ikiwa ndiyo siku mbaya zaidi katika historia ya taifa letu na dunia," alisema Mattis.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Yusra Buwayhid