Marekani yapuuzia maswala muhimu ya mkutano wa G8 | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.05.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Marekani yapuuzia maswala muhimu ya mkutano wa G8

Marekani inaonekena haiyatilii maanani maswala muhimu yatakayojadiliwa kwenye mkutano wa nchi zilizoendelea kiviwanda duniani za G8, uliopangwa kufanyika hapa Ujerumani mwezi ujao.

Heiligendamm mahali patakapofanyika mkutano wa G8

Heiligendamm mahali patakapofanyika mkutano wa G8

Imedhihirika wazi kwamba Marekani haina haja na makubaliano ya kimataifa juu ya sera ya mazingira dhidi ya ongezeko la joto duniani wala haionekani ikijishughulisha na sheria mpya za kudhibiti ulanguzi wa fedha. Serikali ya Marekani ilimuondoa waziri wake wa fedha, Henry Paulson, kwenye mkutano wa maandalizi wa mawaziri wa fedha wa mataifa ya G8 mjini Potsdam karibu na Berlin kati ya tarehe 18 na 19 mwezi huu.

Maelezo rasmi yaliyotolewa ni kwamba waziri Paulson alihitajika abakie mjini Washington kuandaa mazungumzo ya kiuchumi baina ya China na Marekani yatakayofanyika wiki ijayo. Lakini duru mjini Berlin zinasema sababu hasa ni hatua ya Ujerumani kuongezea nguvu sheria za kudhibiti fedha na ulanguzi. Naibu waziri wa fedha wa Marekani, Robert Kimmitt, alihudhuria kwa niaba ya bwana Paulson.

Waziri wa fedha na uchumi wa Ujerumani, Peter Steinbrueck, alieleza wasiwasi wake mnamo mwezi Machi mwaka huu kwamba fedha zinazotumiwa katika ulanguzi huenda zikaathiri maamuzi ya sera au kusababisha kuyumbamba kwa sarafu. ´Nina wasiwasi kwamba kuna fedha za ulanguzi ambazo zimeathiri shughuli kwa mfano mara tano, sita au hata saba, na kwamba wakopeshaji huenda wakaathiriwa ikiwa fedha hizo hazitaweza kutumika.

Aidha waziri Steinbrueck alisema na hapa ninamnukulu, ´Tunazungumzia kiwango kikubwa cha fedha na zinaweza kuathiri uchumi wa nchi au mfumo mzima wa fedha duniani kote,´ mwisho wa kumnukulu.

Ujerumani inaandaa mkutano wa kilele wa mataifa ya G8 utakaofanyika kati ya tarehe 6 na 8 mwezi ujao katika mji wa mapumziko wa Heiligendamm katika bahari ya Baltic, kilomita 300 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Berlin. Viongozi kutoka nchi tano kubwa zinazoendelea, zikiwemo Brazil, China, India, Mexico na Afrika Kusini, zitahudhuria mkutano huo.

Mojawapo ya mada muhimu iliyowekwa kwenye ajenda na serikali ya Ujerumani ni kuboresha ustawi wa mifumo na uwazi katika masoko ya fedha. Waziri wa kazi wa Ujeruamni, Franz Munterfering, amezifananisha fedha za ulanguzi kama nzige wanaoshambulia uchumi unaolegalega na biashara, kwa masilahi ya muda mfupi. Marekani inazitazama fedha hizo kama chombo muhimu cha kuelekeza uwekezaji wa kibinafsi kufikia kiwango cha kimataifa.

Hatua za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ni swala kubwa lililozusha tofauti kubwa baina ya serikali ya Ujerumani na Marekani. Wabunge wa Marekani wamepinga ibara kadhaa katika pendekezo la makubaliano lililotayarishwa na Ujerumani. Wanataka kukwepa lengo la kupunguza gesi zote za viwandani kwa asilimia 50 kufikia mwaka wa 2050. Pia wanapinga kuahidi kupunguza matumizi ya nishati.

Hans-Joachim Schellnhuber, mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa athari za hali ya hewa mjini Potsdam ameliambia shirika la habari la IPS kwamba tokeo kubwa la mkutano wa G8 litakuwa kuidhinishwa kwa pamoja na wajumbe wote katika mkutano huo pendekezo lililowasilishwa na serikali ya Ujerumani.

Kipengele cha tatu muhimu katika pendekezo hilo ni kudhibiti ongezeko la joto duniani kwa kiwango cha nyuzi mbili katika kipimo cha Celcius kufikia mwaka wa 2050 kama ilivyokuwa wakati wa mapinduzi ya teknolojia ya kiviwanda mnamo mwaka wa 1750. B wana Schellnhuber amesema ikiwa serikali za nchi za G8 hazitafikia makubaliano juu ya maswala kama hayo basi mkutano wa Heiligendamm utaonekana umeshindwa kuyafikia malengo yake.

 • Tarehe 21.05.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHE4
 • Tarehe 21.05.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHE4

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com