1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yamtaka Assad kusitisha kushambulia Aleppo

1 Mei 2016

Marekani jana Jumamosi (30.04.2016) imetaka majeshi ya kiongozi wa Syria Bashar al- Assad kusitisha mashambulizi dhidi ya mji wa Aleppo na kusaidia kurejesha usitishaji mapigano kwa nchi nzima.

https://p.dw.com/p/1Ifv6
Syrien Krieg Kämpe in Aleppo 2012
Mji wa Aleppo uliogawika ukidhibitiwa na waasi na serikaliPicha: picture-alliance/dpa/Maysun

Katika miito kwa mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini Syria na mjumbe wa upande wa upinzani katika majadiliano, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema umuhimu ni kuhusu usitishaji wa mapigano utakaodumu nchi nzima.

Usitishaji mapigano uliitishwa Februari mwaka huu baina ya majeshi ya Assad na muungano wa waasi lakini umeanza kuporomoka tangu wakati huo, hususan katika mji uliogawika na uliozingirwa wa Aleppo.

John Kerry
Waziri wa mambo ya kigeni wa marekani JohnKerryPicha: picture alliance/AP Images/J. L. Magana

Wiki hii, Urusi na Marekani zilikubaliana kuzishinikiza pande zinazopigana kusitisha mashambulizi yao katika majimbo ya Latakia na mashariki ya Ghouta -- lakini Aleppo iliachwa nje ya makubaliano hayo.

Mashambulizi dhidi ya Aleppo

Mashambulizi makali ya mabomu yaliendelea katika mji huo, na watu wengi wameuwawa, na Urusi imeweka wazi kwamba haina nia ya kuyalazimisha majeshi ya washirika wake kusitisha mapigano.

Wakati hatua za amani zikionekana kuwa katika wasi wasi mkubwa, Kerry anakwenda Geneva leo Jumapili (01.04.2016) kwa mazungumzo na mjumbe wa Umoja wa mataifa Ataffan de Mistura na mawaziri wa mambo ya kigeni wa Saudi Arabia na Jordan.

Syrien Luftangriff auf IS-Hochburg Raqqa
Majengo yaliyoharibiwa katika mji wa LatakiaPicha: Getty Images/AFP/A. Martins

Lakini kwanza, alitumia miito yake kusisitiza kwamba Marekani haijafikiria wazo la kwamba Aleppo iondolewe katika mpango wa usitishaji mapigano ama raia wanaweza kushambuliwa.

Katika miito kwa De Mistura na mratibu mkuu wa kamati ya juu ya upande wa upinzani kwa ajili ya majadiliano nchini Syria, Riad Hijab, Kerry ameeleza ,"wasi wasi mkubwa" juu ya Aleppo.

Syrien Friedensverhandlungen in Genf Staffan de Mistura
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de MisturaPicha: Reuters/D. Balibouse

"Waziri ameweka wazi kwamba kufikisha mwisho ghasia mjini Aleppo na kurejea kwa hali ya kawaida ya usitishaji mapigano nchi nzima ni suala lililoko katika umihumu wa juu," msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni John Kirby amesema.

Madai ya Urusi

Katika miito hiyo, Kerry alipuuzia madai ya Urusi na serikali kwamba mashambulizi mjini Aleppo yanalenga kundi la Al-Nusra Front, kundi la jihadi ambalo halimo katika mpango wa kusitisha mapigano.

"Utawala wa Assad unaendelea kuchochea mzozo huu kwa kushambulia raia wasio na hatia na makundi yanayohusika katika kupunguza uhasama -- na sio Nusra, kama utawala huo unavyodai," Kirby amesema.

Riyad Farid Hijab
Mjumbe wa majadiliano ya amani upande wa upinzani Riad HijabPicha: picture alliance/AA/M. Yalcin

"Mashambulizi kama hayo yanakwenda kinyume moja kwa moja na usitishaji mapigano na ni lazima kukomeshwa mara moja," ameeleza. "Waziri wa mambo ya kigeni amesisitiza kwamba juhudi za awali kuimarisha usitishaji wa uhasama katika majimbo ya latakia na Ghouta mashariki sio tu kwa maeneo haya mawili pekee na kwamba juhudi za kurejesha tena usitishaji huo ni lazima na ni pamoja na Aleppo.

Moja kati ya mihimili mikubwa ya kiuchumi Aleppo, umeathirika na mapigano mabaya kabisa katika mzozo huo ambao umewauwa zaidi ya watu 270,000 na wengine kwa mamilioni wamekimbia makaazi yao.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Bruce Amani